2014-05-15 15:52:23

Biashara haramu ya silaha na watu kulazimika kuzikimbia nchi zao ni mambo yanayohatarisha amani na utulivu!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 15 Mei 2014 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wapya wa Uswiss, Liberia, Ethiopia, Sudan, Jamaica, Afrika ya Kusini na India, wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashukuru wakuu wa nchi kwa maamuzi yao na kwamba, anawakumbuka na kuwaombea amani na ustawi kwa nchi zao!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kwa namna ya pekee amani ambayo haina budi kufanyiwa kazi na wanadiplomasia, ili kuiwezesha familia ya binadamu kukuwa na kustawi katika haki, changamoto ya kujibidisha zaidi na zaidi kwani amani ni kati ya mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa haijawahi kuifikia, kumbe kuna haja ya kuendelea kuitafuta pamoja na kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazokinzana na amani.

Baba Mtakatifu anasema, amani na utulivu haviwezi kupatikana ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashindwa kudhibiti biashara ya silaha duniani pamoja na uhamiaji wa lazima. Biashara haramu ya silaha duniani inakwamisha juhudi za kutafuta amani na usalama kati ya watu. Vatican kwa upande wake, itaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kutafuta na kudumisha amani, kwa kufanya maamuzi mazito ili kukomesha kuenea kwa biashara ya silaha duniani.

Baba Mtakatifu anasema, maafa ya watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao ni kati ya mambo yanayokwamisha upatikanaji wa amani na utulivu duniani. Wadau mbali mbali wamejitahidi kudhibiti hali hii lakini bado hakuna mafanikio ya kuridhisha hadi sasa. Pengine umefika wakati wa kuanzisha mikakati mipaya ya kupambana na hali hii si tu wakati wa dharura, bali kwa kuwa na sera makini na zinazowajibisha na kuwashirikisha watu katika ngazi mbali mbali.

Tatizo hili lina sehemu kuu mbili, sehemu ya kwanza ni ile ineyoonesha upendo, ukarimu na mshikamano wa binadamu kwa kuwakirimia wahamiaji na wakimbizi huduma msingi na sehemu ya pili ni vikwazo wanavyowekewa wahamiaji na wakimbizi hawa katika mchakato wa kutafuta hifadhi ya maisha na kufanya kazi kwa amani: Hawa ni watu wanaohatarisha maisha yao, wanaoteswa, kudhulumiwa na kunyanyaswa utu wao na hatima yake ni kufa katika hali ya utupu jangwani au baharini.

Baba Mtakatifu anasema, baadhi ya watu wanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita na kinzani za kijamii pamoja na kuenea kwa biashara ya silaha duniani. Baba Mtakatifu anasema, haya ni madonda ya ulimwengu yanayopaswa kuponywa, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Amani na biashara ya silaha anasema Baba Mtakatifu ni mambo ambayo hayawezi kupikika katika chungu kimoja! Haki msingi za binadamu hazina budi kuheshimiwa kwa vitendo vinavyoongozwa na mshikamano wa kimataifa.

Vatican itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kweli: haki, amani na haki msingi za binadamu ziweze kuheshimiwa na kuthaminiwa na wengi. Baba Mtakatifu amewahakikishi Mabalozi wapya ushirikiano wa dhati kutoka Vatican katika utekelezaji wa majukumu na dhamana yao hapa mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.