2014-05-14 16:04:56

NSSF miaka 50 nchini Tanzania


Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwenye ufunguzi wa nne wa wadau wa Shirika la Taifa la hifadhi ya Jamii, NSSF, tarehe 13 Mei 2014.

Nakushukuru Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF kwa kunikaribisha kufungua mkutano wa nne wa wadau wa Hifadhi ya Jamii unaoanza leo hii hapa jijini Arusha. Mkutano wa mwaka huu una umuhimu wa kipekee kwani ni fursa ya kujipongeza kwa NSSF kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964. Wakati ule ikijulikana kama Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi (NPF).

Nakupongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na wajumbe wako, Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti ya shirika pamoja na wafanyakazi wote wa NSSF kwa kazi nzuri mnayoifanya na mafanikio yaliyopatikana. Kazi yenu inaonekana na inapimika. Kutokana na kazi yenu nzuri, mnawatia moyo wanachama wenu na kuwapa imani kuwa amana zao walizowekeza kwenu ziko salama, na kwamba mko tayari kukabiliana na changamoto za leo, na za miaka 50 ijayo.

Umuhimu wa Mikutano ya Wadau

Mheshimiwa Waziri na Wadau;
Nimefurahishwa na utamaduni wenu wa kuwa na mikutano hii ya wadau kila mwaka. Ni utamaduni mzuri kwani unatoa fursa ya wadau kushiriki katika kufanya tathmini ya mwaka hadi mwaka na kupeana mrejesho wa hali ilivyo miongoni mwa wadau. Utaratibu huu unasaidia kuamsha ari ya kutekeleza malengo. Ni fursa nzuri pia ya kuhuisha malengo yenu kuendana na mabadiliko ya mazingira, maana tofauti na zamani, mabadiliko katika dunia ya sasa yanakwenda kwa kasi kubwa. Huu ni utamaduni ambao hamna budi kuudumisha na kuuendeleza.

Umuhimu wa Hifadhi ya Jamii

Mheshimiwa Waziri na wadau wa hifadhi ya jamii,
Hifadhi ya Jamii ni haki ya msingi na asili ya kila mwanadamu. Msingi wa haki yenyewe ni kulinda thamani ya utu wa binadamu. Haki hii inazingatia kuwa binadamu kwa asili ni mwanajamii, anastawi tu akiwa miongoni mwa jamii na anachangia katika maendeleo ya jamii yake, hivyo, anayo haki ya kusitiriwa na kupata hifadhi kutoka kwa jamii pale uwezo wake wa kuchangia unapokoma kutokana na uzee, ulemavu au janga lisilotazamiwa.

Hifadhi ya jamii ina faida kwa mwanajamii na jamii yenyewe. Kwa upande mmoja inamkinga mwanajamii dhidi ya kupoteza utu na thamani katika jamii, na upande wa pili inaikinga na kuinusuru jamii dhidi ya madhara ya kiuchumi na kiusalama yanayoweza kusababishwa na kuwa na jamii iliyokata tamaa.

Upo uhusiano mkubwa kati ya ustawi wa jamii na hifadhi ya jamii. Ndio maana, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu wa mwaka 1948 umetambua haki ya binadamu kupata hifadhi na Katiba ya nchi yetu ya mwaka 1977, nayo imetambua haki ya kupata hifadhi ya jamii. Katika Ibara ya 11, ibara ndogo (i). Katiba inatamka kuwa “Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kufanya kazi, haki ya kupata elimu na haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi au hali ya ulemavu, na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi...” Huu ni wajibu wetu kikatiba na tutaendelea kuutekeleza.

Hali ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii Nchini

Ndugu Wadau;
Shughuli za Hifadhi ya Jamii nchini imeanza miaka 50 iliyopita na hatua kubwa imepigwa katika kipindi hicho. Sisi sote ni mashahidi wa mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika Sekta hii. Idadi ya mifuko, wigo wa wanachama na idadi ya mafao.

Tulianza na Mfuko mmoja tu wa akiba ya wafanyakazi maaarufu kwa jina la NPF mwaka 1964. Leo tuna mifuko 6 ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF. Wigo wa wanachama wa mifuko hii nao umetanuka. Mwanzoni ilihusu watumishi walioajiriwa, tena walichaguliwa mfuko wa kujiunga nao kutokana na sekta zao lakini leo tunao wanachama kutoka sekta binafsi waliojiajiri, na wako huru kuchagua mfuko wanaoupenda kujiunga nao. Hali kadhalika, mafao yaliyokuwa yakitolewa wakati ule yalikuwa ni mafao ya pensheni tu, tena kwa mkupuo mmoja, hivi sasa kuna mafao mengi na malipo ni kwa mwezi katika uhai wote wa mwanachama. Mafao mengine hufaidisha hata wategemezi wa mwanachama.

Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya Hifadhi ya Jamii yamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa letu. Sekta hii ilichangia wastani wa asilimia 11 ya pato la taifa kwa mwaka 2011/2012. Mtaji wa mifuko hii sasa umefikia shilingi trilioni 5,242 kutoka trilioni 1.36 mwaka 2005/2006. Kutokana na hali nzuri ya ukwasi tayari mifuko hii imewekeza kiasi cha shilingi trilioni 4.4 mwaka 2012 ambapo asilimia 19 imewekezwa kwenye sekta ya ujenzi na makazi, asilimia 18 kwenye hisa na asilimia 63 kwenye amana za serikali na mikopo.

Miaka 50 kutoka Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi (NPF) hadi Mifuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Ndugu Wadau wa Hifadhi ya Jamii;
Serikali, kupitia Sheria Na. 28 ya mwaka 1997, ilianzisha Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii – NSSF, kwa kuboresha Shirika la Akiba ya Wafanyakazi (NPF) lililoanzishwa mwaka 1964. Maboresho hayo yalilenga kuongeza ubora na idadi ya mafao, kupanua wigo wa wanachama na kuisaidia Serikali katika kutoa huduma za hifadhi ya jamii. Mabadiliko haya yaliliwezesha Shirika la NSSF kutoa mafao ya pensheni ya uzeeni, urithi na ulemavu kwa wanachama wake pamoja na mafao mengine kama vile matibabu, uzazi, fidia ya kuumia kazini na gharama za mazishi.

NSSF imeendelea kukua na kuimarika mwaka hadi mwaka. Thamani ya mfuko imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.97 katika mwaka 2011/2012 hadi kufikia shilingi trilioni 2.24 mwaka 2012/2013. Kuongezeka huko kwa thamani ya mfuko kumeambatana na kuongezeka kwa mafao yanayolipwa na NSSF kutoka shilingi bilioni 178 mwaka 2011/2012 hadi shilingi bilioni 228 mwaka 2012/2013.

NSSF imekuwa mchangiaji muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu kwa kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo inayochochea ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa ajira. Tumeona manufaa ya uwekezaji wa NSSF katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, daraja la Kigamboni, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na miradi ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma na nyumba za wafanyakazi.

Inafurahisha kusikia kuwa shirika limetunukiwa cheti cha kimataifa cha utoaji wa huduma bora (ISO 9001:2008 CERTIFICATION), na hivi karibuni, kutunukiwa cheti cha utawala bora kwa kufuata kanuni bora za manunuzi na ugavi (PPRA Award). Kwa haya mawili nawapongeza sana na kuwaomba muendelee na viwango hivi vya ueledi. Maana shirika lenu ni nyeti katika uchumi wa taifa, kwa kuwa mmeaminiwa kuhifadhi na kuwekeza kwa fedha za akiba za wanachama. Umakini mkubwa unahitajika katika kuwekeza. Hamna budi kuwekeza vizuri ili mfuko uendelee kustawi na wanachama wake waendelee kupata hifadhi kutoka kwenu.

Wajibu wa Serikali: Usimamizi na Uendeshaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

Ndugu Wadau wa Hifadhi ya Jamii;
Sisi katika Serikali tunao wajibu wa msingi wa kulea mifuko hii ili iweze kustawi na kuwa endelevu. Katika kutekeleza wajibu wetu huo, na kwa kuzingatia ukuaji wa sekta yenyewe, Serikali ilianzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) mwaka 2010. Lengo kuu la kuanzishwa kwa SSRA ni kusimamia na kuratibu shughuli zote katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho katika nyanja za uwekezaji na mafao yanayotolewa kwa wanachama.

Naipongeza Wizara ya Kazi na Ajira pamoja na Msimamizi na Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia mageuzi ya kiutendaji na ya uendeshaji wa Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii. Naiomba SSRA iendelee kuboresha mazingira ya ushindani katika mifuko kwani ushindani hatimaye huleta unafuu kwa wanachama. Tumeona namna ambavyo ushindani umechochea kila Mfuko kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma na aina ya mafao yanayotolewa. Kazi kubwa waliyonayo sasa, ni kubuni mkokotoo mpya utakaosaidia kuoanisha mafao yatolewayo na mifuko hiyo.
Wito kwa NSSF na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

Ndugu wadau wa hifadhi ya jamii,
Pamoja na mchango mkubwa wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla, bado ni sehemu ndogo sana ya Watanzania wanapata kinga dhidi ya majanga kupitia Mifuko hii. Takwimu zinaonyesha kwamba kati ya Watanzania milioni 22.4 wenye uwezo wa kuzalisha kipato, waliomo katika Mifuko yote 6 si zaidi ya asilimia 6 tu. Idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya Watanzania ambao wanafanya kazi zenye kipato. Aidha idadi hii ni ndogo ikilinganishwa na wastani wa asilimia 10kwa nchi za Afrika na Kusini mwa Asia.

Kwa mujibu wa tathmini ya Sekta ya Viwanda na Biashara Ndogondogo (SMEs) ya mwaka 2013, sekta isiyo rasmi ilichangia asilimia 39.7 ya pato la taifa kwa mwaka 2010. Vile vile, ilikadiriwa kuwa zipo SMEsmilioni 3 zinazoajiri wananchi milioni 5.2. Wito wangu kwenu ni mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka maofisini kwenda kuhamasisha wananchi wengi wajiunge na mifuko hii.

Waelezeni manufaa yake, na watoeni hofu zao juu ya fikra potofu walizonazo kuhusu hifadhi ya jamii. Wengi wanaamini hifadhi ya jamii ni stahili ya wafanyakazi wajiriwa tu, tena wafanyakazi wa kipato kikubwa. Wajulisheni kuwa hivi sasa hifadhi ya jamii ni fursa huru kwa wote, wale walioajiriwa na wale waliojiajiri. Wafafanulieni wale walio kwenye sekta isiyo rasmi kuwa, utaratibu wa wao kujiunga, kuchangia na kunufaika. Waonyesheni mifano hai ya wale wakulima na wajasiriamali namna wanavyochangia na wanavyofaidika.

Natoa rai hii nikitambua kuwa wako wananchi wengi katika sekta ya kilimo na sekta isiyo rasmi ambao kwa vipato vyao wangeweza kujiunga na hifadhi ya jamii. Nawapongeza NSSF kwa mpango wake wa kuwafikia wakulima na wachimbaji wa madini ambapo hadi sasa wakulima 29,000 wachimbaji madini 7000 wamejiunga na NSSF na wanafaidika na mafao yanayotolewa.

Uzoefu wa NSSF unatuonyesha kwamba wananchi wengi wamekosa tu uelewa na taarifa sahihi. Wakumbusheni kuwa hifadhi ya jamii si jambo jipya au la kigeni, hata katika jamii zetu kabla ya kuja kwa mifumo hii rasmi, kumekuwepo na utaratibu wa jamii kujiwekea mifumo ya hifadhi ya jamii. Katika jamii zetu kumekuwa na utaratibu wa kuwahudumia wazee, wasiojiweza na watoto. Mtu hakupoteza heshima na thamani yake katika jamii kwa kuwa amepoteza uwezo wake wa kuchangia katika jamii, ama kwa kustaafu, kwa ajali au kwa kutojaaliwa uwezo wa kuchangia.

Mabadiliko ya kidunia yameifanya mifumo hiyo sasa isiweze kuhimili jukumu hilo. Hivyo, mifuko ya hifadhi ya jamii ndio mbadala na salama ya ustawi wa mtu katika dunia ya leo. Wakumbusheni kuwa shida na majanga huwafika watu wakati ambao hawajajiandaa. Hivyo, ni vyema kujisitiri kabla hujasitiriwa.

Ndugu wadau wa hifadhi ya jamii,
Ni vizuri kukumbushana pia kwamba, uhai wa mifuko ya hifadhi ya jamii unategemeana pia na uendelevu wa michango ya wanachama. Hivyo, hatuna budi pia kutoa kipaumbele katika kuelimishana juu ya umuhimu na wajibu wa waajiri kuwasilisha michango ya wanachama kwa wakati. Mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa kuhakikisha inakusanya michango ya wanachama wake bila ajizi. Wahamasisheni wanachama wa mifuko juu ya umuhimu wa kuhakikisha michango yao inawasilishwa, na inabaki katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili iwafae wakati wa matatizo na maisha ya uzeeni. Waelemisheni juu ya athari ya tabia ya sasa ya baadhi ya watumishi kuamua kushirikiana na waajiri wasio waaminifu kutopeleka michango hiyo, au baadhi ya wanachama kujitoa katika mifuko ya awali pale inapotokea amebadilisha ajira kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwingine.

Mchango wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuelekea Dira ya 2025

Ndugu Wadau wa Hifadhi ya Jamii;
Mifuko ya hifadhi ya jamii ina wajibu mkubwa wa kuchangia juhudi za Serikali katika kufikia dira yetu ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Mifuko hii imeonyesha uwezo wa kuwekeza katika sekta na miradi ya uwekezaji wa muda mrefu ambayo sekta binafsi imekuwa ikikwepa. Miradi ya aina hii kama miundombinu msingi na nishati ndio inayoweza kukwamua nchi katika umasikini, na kuleta mapinduzi kimaendeleo.

Uzoefu huu unashawishi kuwa mifuko hii sasa itazame katika sekta ya Kilimo. Kilimo ndio sekta mama ya uchumi wetu na inaajiri zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wetu, lakini ukuaji wake ni asilimia 4.4 ambayo ni chini ya kiwango kinachotakiwa cha asilimia 6 kwa mwaka kutokana na kukosa uwekezaji wa kutosha. Ndio sababu, pamoja na kasi nzuri ya ukuaji wa uchumi ya wastani wa asilimia 7, umasikini umepungua kwa asilimia 2 tu.

Umasikini huzuia pia kasi ya ukuaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii. Hivyo, uwekezaji wenu katika sekta itakayosaidia kuondoa umasikini, ni kujitengenezea pia fursa kwa mifuko yenu kupata wanachama wengi zaidi siku za usoni. Tumeshuhudia namna ambavyo uwekezaji wa pamoja wa NSSF, PPF na PSPF wa kiasi cha asilimia 45katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera kumezalisha ajira 3,500. Mbali na ajira, wataalam wanasema pia kuwa katika kila shilingi moja inayowekezwa vizuri kwenye kilimo, huzalisha faida ya hadi shilingi 3.2. Nawatia shime muangalie uwezekano wa kuwekeza katika kilimo hususan kwenye viwanda vya pembejeo za kilimo na vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao. Tukiweza kuongeza thamani na kuepuka kuuza nje mazao ghafi, tutakuwa tumewatoa Watanzania wengi kutoka kwenye umasikini na mifuko yetu itapata wanachama wengi zaidi na wenye uwezo mkubwa zaidi wa kuchangia mifuko hiyo.

Hitimisho
Ndugu wadau wa hifadhi ya jamii,
Kwa kumalizia napenda kwa mara nyingine tena kukushukuru Mheshimiwa Waziri kunialika na nikupongeze kwa namna unavyilea vizuri mifuko yetu ya hifadhi ya jamii. Nakupongeza Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF kwa uongozi wenu mzuri. Natoa pongezi nyingi kwa Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Ramadhani Dau kwa kazi nzuri unayoifanya, na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika NSSF chini ya uongozi wako. Nifikishie pongezi hizi pia menejimenti na wafanyakazi wote wa NSSF. Kazi mnayoifanya inaonekana na tuna matarajio ya kuona mengi na makubwa zaidi miaka hamsini ijayo.

Baada ya kusema hayo, napenda kutangaza kwamba mkutano huu wa nne wa wadau wa Shirika la Taifa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefunguliwa rasmi. Nawatakia mkutano mwema. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.








All the contents on this site are copyrighted ©.