Tamko la pamoja ili kujenga mshikamano wa kimataifa!
Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja
na Mfalme El Hassan bin Talal kutoka Amman Yordan, katika mazungumzo yao yaliyofanyika
kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 14 Mei 2014, kuzungumzia kuhusu changamoto katika elimu,
wakati huu wananchi wa Yordan wanapoendelea kujiandaa kwa ajili ya hija ya kichungaji
ya Baba Mtakatifu Francisko, kama cheche ya matumaini kwa wananchi wanaoishi huko
Mashariki ya Kati, wametoa tamko la pamoja kama njia ya kujenga na kudumisha mshikamano
duniani.
Katika sala zao wamewakumbuka wasichana waliotekwa nyara na kikundi
cha kigaidi cha Boko Haram, Kaskazini mwa Nigeria na kutaka waachiliwe mara moja,
ili waweze kujiunga tena na familia zao. Wameitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika
mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kudumisha amani katika maeneo ambayo
bado yanakabiliwa na vita pamoja kinzani za kijamii.
Viongozi hawa kwa pamoja
wamekubaliana kimsingi kwamba, familia na shule ni mahali ambapo watoto wanarithishwa
elimu, maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho na kijamii. Kumbe, kuna haja kwa
watoto kuelimishwa kuhusu utu na heshima ya binadamu; umuhimu wa kuzingatia haki msingi
hususan uhuru wa kuabudu pamoja na kujikita katika kulinda na kudumisha misingi ya
haki, amani, umoja na mshikamano kwa kupambana na: ujinga, umaskini pamoja na mmong'onyoko
wa maadili na utu wema.
Jamii zijitahidi kujenga mchakato wa upatanisho pale
ambako kumekuwepo na vita, migogoro na kinzani za kijamii, ili amani ya kweli iweze
kupatikana na kuendelezwa. Viongozi hawa wanatambua kwamba, mustakabali wa mwanadamu
na maendeleo yake uko mikononi mwa vijana wa kizazi kipya wanaopaswa kukuza kipaji
cha udadisi na ujasiri ili kuondokana na woga; kujenga na kudumisha moyo wa unyenyekevu
badala ya majivuno na kiburi; ni wajibu wa vijana kudumisha ukomavu na uhuru kwa kujiaminisha
katika uwezo wa kufikiri pamoja na kujitahidi kuwa wakweli kwa kutambua kwamba, tofauti
zilizopo ni utajiri mkubwa kati ya watu!.