2014-05-14 15:05:42

Paji la Nguvu liwawezeshe waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kutafakari kwa kina kuhusu Mapaji ya Roho Mtakatifu yaani: hekima, akili na ushauri yanawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kuhusu Mpango wa Mungu pamoja na jitihada za kufahamu mapenzi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu, Jumatano tarehe 14 Mei 2014 ametafakari kuhusu Paji la Nguvu!

Baba Mtakatifu anasema, Paji la Nguvu linamwimarisha mwamini kutekeleza mapenzi ya Mungu licha ya mapungufu na udhaifu wa kibinadamu. Katika mfano wa mkulima na mbegu, Yesu anafundisha kwamba, mbegu ya Neno la Mungu iliyopandikizwa mioyoni mwao inaweza kukabiliana na magumu kutoka ndani na nje ya mwanadamu; mbegu hii pia inaweza kudhohofishwa na mateso pamoja na majaribu ya maisha.

Kwa njia ya Paji la Nguvu, Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuendelea kuwa waaminifu katika maisha yao licha ya magumu na majaribu wanayoweza kukabiliana nayo katika hija ya maisha. Haya ndiyo mang'amuzi na uzoefu unaooneshwa na Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia hata katika madhulumu na ushuhuda bado wanaendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa waamini wengi anasema Baba Mtakatifu Paji la Nguvu linajionesha kwa namna ya pekee kwa kudumu katika mchakato wa kutafuta utakatifu katika hali na mazingira ya maisha ya kila siku.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wanapojisikia kwamba, wamechoka na kudhohofu katika safari ya imani, wasisite kumwomba Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia Paji la Nguvu, ili kuwapatia nguvu na kuwaongoza katika maisha yao wakiwa na ari pamoja na nguvu mpya. Paji la Nguvu liwawezeshe waamini kuwa kweli ni wafuasi hodari wa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anasema, katika kipindi cha Mwezi Mei, uliotengwa maalum kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, waamini wajibidishe zaidi na zaidi kurutubisha maisha yao ya kiroho kwa Ibada kwa Bikira Maria hasa kwa kusali Rozari na kujiaminisha kwa Bikira Maria Mama wa Kanisa.

Akizungumza na waamini kutoka Mashariki ya Kati, Baba Mtakatifu anawataka kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwajalia Paji la Nguvu ili wadumu katika kutafuta mafao ya wengi, wakiwa na imani thabiti kwa Mungu hata wakati wa madhulumu, njaa, hatari au kifo. Wawe ni kielelezo cha watu wanaoshinda kishawishi cha uvivu kwa kufanya kazi; wanaojibu mabaya kwa kutenda mema na chuki kwa njia ya mapendo. Waendelee kuwa ni mashahidi thabiti wa Kristo na Injili yake kati ya watu!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujishikamanisha na Kristo katika nguvu na uaminifu kwa njia ya mwanga wa Injili yake, hasa nyakati za shida na majaribu. Anawasihi Mapadre na Watawa kuwa kweli ni alama ya furaha na mapendo kwa watu. Waamini kwa upande wao, wajitahidi kuwa ni vyombo vya amani na upatanisho; kwa kuendelea kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu wanapojitahidi kutafuta mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu amewashukuru waamini na viongozi kutoka Sardegna, Kusini mwa Italia, waliofika kwenye Katekesi yake siku ya Jumatano. Anakumbuka hija yake ya kichungaji Kisiwani humo anaendelea kuwatia moyo, ili waweze kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kisiwani hapo, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na haki msingi ya afya.







All the contents on this site are copyrighted ©.