2014-05-14 09:03:15

Uongozi ni huduma ya unyenyekevu na upendo!


Katika sehemu ya kwanza ya mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Majaalimu, walezi, Makleri na Waseminari wanaoishi na kusoma mjini Roma siku ya Jumatatu mchana, tarehe 12 Mei 2014, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican imekushirikisha kuhusu mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika majiundo ya Kipadre.

Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee majiundo ya maisha ya kiroho na kiakili; majiundo ya kijumuiya na shughuli za kichungajI, yote haya yanategemeana na kukamilishana. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa Seminari kama kitalu cha kuwafunda Mapadre pamoja na Makleri kuhakikisha kuwa wanajikita katika maisha ya: Sala, Sakramenti na tafakari ya Neno la Mungu.

Sehemu hii ya pili ya mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Wasomi wa Kanisa waliko mjini Roma, anasema kwamba, Kanisa linawahitaji viongozi wanaoweza kujisadaka katika maisha yao kwa ajili ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Kristo kwa ndugu zake, kwa kujikita katika upendo na unyenyekevu; uvumilivu na udumifu, ili Familia ya Mungu iweze kukua, kutembea, kujenga na kumshuhudia Kristo Mkombozi wa Ulimwengu.

Viongozi wa Kanisa waoneshe dira na njia ya kufuata kwa mfano na ushuhuda wa maisha yao. Ni hatari ikiwa kama viongozi wa Kanisa watageuka kuwa ni mbwa mwitu na kuanza kumezwa na malimwengu kwa kutafuta madaraka, fedha na mali. Hizi ni dhambi kuu zinazowaandama Makleri katika maisha na utume wao! Waamini si rahisi sana kumsamehe kiongozi wa Kanisa anayekumbatia fedha na mali kwa mafao yake binafsi!

Waamini hawawapendi anasema Baba Mtakatifu Francisko, Mapadre wenye dharau wasiowajali watu, wanaowaangalia maskini kama "soli ya kiatu"! Mapadre wajitaabishe kuwapenda, kuwafahamu kwa majina waamini wao na kuwasaidia kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho na kiutu! Mapadre wawe karibu na waamini wao kwa njia ya huduma, katika hali ya unyenyekevu, kiasi na sadaka.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuhakikisha kwamba, wanakuwa na uwiano mzuri wa maisha na utume wao kwa kujikita katika Sala, Ibada ya Misa Takatifu na baadaye utume unafuata baada ya kujitajirisha katika Neno la Mungu, linalokuwa ni dira na mwongozo wa siku. Padre anahitaji mapumziko kidogo ili kujichotea nguvu ya kusonga mbele katika utume wake. Ni muhimu sana kwa Mapadre kujenga utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu na kusali Rozari Takatifu. Mapadre wafanye mazoezi ya viungo, kwani ushauri anaoutoa ni ule ambao yeye mwenyewe anaufanyia kazi katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Uinjilishaji Mpya unawahitaji watu wenye uwezo wa kutolea ushuhuda amini imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Viongozi wanaotambua umuhimu wa muda na kuutumia vyema hasa katika kuandaa na kutoa mahubiri kwa waamini. Uinjilishaji mpya ni dhana inayojikita katika utakatifu wa maisha kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utukufu wa Mungu na heshima kwa binadamu kwa kujenga umoja, upendo na mshikamano wa kidugu.

Mahubiri anasema Baba Mtakatifu ni kipimo cha ukaribu wa kiongozi wa Kanisa kwa watu wake. Mahubiri yanapaswa kujikita katika Neno la Mungu ambalo ni Kisakramenti inayojikita katika Sala, Tafakari pamoja na kuifahamu hadhira inayokusudiwa, ili kuwasaidia waamini kuweza kutubu na kumwongokea Mungu. Mapadre wajifunze kutoa mahubiri yanayogusa watu na wala mimbari si mahali pa kufanyia mkutano wa hadhara. Jumuiya za Mapadre ziwe ni shule ya kusaidiana katika kuandaa mahubiri, kwani mahubiri yaliyotayarishwa na wengi yana utajiri mkubwa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utamaduni wa kukutana na watu unajengeka katika uwezo wa kusikiliza kwa makini, kujadiliana na kutafuta suluhu ya pamoja. Mapadre wajenge utamaduni wa kusikilizana, kupendana, kusaidiana na kutaabikiana wakati wa furaha na shida, wakazi wa majonzi na karaha. Kwa njia hii Mapadre wanaweza kuishi kwa furaha wito wao wa Kipadre kwa kujikita katika maisha ya kiroho, kichungaji, kiutu, kiakili na kijumuiya.

Huu ndio utajiri ambao Baba Mtakatifu amependa kuwashirikisha Makleri, Walezi na Waseminari wanaosoma kwenye vyuo na taasisi mbali mbali za kipapa zilizoko mjini Roma.

Mazungumzo haya yamehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.