Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia anasema, maadhimisho
ya Siku ya Familia Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Mei ni fursa
muhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia, kwa kuibua
sera na mikakati itakayolinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia.
Wanadiplomasia
wanaoiwakilisha Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wanapenda kutoa mchango wao katika
kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya familia, kwa kutambua na kuthamini familia
kama chanzo cha maisha ya kijamii, rasilimali kuu katika maendeleo ya watu mintarafu
kipimo cha ubinadamu.
Waamini walei, asema Askofu mkuu Paglia wanalojukumu
la kuhakikisha kwamba, familia zao zinakuwa ni mfano bora wa kuigwa, kwa kutambua
kwamba, upendo wao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa,
kwa kujikita katika mshikamano wa dhati, ili kuonesha ile furaha ya maisha ya ndoa
inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Familia za Kikristo zinaalikwa
kwa namna ya pekee, kujibidisha kutoa malezi makini kwa watoto wao pamoja na kumwilisha
imani katika matendo kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Kimsingi anasema Askofu mkuu Paglia kwamba, familia za Kikristo
zinatumwa kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Mungu
na jirani.
Kuna haja ya kujenga na kudumisha mahusiano ya dhati kati ya kizazi
kimoja na kizazi kingine kwa njia ya mchakato wa elimu na malezi bora. Baba wa familia
wanapaswa kutekeleza dhamana yao katika malezi, lakini jambo la kusikitisha ni kuona
kwamba, kutokana na sababu mbali mbali baadhi ya wanaume wanashindwa kutekeleza utume
wao barabara hali ambayo inaweza kusababisha malezi tenge kwa watoto.
Familia
zinapaswa kujikita katika umoja na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya
familia nzima na kwamba, ndoa si mkataba wa mpito, bali ni hija ya maisha, hadi pale
kifo kitakapowatenganisha kadiri ya mapenzi ya Mungu. Familia zijitahidi kufisha ubinafsi
ili kujisadaka kwa ajili ya maendeleo yao na jamii inayowazunguka!