Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro
Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawapongeza washiriki wa kongamano la kitaifa nchini
Ufilippini, lililojikita katika kuchambua umuhimu wa familia ambao unatoa fursa kwa
watu kujifunza kuishi na watu wengine licha ya tofauti zao, kwa kutambua kwamba, wote
ni wamoja!
Kongamano hili limezinduliwa hapo tarehe 13 na kufungwa rasmi tarehe
16 Mei 2014, kwa kuwashirikisha viongozi wa Kanisa na waamini walei, ambao Baba Mtakatifu
anawataka kuimarisha imani na umoja miongoni mwao chini ya usimamizi wa Khalifa wa
Mtakatifu Petro na Maaskofu wao, ili waweze kuwa kweli ni chachu ya kuyatakatifuza
malimwengu kwa uwepo endelevu wa upendo wa Kristo kati ya wanadamu.
Baba Mtakatifu
Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa kuwaweka washiriki wa kongamano hili chini
ya ulinzi wa Bikira Maria Mama wa Kanisa na Mtakatifu Yosefu pamoja na kuwapatia baraka
zake za kitume!