2014-05-16 07:47:29

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili V ya Pasaka


Ninaendelea tena kuwa nawe katika kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, tukiwa tayari Dominika ya V ya Pasaka. Ujumbe wa Neno la Mungu umezama katika kuamini kina katika Bwana na kisha kutoa huduma katika jumuiya kama njia ya kukamilisha unachoamini na hivi baadaye kukuwezesha kufika mbinguni. Bwana anaenda huko kutayarisha makao ya kutosha kwa ajili yetu. RealAudioMP3

Katika somo la kwanza: (Mdo, 6:1-7), tunakutana na ongezeko la wanafunzi katika jumuiya ya kwanza, na katika ongezeko hili, kunatokea malalamiko ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu ya huduma pungufu kwa wajane. Basi Mitume wakishauriana na kusali wanaona kuwa haipendezi wao kuacha huduma ya Neno la Mungu na kuhudumu mezani.

Uamuzi unaotolewa ni kuwaambia wanajumuiya ya wa jumuiya ya kwanza wakisema chagueni kati yenu watu 7 wenye karama ya wema, wenye kujawa na roho na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili na sisi tutadumu katika kuomba na kuhudumia lile Neno”. Baada ya ushauri huo wakachaguliwa watu 7 kati yao alikuwako Stefano aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, wakasali na wakawawekea mikono na tayari wakawa mashemasi katika Kanisa.

Mpendwa msikilizaji kwa nini kunatokea malumbano na mikingamo katika Jumuiya ya kwanza? Kwa nini mwandishi anaweka jambo hili mbele yetu? Jambo la kukumbuka katika simulizi hili ni kwamba hapo mwanzo Jumuiya ilikuwa na Waebrania tu na polepole kadiri ya kazi ya kimisionari ilivyokuwa ikisonga mbele, wakajiunga hata Wayahudi wa Kiyunani ambao walikuwa wakitumia lugha ya Kigriki. Wayahudi wa Kiyunani walikuwa na mchanganyiko wa tamaduni kwa maana walikuwa wakiishi nje ya Palestina.

Waebrania ambao hawakuwa na mchanganyiko, wao waliendelea kutumia lugha ya Kiebrania kama kawaida! Basi jumuiya ilivyozidi kuongezeka vilianza kujitokeza vijidharau vya hapa na pale dhidi ya Wayahudi wa Kiyunani na hasa wajane na yatima wao kuhusiana na ugawanyaji wa mali za jumuiya! Kumbuka kuwa, tangu mwanzo walikuwa wameweka mali pamoja. Mambo haya yalianza kujitokeza baada ya miaka 3 hivi. Kilele cha dharau ni malumbano na madai ya kutaka Mitume washiriki katika kuhudumu mezani, ili kuweka haki katika maisha ya jumuiya kila siku.

Basi, shauri hilo likiwafikia Mitume, na Mitume wataamua kwa hekima ya kimungu kuwaweka wakfu watu saba kwa ajili ya huduma hiyo. Mpendwa msikilizaji hiki ndicho chanzo cha ushemasi katika Kanisa Moja,Takatifu, Katoliki na la Mitume.

Mpendwa mwana wa Mungu, tunajifunza nini katika hili? Jambo la kwanza tunajifunza kuwa tangu mwanzo Kanisa limekuwa likikumbwa na matatizo na hivi kuonesha sura mbili za Kanisa: Kanisa la wema na wadhambi. Kumbe hata hivi leo inapotokea purukushani fulani katika Kanisa tusishangae, ni hali ya mwanadamu tangu mwanzo. Wajibu na jambo la kufanya ni kusali na kuomba kwa ajili ya kupatikana suluhu kwa njia ya amani.

Jambo la pili Mitume wametupa mfano bora yaani wakati Kanisa linakua nao wanaona ni vema kushirikisha madaraka waliyokabidhiwa na Mungu kwa wengine, kwa ajili ya faida ya Taifa la Mungu. Wanapoamua jambo hili wanashirikisha jumuiya yote; huu ndio umoja wa Kanisa, ndicho Bwana anachotaka katika kuwa mchungaji mwema. Mitume wanabaki na lengo moja yaani utume wa Neno la Mungu.

Katika somo la Pili: (1Mt Petro 2:4-9) Mt Petro awaalika watu wote kumwendea Yesu Kristu jiwe hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule. Jiwe hili ndo lile jiwe kuu la pembeni ambalo Mungu ndiye mjenzi wake. Mungu anapojenga nyumba yake akisha kuweka jiwe kuu anasonga mbele akitumia mawe mengine, yaani wanadamu ambao Mt Petro anasema “Katika yeye nasi tunaitwa kuwa nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu tena tunaalikwa kutolea daima dhabihu njema zinazokubaliwa na Mungu. Ndiyo kusema Mungu, anajenga nyumba yake kwa kutumia mawe yaliyohai, yaliyojaa upendo! Hawa ni wabatizwa wanaomkubali Kristu na hivi kujenga nyumba ya kiroho yaani Kanisa la Mungu.

Mpendwa msikilizaji yafaa kujiuliza ujenzi huu ulianza lini? Kwa hakika ujenzi umeanza wakati wa ufufuko wa Bwana, maana waashi walilikataa jiwe hai na Mungu akalifanya kwa njia ya ufufuko kuwa jiwe kuu la pembeni. Jambo hili lilishaaguliwa na manabii wa kale “tazama naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule lenye heshima”. Ni kwa jinsi hiyo basi uaguzi huu umekamilika katika ufufuko wa Bwana. Mpendwa msikilizaji kwa kuwa mawe hai ya nyumba ya Mungu, Bwana anatuita daima kuachana na giza na tunaalikwa kuzitangaza fadhili zake daima kwa mataifa ili waweze kuingia katika nuru yake ya ajabu.

Katika Injili: (Yn 14:1-12) Mwinjili anaweka mbele yetu mafundisho ya Bwana aliyoyatoa katika chakula cha jioni siku iliyotangulia kuteswa kwake. Ndiyo kusema anawaachia wosia Mitume na vizazi vyote. Mmoja anaweza kuuliza hivi kwa nini Mama Kanisa ameweka somo hili baada ya Pasaka? Ni kwa sababu moja ya kawaida kwamba wosia husomwa baada ya mwenye kuandika wosia anapokuwa ameondoka duniani!

Katika mafundisho ya Bwana tunaona jinsi Bwana mwenyewe akiwatayarisha wanafunzi wake kwa ajili ya Kupaa kwake. Anasema wasifadhaike bali wawe na imani katika Mungu na yeye mwenyewe, na kisha wakumbuke anaenda kuwatayarishia makao tele ili atakapokuwepo nao wawepo. Jambo la kwenda kutayarisha makao linashangaza kidogo kwa sababu kuna mawazo kwamba tayari pamekwishaandaliwa! Ni kweli, lakini ataka kutuambia suala la kusafiri na ugumu wake linahitaji maandalizi. Kwa sababu hiyo basi, Bwana ataongeza neno akisema huko niendako mwaijua njia!

Mpendwa mwanatafakari, kwa kuwa njia na makao tunayopaswa kuyafikia ni kazi nyeti, mara moja Tomaso atasema hatujui njia! Bwana mkarimu na Mchungaji mwema anamjibu “mimi ndimi njia na ukweli na uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi”. Hili maana yake nini? Jambo hili lamaanisha lazima kufuata njia ya mapendo, njia ya mateso hadi msalabani na kisha hapo kutakuwa na ufufuko.

Kumbe, matayarisho ya makao yanaanza na msalaba wake na kisha ufufuko furaha ya milele na Baba mbinguni. Ili tuweze kupita katika njia ya Bwana tunahitaji msaada wake na ndiyo maana alisema, nitaenda na kisha nitarudi kuwachukua pamoja nami! Katika kutangaza makao, Bwana ansema nyumbani mwa Baba yake, kuna makao mengi. Bwana ataka kusema nini katika hili? Ataka kusema tukikubali kumfuasa yeye basi kuna wajibu na shughuli za kutosha kama tuonavyo leo katika Kanisa. Nyajibu hizi tunaalikwa kuzifanya kwa mapendo tukishirikiana katika raha na taabu mpaka kufikia mwisho wa nyakati na hapa ndipo kuna kumwona Baba.

Wakati Bwana anatangaza kuwa yeye ni njia ya kwenda kwa Baba, mara moja Filipo anauliza utuoneshe Baba yatutosha! Ombi hili linamwendea Bwana na hata sisi wakristu wa leo. Kwa upande wake Bwana anajibu akisema aliyeniona mimi amemwona Baba, kwa kuwa mimi ni ndani ya Baba na Baba yu ndani yangu. Kwa upande wetu tunapaswa kusema daima aliyemwona Kristu amemwona Baba. Baada ya fundisho hilo lililo gumu kwao, Bwana atawaalika kusadiki hilo na kama hawasadiki basi wasadikini kwa sababu ya kazi zenyewe!

Mpendwa, kwa kumtambua na kumjua Baba haina haja ya kujenga falsafa ya pekee bali ni kuitikia kile ambacho Bwana anasema. Ndiyo kusema inatosha tu kumtazama Kristu yaani Mwana, ambaye ni sura kamilifu ya Mungu. Inatosha kumtazama Mwana, yamaanisha na yatulazimu kusoma Neno la Mungu na kutafakari, kusikia kile anachofundisha kwa njia ya Kanisa, kupambanua namna yake ya kupenda yaani mpende adui yako, namna yake ya kukosoa kunapokuwa na shida au dhambi na mwishoni kuyashika yale yote mema aliyoliachia Kanisa la Kitume.

Mpendwa msikilizaji, katika kusadiki yaani, kuamini kuliko kina Bwana anafungamanisha zawadi, yaani anasema kama mmoja akisadiki ataweza kufanya mambo makubwa katika maisha yake. Hili ni kweli nami nasadiki.

Nakutakieni furaha tele katika Dominika hii ya Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe, ukitekeleza mapenzi yake katika maisha yako. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.