Wananchi wa Sudan ya Kusini hawataweza kufanya uchaguzi mkuu hapo mwakani kama ilivyokuwa
imepangwa awali, bali uchaguzi huu unaweza kufanyika kati ya mwaka 2017 hadi mwaka
2018 kadiri hali itakavyoruhusu. Hatua hii imetangazwa na Rais Salva Kiir Mayardit
wa Sudan ya Kusini, ili kusaidia mchakato wa upatanisho wa kitaifa baada ya machafuko
ya kisiasa yaliyojitokeza nchini humo kuanzia Mwezi Desemba, 2013 na hivyo kupelekea
watu wengi kupoteza maisha na wengine kulazimika kuyakimbia makazi yao.
Tamko
hili linakuja siku chache tu tangu Serikali na wapinzani Sudan ya Kusini walipoamua
kwa pamoja kusitisha vita ili kutoa nafasi kwa wakulima kuanza kushughulikia mashamba
yao pamoja na uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kama ilivyokubalika kwenye
mkutano uliofanyika hivi karibuni mjini Addis Ababa, Ethiopia. Hata hivyo pande hizi
mbili zimekuwa zikishutumiana kwa kuvunja mkataba wa kusitisha mapigano.
Wakati
huo huo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon ameshauri kwamba, liundwe
Baraza maalum litakalochunguza kuhusu mauaji ya kivita na vitendo dhidi ya ubinadamu
vilivyofanywa wakati wa machafuko ya hali ya hewa nchini humo.