2014-05-17 11:49:11

Jengeni na kuimarisha familia moja ya binadamu!


Mama Kanisa anaendelea kufundisha kwamba, familia ni kiini cha maendeleo endelevu ya binadamu na kwamba, hakuna maendeleo ya kweli, ikiwa kama familia haitapewa kipaumbele cha kwanza. Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia mjini New York, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 20 ya Familia Duniani iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako Mwaka 1994.

Huu ni ushahidi unaoungwa mkono na waamini wa dini kuu duniani, yaani: Wayahudi, Waislam na Wakristo na kwamba, Kanisa Katoliki linapenda kuunga mkono jitihada za makusudi zinazofanywa na Umoja wa Mataifa katika mchakato wa kuwasaidia watu kujitambua kwamba, wao ni Jumuiya na wanapaswa kujenga na kuimarisha familia moja ya binadamu, kwa kuishi katika misingi ya haki, amani na utulivu.

Askofu mkuu Paglia anasema, si haba kuona kwamba, Umoja wa Mataifa unaendelea kujitaabisha kugundua umuhimu wa familia kama kiini cha maendeleo endelevu katika jamii. Kama familia ya binadamu kila mmoja ana jukumu la dhamana ambayo anapaswa kuitekeleza kwa kutambua na kuheshimu pia tofauti zilizopo!

Anasema, Familia ni kiini cha majiundo makini ya binadamu ni mahali ambapo binadamu anajifunza kupenda na kupendwa pamoja na kujisadaka kwa ajili ya jirani zake. Familia ni mahali ambapo Jamii inafundwa katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kimwili, kiutu na kijamii, ili kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya wengi.

Familia ni kiini cha mikakati na sera zote za maendeleo endelevu alikazia hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na ujumbe wake mjini Vatican. Hapa ni mahali ambapo, familia inapaswa kujifunga kibwebwe kupambana na ukosefu wa misingi ya haki, kwa kukataa sera za uchumi zisizojali na kuthamini watu; pamoja na kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo!

Askofu mkuu Paglia katika hotuba yake kwenye Umoja wa Mataifa amegusia kuhusu matatizo na changamoto zinazoikabili familia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la ndoa zinazovunjika hali ambayo inasababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa watoto.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna wimbi kubwa la watoto wanaozaliwa nje ya ndoa kwa baadhi ya watu kuendekeza "tabia ya kwenda chocho". Kuna baadhi ya watu wanaodai haki za maisha ya ndoa na familia kinyume cha maadili na utu wema. Matatizo na changamoto zote hizi iwe ni fursa ya kujenga na kuimarisha utamaduni wa mshikamano kati ya watu ili kujenga familia moja ya binadamu!







All the contents on this site are copyrighted ©.