Imani na vita ni mambo ambayo hayawezi kupikika chungu kimoja!
Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika
safari yake ya kikazi nchini Yordan iliyomwezesha kuzungumza na viongozi mbali mbali
wa kidini nchini humo amesema kwamba, imani na vita ni mambo mawili ambayo yanasigana
sana na kamwe hayawezi kupikika chungu kimoja! Hakuna mtu yeyote anayeweza kuhalalisha
vita ya kidini, dhana ambayo imetawala sana huko Mashariki ya Kati, jambo linalosababisha
maafa makubwa kwa watu na mali zao!
Dhana ya vita ya kidini inajengeka katika
ujinga wa watu kutofahamiana vyema pamoja na kuendekeza mawazo potofu kuhusu mambo
ya dini na imani. Dini zinapaswa kuwa ni chombo kikuu cha kusaidia kuleta amani, upendo
na mshikamano kati ya watu na wala si chanzo cha vita, kinzani na migogoro ya kijamii.
Kardinali
Tauran anasema, wananchi wa mji wa Amman wanaendelea kujiandaa vyema kwa ajili ya
kumpokea Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kiekumene huko Mashariki
ya Kati. Waamini na watu wenye mapenzi mema, wanaendelea kusali na kumwombea Baba
Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume, ili waweze kumwonjesha ukarimu na
upendo, watu wana shauku kubwa ya kuonana na Baba Mtakatifu Francisko.
Kardinali
Tauran alikuwa mjini Amman kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 14 Mei 2014, kama sehemu
ya maandalizi ya hija ya kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu ambako
pia alipata nafasi ya kuweza kujadiliana na viongozi mbali mbali wa kidini kuhusu
changamoto zinazojitokeza katika sekta ya elimu huko Mashariki ya Kati. Waamini na
watu wenye mapenzi mema wanamwona Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni alama ya matumaini
kwa wananchi walioko Mashariki ya Kati.