2014-05-15 15:50:15

Wasifu wa mabalozi wapya waliowasilisha hati zao za utambulisho mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Mei 2014 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wa Uswiss, Liberia, Ethiopia, Sudan, Jamaica, Afrika ya Kusini na India.

Balozi Pierre- Yves FUX kutoka Uswiss, alizaliwa kunako tarehe 2 Julai 1976, bado hajaoa. Alipata shahada yake ya uzamili kunako mwaka 1990 na baadaye mwaka 1994 akafuzu shahada ya uzamivu katika Falsafa. Amewahi kufanya kazi kwenye balozi za Uswiss nchini Israel, Japan, Iran na baadaye aliteuliwa kuwa Mratibu wa mgawanyo wa kazi Wizara ya mambo ya nchi za nje. Kuanzia Mwaka 2013 aliteuliwa kuwa Balozi wa Uswiss Berna ambako anaishi hadi sasa.

Balozi Margaret Ann Louise JOBSON kutoka Jamaica, alizaliwa kunako tarehe 14 Machi 1955, ameolewa na ana mtoto mmoja. Alipata shahada yake ya uzamivu kutoka katika Chuo Kikuu cha West Indies kunako mwaka 1977 na baadaye akajiendeleza katika masuala ya rasilimali watu na kufuzu katika shahada ya uzamili. Kwa miaka kadhaa alijihusisha na masuala ya tafiti; msimamizi na mshauri wa masuala ya lugha, mshauri wa UNESCO katika mkoa wa Caraib, baadaye akaajiriwa na UNDP katika nyadhifa mbali mbali. Kunako mwaka 2003 - 2013 aliteuliwa kuwa Katibu mkuu msaidizi Wizara ya mambo ya nchi za nje na biashara ya kimataifa. Mwezi Novemba 2013 aliteuliwa kuwa Balozi wa Jamaica nchini Ujerumani ambako anaishi hadi sasa.

Balozi Rudolf P. Von Ballmoos kutoka Liberia, alizaliwa tarehe 9 Julai 1960 ameoa. Alijipatia shahada ya uzamivu katika sayansi za kisiasa kunako mwaka 1983 na baadaye akajiendeleza katika masuala ya maendeleo kimataifa na kujipatia diploma kunako mwaka 1985, huko Berlin. Amewahi kufanya kazi kwenye Wizara ya Mambo ya nchi za nje Liberia kati ya mwaka 1979 - 1985; mshauri wa ubalozi nchini Uingereza na Balozi kamili nchini Ghana kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2013. Mwezi agosti 2013 aliteuliwa kuwa Balozi wa Liberia nchini Uingereza ambako anaishi hadi sasa.

Balozi Claudina Ntini Ramosepele, alizaliwa mjini Soweto kunako tarehe 11 Aprili 1957, ameolewa. Kunako mwaka 1988 alijipatia shahada ya uzamili katika uandishi wa habari kutoka Chuo kikuu cha Patrick Lumumba, Moscow, Russia. Amewahi kuwa mfanyakazi katika Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Afrika ya Kusini, Katibu wa Ubalozi wa Afrika ya Kusini nchini Canada, Mshauri wa ubalozi wa Ubalozi wa Afrika ya Kusini, nchini Uingereza, Cameroon na mkurugenzi mkuu wa masuala haki za binadamu wizarani. Mwaka 2013 akateuliwa kuwa Balozi na sasa anaishi Berna.

Balozi Nega Tsegaye Tessema kutoka Ethiopia, alizaliwa tarehe 30 Novemba 1966, ameoa na ana watoto watatu. Ni mtaalam wa uchumi kwa shahada ya uzamivu aliyojipatia kutoka Chuo kikuu cha Addis Ababa, Ethiopia na baadaye akajipatia shahada ya uzamili katika masuala ya viwanda huko Uingereza. Kwa miaka mingi alikuwa ni mtaalam wa masuala ya uchumi Wizara ya madini na nishati; mkurugenzi wa maendeleo ya viwanda, Spika, mshauri wa masuala ya kijamii katika Ofisi ya waziri mkuu, Waziri wa mambo ya nchi za nje na mwaka 2013 akateuliwa kuwa ni Balozi wa Ethiopia nchini Ufaransa anakoishi hadi sasa.

Balozi Mysore Kanpaniah Lokesh, kutoka India, alizaliwa tarehe 20 Mei 1955 ameoa na ana watoto wawili. Amewahi kuwa mfanyakazi katika Wizara ya mambo ya nchi za nje, katibu Ubalozi wa India nchini Colombia, Ubelgiji, India, Lagos, Afrika ya Kusini, USA. Kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2013 alikuwa ni Balozi wa India katika Falme za Kiarabu. Tangu Desemba 2013 anaishi Berna.

Balozi Nasreldin Ahmed Wali Abdeltif kutoka Sudan alizaliwa kumnako tarehe 8 Julai 1960 ameoa na ana watoto watatu. Ni mtaalam wa lugha kwa shahada ya uzamili aliyojipatia huko Iraq, sheria za kimataifa huko Aia na ana diplomasa ya uhusiano wa kimataifa aliyojipatia kutoka Ufaransa. Amewahi kufanya kazi Wizarani, kwenye Ubalozi wa Sudan huko Morocco, Chad, Umoja wa Mataifa, USA na mkurugenzi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa na Marekani. Kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2013 alikuwa ni Balozi nchini Rwanda. Mwaka 2013 akateuliwa kuwa Balozi wa Sudan, nchini Ufaransa anakoishi kadi sasa.







All the contents on this site are copyrighted ©.