Jina hili Bethlehemu linatokana na maneno mawili ya Kiebrania, Bet ni nyumba na Lehem
(lexem) ni mkate, kwa hiyo Beth-Lehem au bet-lexem maana yake nyumba ya mkate.
Kwa lugha
ya kigiriki cha zamani walitamka Bethleem. Ziko sehemu nyingi zenye nyumba ya mkate
mathalani Beth-lehem-ephratah, Bethlehemjudah, lakini Bethlehemu iliyokuwa kusini
karibu na Yerusalemu ndiyo iliyokuwa inaitwa Bethlehemu katika mji wa Daudi. Hapo
ndipo alipozaliwa Yesu. Ni mji ambao toka zamani wameishi wakristu wengi, lakini sasa
wanaishi pia watu wa dini mchanganyiko. Sehemu hii wanafurika wahaji na watalii wengi
sana hususani wakati wa Kipindi cha Noeli.
Kisa cha kujulikana Betlehemu kilianza
na safari ya Yosefu na Maria aliyekuwa na baraka tumboni. Walienda huko kwa ajili
ya senza. Katika pilikapilika za kutafuta mahali pa kulala mama akajifungua mtoto
wake hapo Betlehemu mji wa Daudi (Lk. 2:4). Baada ya kuzaliwa, mtoto huyo akaviringishwa
nguo za mtoto mchanga na kulazwa kwenye hori la kulishilia wanyama.
Hii ndiyo
alama ambayo malaika waliwapa maelezo wachungaji na kuwaagiza waende huko kumwona
mtoto. Malaika wakawaambia wachungaji: “Leo katika mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili
yenu, Mwokozi, ndiye Kristu Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga
amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hoi ya kulia ng’ombe.”
Kumbe yawezekana
malaika walikuwa wa kwanza kufika hapo Betlehemu na kushuhudia mambo yalivyo kabla
ya kwenda kuwahabarisha wachungaji. Tunaambiwa pia kwamba mara tu baada ya malaika
kuondoka, wachungaji nao wakaambizana wenyewe, Jamani tusiilazie damu taarifa hii
ya malaika: “Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.”
(Lk. 2:15). Baada ya kumwona mtoto wakaanza nao wakaanza kutawanya habari: “Walipomwona
(mtoto Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote waliosikia
wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” (Lk 2:27).
Malaika walipoona
utukufu umetua Bethlehemu, hawakuuacha utulie tu pale pangoni, bali wakaondoka kwenda
kuutangaza kwa wachungaji. Kwa hiyo utukufu haukuhusu pango ila unawahusu wachungaji
wanaowakilisha wanyonge wote. Wachungaji ndiyo wanaodhihirisha utukufu wa Mungu. Mungu
anajidhihirisha na kutukuzwa pale tu ambapo wanyonge, fukara wanapofurahi. Huo ni
utukufu wa Mungu. Wachungaji wanafurahi kwa sababu kutokana na hali halisi ya
unyonge wao, walijisikia kama watu waliolaaniwa, kwa hiyo hawakutegemea kabisa kupata
mawasiliano na Mungu. Kumbe amezaliwa mchungaji mwenzao, anayejua unyonge wao. Hawakujiamini
wenyewe, na mara moja wakaanza kushauriana wenyewe na kuchukua maamuzi ya kwenda kushuhudia
na baadaye kutoa ushuhuda.
“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo
alilotujulisha Bwana.” Wanaenda haraka, kushuhudia utukufu wa Mungu, ambao ni kutaka
watu wapate furaha haraka. Kwetu sisi tungetegemea kusikia mambo ya ajabu zaidi au
hata kusikia muujiza. Hakuna maelekezo zaidi, ni kama vile amezaliwa mtoto wa kawaida.
Maisha ya kawaida yanaendelea. Yesu kuwa Mungu hakutegemei muujiza wa pekee, bali
yeye mwenyewe jinsi alivyo. Yeye ni kama sisi, Mungu amekuwa mwenzetu. Anayemtegemea
Mungu wa kufanya miujiza, ujue mungu aina hiyo ni mungu wa kipagani.
Wachungaji
wanaenda Betlehemu na wanamwona mtoto aliyeviringishwa nguo. Hiyo ndiyo picha mpya
ya Mungu anayejidhihirisha kwa binadamu. Watoto waliviringishwa nguo ili kuwakinga
na baridi lakini pia inayo maana ya kidini. Mtoto ni safi, hivi huwezi kumshika tu
kwa mikono, lakini kuna maana pia muhimu ya kiroho, hasa mwinjili anaposisitiza jinsi
mtoto alivyoviringishwa nguo, hoja kubwa ni kusudi mtoto huyo aweze kuguswa, kushikwashikwa
na kubebwa na watu wote.
Aidha imeandikwa mara tatu kuwa aliwekwa katika hori
la kulishia chakula wanyama (ng’ombe). Kwa hiyo msisitizo huo unahusu chakula. Mtoto
aliviringishwa nguo, kama vile mkate unavyoviringishwa karatasi au majani na kuwekwa
kwenye nyumba ya mkate (Bethlehemu). Kwamba Yesu anadhihirishwa hapa kama mkate yaani
chakula. Malaika wanawaelekeza wachungaji kwenda kwenye nyumba ya mkate (bethlehemu)
huko watauona mkate umeviringishwa.
“Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto
mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hoi ya kulia ng’ombe.”Yesu aliishi
na kuhitimisha historia ya maisha yake hapa duniani akijionesha mwenyewe daima kuwa
ni mkate utokao mbinguni. Maisha yake yote akayatolea hadi chembe ya mwisho ya mkate.
“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.”
Wachungaji
wanapofika pangoni wakamwona Maria, Yosefu na mtoto mchanga amelala horini. Hawaoni
cha pekee zaidi. Kisha wakatoa taarifa juu ya kile walichoambiwa juu ya huyo mtoto.
“Walipomwona (mtoto Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote
waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” Nadhani watu wote walishangazwa
na taarifa hizo kwani ni Mungu aina gani anayeweza kuwatokea watu wanyonge kama wachungaji.
Kama ndivyo basi hayo ni maajabu.
Tunaambiwa jambo jingine lililotokea pale
Bethlehemu ni kuwa Maria akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Neno
kufikiri, siyo tafsiri sahihi, kwa kigiriki “sinmbalus” inamanisha kuweka mambo pamoja
na kutafakari, hasa kule ambako mmoja unapoona mambo lakini unashindwa kuyaelewa.
Maria anatulia, anaangalia, anaunganisha mambo anaweka pamoja mambo yanayomtukia.
Atakuja kufahamu atakapokuwa amesimama chini ya Msalaba.
Wachungaji wanaondoka
wakimshukuru na kumsifu Mungu – wameyaona maisha mapya. Wamemwona Mungu aliyejifanya
binadamu na kulingana na watu. Wamemwona Mungu anayejiacha kushikwashikwa na watu
wenye mikono michafu, watu wanaonuka, yaani wanyonge, maskini, wazee, wenye dhambi,
walalahoi. Watu hawa wanyonge wameona na wanafurahi, wanamshukuru na kumsifu Mungu,
kisha wanamshuhudia.
Kumbe, watu hawa wanyonge tu ndiyo wanaoweza kutambua
na kushabikia sera hii kubwa ya Mungu kujifanya mtu. Ni watu kama hawa ndiyo wanaoweza
kuwa na furaha, na kusifu na kumshukuru Mungu. Kwa wataalamu, wakuu, matajiri sera
hii haiingii akili na mioyoni mwao.
Ni muhimu hata kwetu kwamba badala ya
kujihoji na kufikri nini tufanye nini katika maisha, baada ya kumwona Kristu tubaki
tu kufurahi. Tumeona tendo kuu la upendo alilotufanyia Mungu. Huo ndiyo mwanzo wa
uchumba kati ya Mungu na binadamu, kati ya Yesu na Kanisa lake. Sisi tunafunganishwa
na Yesu katika upendo. Ndiyo mwanzo wa maisha ya upendo na ya furaha. Wanaopendana
daima wanashika simu mkononi wakisubiri ”message au kupib”, au kuitwa na mpendwa wao
ili kuongeana.
Sisi tukitaka kugundua utukufu na upendo huo wa Mungu tuanza
Bethlehemu, na kuendelea mbele hadi kwenye majitoleo kamili ya Yesu kule Kalvari.
Kwa hiyo ndugu zangu “twendeni na Papa mpaka Betlehemu” tukirudi toka huko tuwapagawaze
watu kwa tutakayoyaona. Hebu sasa tutoke Bethlehemu kuongozane na Papa hadi mto Yordani.