2014-05-15 08:32:27

Wanawake simameni kidete kutetea uhai!


Waraka wa kitume wa Injili ya Uhai ulioandikwa na Mtakatifu Yohane Paulo II ni "Magna Carta" kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. RealAudioMP3

Ni changamoto kwa akina mama kujifunga kibwebwe kudumisha uhai wanaoubeba tumboni mwao, kama alivyofanya Bikira Maria, akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati ya watu wake.

Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Mama Hellen Mosha kutoka Dar es Salaam, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, kama njia ya kumuenzi Mtakatifu Yohane Paulo II aliyesimama kidete kutetea utu, heshima na uhai wa binadamu, akanonesha umuhimu wa kusamehe na kusahau kama njia ya kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataiafa. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema Mama Mosha aliwahamasisha wanawake kukataa katu katu kukumbatia utamaduni wa kifo ambao leo hii unaonekana kuwa kama "fashion" kutokana na watu kumezwa mno na malimwengu.

Mama Hellen Mosha anawasihi wanawake kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani, upendo, umoja, msamaha na mshikamano wa dhati. Amani ipate chimbuko kutoka katika undani wa mtu na kuenea katika familia, jamii na sehemu mbali mbali za maisha ya mwanadamu na kwa njia hii kama Wakristo, basi watakuwa ni chechu ya ushuhuda wa Uinjilishaji mpya!







All the contents on this site are copyrighted ©.