2014-05-17 09:11:57

Ekaristi Takatifu!


Ndugu msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, tulianza maandalizi ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu kwa kukufafanulia maeneo muhimu katika historia na maisha ya Yesu. Tumekwishatembelea Bethlehemu mahali alipozaliwa Yesu, tukavuka ng'ambo ya pili ya Mto Yordan, mahali alipobatizwa na leo tuko chumba cha juu, mahali alipoweka Ekaristi Takatifu na kuwataka wanafunzi wake wawe ni watu wa huduma! RealAudioMP3
Karibu Wainjili wote wanatupatia maelezo ya karamu ya mwisho. Katika chumba kilicho juu. Wainjili wanasema kwamba karamu hiyo ilikuwa ya Agano Jipya na la milele.

Katika mazingira hayohayo ya kula Yesu akawaosha miguu wafuasi wake. Kila mwenjili anajitahidi kutoa fundisho la pekee kadiri anavyoona yeye. Hapa sisi tufuate maelezo ya mwinjili Luka. Sote tunafahamu kilichotokea siku ile ya karamu ya mwisho. Maneno ambayo Luka anayoyatumia na ambayo yabidi kuyafanyia tafakuri ni yake tunayoyasikia katika kila misa: “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Ni mwinjili Luka peke yake anayesema maneno hayo.

Lengo la Yesu lilikuwa ni kuwaalika wafuasi wake wote kumkumbuka Yeye, yaani daima kurudia kufanya kitendo hicho. Lakini zaidi pia aliwataka wamege mkate na kula ikiwa kama alama ya msingi katika imani yetu. Tendo la kumega mkate ni ufupisho wa maisha yake yote toka kuzaliwa hadi kufa kwake. “Mimi nimejifanya chakula ili kuyalisha maisha.” Ni kama vile angekuwa Bethlehemu inayotembea (mobile bakery).

Luka anataka kutuambia kuwa mnapokuwa katika karamu hii, au mnapokula chakula hiki, mnafanya uchaguzi kama wangu wa kujitoa na kujitolea. Huo ni mwaliko wa kuwa kama Kristu, wa kuwa mkate na kujigawa kwa wengine. Kwa hiyo haitaeleweka kabisa kumwona mkristu baada ya kuadhimisha ekaristi, anashindwa kusaidia wengine.

Hali halisi nyingine inayoonekana humo chumbani, wakati wa sherehe hiyo kuliibuka mabishano mazito hasahasa tungeweza kuyaita mahojiano makali kati ya mitume. Kisa walikuwa wanabishana juu ya ukuu, juu ya kuwa na heshima na cheo kati yao “ni nani anayehesabiwa kuwa mkuubwa.” Yesu akawaambia: “Wakuu wa mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Mimi niko kati yenu kama atumikaye.” Haya tena ni maneno yanayoletwa na Luka peke yake wakati huu wa mlo. Ni maneno kwa ajili ya kila mtu hasahasa yule anayejiita mkristu. Hayo ndiyo mambo yanayoharibu jumuia za kiristu siku za leo. Kazi ya mtu aliyeshiba ni kutafuta cheo.

Mahojiano hayo ya mitume hayakuishia kwao tu. Mabishano hayo yameletwa hapa kuonesha kuwa yanaweza kumpata kila mmoja katika maisha yake. Hasa kuhusu kujihoji wewe mwenyewe kuhusu kuchagua mambo. Hali kadhalika Yesu Kristu katika maisha yake hapa duniani alikabiliwa na changamoto hii ya kujihoji nafsini mwake.

Mahojiano hayo ya Yesu tutayaona baada ya karamu ya mwisho akiwa kwenye mlima wa Mizeituni. Tunaambiwa kuwa alipatwa na uchungu sana ambao katika Injili ya Kiswahili wanafasiri kuwa ni dhiki. “Yesu akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; ...akajitenga na mitume wake… huko akasali... kwa vile alikuwa katika dhiki... hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchi.”

Alikuwa katika katika dhidi au tuseme alikuwa na hali mbaya sana. Yaani ni kama hali ile anayokuwa nayo mtu kabla ya kufa. Neno hili uchungu pia limetokea katika injili ya Luka peke yake, kwa kiingereza ni "Agony". Maana halisi ya neno hilo agoni lamaanisha mapambano, mashindano au mahojiano makali. Hasa mashindano kama yale ya wanariadha. Yesu aliingia katika mashindano kama hayo.

Toka mwanzo wa maisha yake, Yesu ilimbidi aingie katika mapambano na mashindano na nguvu za shetani. Mapambano hayo hayakwisha katika vishawishi, yaani pale shetani alipomjia Yesu jangwani mara tu baada ya kubatizwa. La hasha, baada ya vishawishi vile tunasikia kuwa shetani alimwacha Yesu kwa muda. “Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.” (Lk. 4:13). Shetani anakuja tena akijua kwamba hapa sasa ni lala salama!

Hapa kuna mapambano makali ya roho yanayomdai Yesu kuwa mwaminifu na inabidi kuyashinda. Yesu anashinda! Kuonesha kwamba hayo yalikuwa ni mashindano makali, Yesu anatoka jasho, hilo kama vile jasho linalomtoka mwanariadha wakati wa mashindano. Kwa hiyo "agony" siyo uchungu bali ni mapambano, kuvutana, ukinzani, ugomvi ndani ya mtu. Mapigano yaliyoko ndani ya mtu.

Katika mapambano hayo Yesu anajiandaa kwa kujitenga na kusali. “Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba.” Anajiweka katika mahusiano na Mungu ili kuweza kuiona mipango ya Mungu. Anajiweka katika mahusiano na Mungu, ili kujua Mungu anao mpango gani kwa ajili yake. Yesu alisali sana na akawahimiza mitume wake kukesha na kusali. “Alipofika mahali pake aliwaambia: ‘ombeni kwamba msiingie majaribuni. Ondokeni, mkaombe msije mkaingia majaribuni.” Sala inamsaidia Yesu. Kisha wanafika malaika kumliwaza. Hiyo ni alama ya kuwa na mawazo ya ndani ya Mungu. Endapo alifikiria kutoroka maisha, kutoroka mateso sasa anaimarika, na kuhiari kuurekebisha ulimwengu. Kwa hiyo ili kushinda mapambano ya ndani ya mtu, yabidi kusali sana. Kuunganisha mipango yako na mipango ya Mwenyewe Mungu.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakutakia hija njema na Baba Mtakatifu Francisko huko Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014 kwa kuongozwa na kauli mbiu " Wote wawe wamoja".

Imetaraishwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.