2014-05-14 08:11:31

Wasaidieni waamini kuzima kiu ya Mungu ndani mwao!


Yesu Kristo anaendelea kuwahamasisha wafuasi wake kujikita katika upendo na kubaki wakiwa wameungana naye. Huu ni mwaliko endelevu hata baada ya kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Upadre na Miaka 25 ya Uaskofu. Ni changamoto kwa Wakristo wote, lakini maneno haya yana umuhimu wa pekee kwa wale ambao wameteuliwa kati ya watu kwa ajili ya kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika maisha ya Daraja Takatifu.

Yesu anaita na kuchagua mtu yule anayempenda kadiri ya matakwa yake, ili aweze kushiriki katika mchakato wa kuwatangazia watu Injili ya Furaha, kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja na kuwaongoza Watu wa Mungu, ili waweze kufikia utimilifu wa maisha. Mapadre wema na watakatifu ni mashahidi wanaoweza kusaidia kukuza na kukoleza wito na maisha ya Kipadre pamoja na kuendelea kuwa na imani na matumaini hata pale mwamini anapokabiliana na majanga katika maisha yake.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Agostino Vallini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, mjini Roma, tarehe 13 Mei 2014 katika maadhimisho ya Jubilee yake ya Miaka 50 ya Upadre na Miaka 25 ya Uaskofu ndani ya Kanisa Katoliki. Kwa hakika anasema Kardinali Vallini, Roho wa Bwana yu juu yake kwani amempaka mafuta ili kuwahubiria maskini Habari Njema ya Wokovu, kama Padre na Askofu, dhamana kubwa anayopaswa kuitekeleza kwa ajili ya Watu wa Mungu.

Kardinali Vallini anamshukuru Mungu kwa kumwangazia na kumwimarisha kwa karama na utume kwa Kanisa lake, kama Askofu wa Albano na Msaidizi wa Karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anasema, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, wanawataka Wakristo wote kujitosa kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwasaidia waamini waliopoteza njia na maana ya maisha ya Ukristo kugundua tena mwanga na maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; watu wana kiu ya kuelewa ukweli kuhusu Mungu na maana ya maisha ya mwanadamu, dhamana ya Padre ni kuwasaidia waamini kuzima kiu ya Mungu ndani mwao, kwa kuwatangazia kweli za Kiinjili!

Katika mazingira ya utepetevu wa imani na ukanimungu, kuna haja kwa viongozi wa Kanisa kuwafunda waamini kutembea kwa pamoja kama Jumuiya ya waamini, iliyoshikamana katika mapendo ya kidugu inayopania kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu anasema Kardinali Vallini, waoneshe jicho la upendo kwa Mapadre wao, kwa kutambua kwamba, hawa kwanza kabisa ni ndugu zao katika Kristo ni marafiki na wadau katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu.

Askofu anadhamana ya kuwalinda na kuwatunza Mapadre wake, kwa kushirikishana nao furaha na majonzi katika maisha. Jambo la msingi kwa Askofu daima atoe kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na maendeleo ya watu wake, bila kuwasahau maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Kardinali Vallini anasema, hata leo hii, Roma ina maskini wapya na wale wa zamani, kuna watu wanakabiliana na hali ngumu ya maisha; watu wanakumbana na majanga wakiwa safarini kutafuta nafuu ya maisha, kama inavyojionesha kwa watu wanaoendelea kufa maji Baharini. Kanisa haliwezi kukaa kimya na kufunga milango yake ya huruma na mapendo kwa watu hawa, kwani imani ya kweli inamwilishwa katika huduma ya mapendo kwa Mungu na jirani.

Jimbo kuu la Roma halina budi kuonesha ushuhuda kwamba, ni mji mkuu wa upendo. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia jirani zao katika upendo!







All the contents on this site are copyrighted ©.