Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaendelea kukuletea tafakari kuhusu maeneo matakatifu
yatakatotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume na kiekumene
huko Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014. Leo tuko Yordani. Baada
ya kuzaliwa, kukimbilia Misri na kurudi toka huko, Yesu akaenda na wazazi wake kukaa
Galilaya (nyumbani kwake) kwa miaka hii 33. Kabla ya kuanza utume rasmi Yesu anaenda
Yordani kubatizwa na Yohane. Baada ya kubatizwa anaenda Kafarnaum na huko ndiko anaanza
kazi ya kuhubiri.
Ebu tuangalie
pahali hapa alipobatizwa Yesu. Kwa kawaida, Yohane mbatizaji alikuwa upande wa mashariki,
ng’ambo ya mto Yordani (Galilaya ya Upagani). Huko akawabatiza watu na kuwataka wauvuke
tena mto Yordani na kuingia Magharibi yaani nchi ya ahadi. Akawasadikisha watu kwamba
sehemu hiyo ya ubatizo ilikuwa ni sehemu halisi ambayo Musa angewaingiza watu katika
nchi ya ahadi, walipofika toka utumwani Misri.
Kwa hiyo, wale wote waliojidhani
kwamba wameingia nchi ya ahadi kumbe walikuwa bado hawajakuingia kidhati. Kwa hiyo,
Yohane akawaita watu toka Yudea warudi tena ng’ambo ya Yordani ili wabatizwe upya,
na kuingia nchi ya ahadi kama ilivyokuwa walipotoka Misri. Watu wakafika pahala hapo
palipokuwa panaitwa kwa kiyahudi Bethabàra maana yake ni mahali pa kukatisha, pahala
pa kusimama na kuangalia kwa mbali au nyumba ya Bwana.
Yaonekana kwamba, mahali
hapa alisimama Musa juu ya mlima Nebo na kutafakari nchi ya ahadi na kuona ni mahali
gani ambapo angewaingiza Wayahudi katika nchi ya ahadi. Kwa bahati mbaya yeye mwenyewe
hakuingia, badala yake Yoshua ndiye aliyeliingiza taifa katika nchi ya ahadi.
Bethbara
iko karibu sana na Ziwa la mauti. Yesu anavuka mto na kuingia nchi Takatifu kuanza
kufanya kazi ya kuhubiri na hatimaye kwenda kuteswa na kufa na kufufuka. Maelezo ya
kitaalilimungu ya mahali hapa, ni kwamba yabidi kujiruhusu kuongozwa na Yesu toka
nchi ya utumwa wa dhambi na kuingia katika nchi ya uhuru kamili wa kiroho.
Kabla
ya kubatizwa, Yesu alibadilishana kauli kidogo na Yohane aliyekuwa anakataa. Kwa hoja
kwamba kumbatiza huko kungeonesha kuwa Yesu ni mdhambi aliye mbali na Mungu. Yesu
anasema: “Kubali hivi sasa, kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote.” Hapa
Yesu anataka kumwambia Yohane kuwa anayo picha tofauti ya haki yaani, haki anayoijua
Yohane ni tofauti na haki ile ya Yesu. Haki ya Mungu anayotaka kuiingiza Yesu duniani
ni ile inayowakomboa na kuwapenda watu wote.
Yohane anakubali na kumfanya
Yesu avuke mto kwenda nchi ya ahadi yaani nchi ya uhuru. Kuingia huko kwa Yesu katika
nchi ya Ahadi (Galilaya) ni kama kule kwa kutoka Misri alikokimbili. Sasa inaamana
ya kuingia tena katika nchi ya Misri ya maisha yetu, yaani nchi ya utumwa wakaao Farao
wanaotukandamiza na kunuonea. Sasa mkombozi anatujia na kutukomboa. Yesu ni Musa mpya.
Siku
ile ya ubatizo wa Yesu pale Yordani kuna vituko vitatu vinavyoweza kutufundisha. Mosi,
tunaambiwa kwamba mara tu baada ya kubatizwa, Yesu anapotoka majini anga linafunguka.
Maelezo yake ni ya kihistoria ya mahusiano ya Mungu na binadamu. Kwamba, hapo mwanzo
karibu katika karne kama tatu hivi, Mungu alikuwa anaongea na watu kwa njia ya manabii
aliokuwa anawatuma kwao. Baadaye, akaacha kutuma manabii kwa sababu watu hawakuwa
tena wanawasikiliza. Mungu akafunga mbingu zake zilizokuwa saba. Watu wakabaki wanateseka,
wakalalamika kwamba hatuna tena nabii, itakuwaje, tutatambuaje mawazo ya Mungu kama
hakuna nabii?
Unaona sasa kwa mara nyingine Yesu anapoibuka toka majini, anga
linafunguka. Milango ya mbingu zote saba inafunguka.“Bwana ulikuwa na haki ya kutukasirikia,
maana tulitenda dhambi; Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe
u mfinyanzi wetu, sisi sote ni kazi ya mikono yako. Ukifungua mbingu tutaokoka”. (Isaya
64). Kwa ujio wa Yesu, hatuhitaji tena nabii kwani tunaye Mungu hapahapa “Emmanueli”.
Pili, tunasikia kwamba Roho ya Mungu akamshukia Yesu kama njiwa. Njiwa huyo
anatukumbusha Agano la Kale, baada ya tufani kuu, alitumwa njiwa kuangalia gharika
kuu, baadaye anarudi akiwa na tawi la mzeituni mdomoni. Njiwa ni alama ya wema, uzuri,
unyofu. Ndivyo Yesu anavyofika. Baada ya Tufani, Mungu anasema, sitaharibu tena nchi.
Hakutakuwa tena tufani itakayoharibu nchi, bali atatuma roho aliye alama ya uzima
mpya. Ndivyo sasa Yesu anapoibuka toka majini roho anaingia duniani.
Tatu,
sauti ikasikika toka mbinguni. Sauti inayomtambua Yesu. Sauti inatambua kitendo kinachofanyika.
Yaani ufunuo au epifania ya Mungu. Sasa ni wakati rasmi Mungu anapoanza shughuli yake
mpya. Kwa hiyo anapoibuka toka majini, Mungu anatamtambua kuwa ndiye mwanae mpenzi.
Mwana anafanana na wazazi wake katika sifa na thamani zote muhimu, hata namna ya kuongea
na kutenda mambo. Sisi tumwangalie mwanae anayefanana na Mungu, nasi tutakuwa na roho
hiyohiyo kwani tunafanana na Baba. Wote ni watoto wa Mungu, Yeye ni mwanae wa pekee
mpendwa kwani ameleta habari njema ya upendo, na ya haki kwa watu wote.
Tujikubali
kwamba tuko katika nchi ya utumwa mwa dhambi, tugeuke kwa kuvuka Yordani pamoja na
Yesu, tutaibuka na roho wa Bwana, aliye roho wa unyenyekevu, upole, wema, upendo na
haki. Roho atakayetupa nguvu ya kushinda majaribu ya maisha magumu ya humu jangwani
(ulimwenguni). Kisha tutaibuka kidedea katika maisha mapya pamoja na Kristu Mfufuka.
Yesu anatuagiza kutenda mambo yote kwa kufuata mfano wa maisha yake. Ndivyo
alivyowaagiza mitume wake siku ya karamu ya mwisho, “fanyeni hivi kwa kunikumbuka
mimi.” Sasa twende tukakiangalie chumba ambacho Yesu alifanya sherehe mara ya mwisho
hapa duniani na kuyatamka maneno hayo. Tafakari hii imeandaliwa na Padre Alcuin
Nyirenda, OSB.