2014-05-14 07:41:48

Kardinali Valllini anasherehekea Jubilee ya Miaka 50 ya Upadre na 25 ya Uaskofu!


Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam na matashi mema Kardinali Agostini Vallini, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma wakati huu anapoadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya Upadre na Miaka 25 ya Uaskofu, kielelezo makini cha uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake unaojikita katika huduma makini.

Baba Mtakatifu anamkumbushia matukio muhimu katika historia ya maisha ya familia yake, tangu alipokuwa mtoto mdogo, kwa kufariki kwa wazazi wake pamoja na madhara ya vita kuu ya pili ya dunia, mambo ambayo kwa kweli yalikuwa yanakatisha tamaa, lakini Kardinali Vallini alipiga moyo konde na kusonga mbele katika maisha na wito wake wa Kipadre.

Kardinali Vallini ameonesha weledi na majitoleo makubwa katika maisha yake kama Jaalimu wa sheria za Kanisa sanjari na utekelezaji wa majukumu yake kama Padre, kwa ajili ya kuwashirikisha waamini Injili ya Furaha, kiasi cha kuteuliwa na Mapapa waliotangulia kwa kazi maalum kama: Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Napoli, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Albano na baadaye kuteuliwa kuwa niMwenyekiti wa Mahakama kuu ya Vatican. Ni Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliyemteua kuwa Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, kielelezo cha huduma makini katika shamba la Bwana, cha kiongozi mchapa kazi anayethubutu kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapenda kumshukuru Kardinali Vallini kwa sababu amekuwa ni msaada mkubwa kwake, alipokuwa anauanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amekuwa kweli ni kielelezo cha upendo na udugu katika huduma.

Baba Mtakatifu anasema, hakuna haja kusoma litania ya huduma mbali mbali ambazo amezifanya katika maisha na utume wake, jambo la msingi kwa wakati huu anapoadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Upadre na Miaka 25 ya Uaskofu ni kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mema na ukarimu ambao Mwenyezi Mungu amemtendea.

Baba Mtakatifu Francisko anakamilisha ujumbe na matashi mema kwa Kardinali Agostino Vallini kwa kumpatia baraka zake za kitume. Anamwomba amkumbuke pia katika maisha na utume wake kwa njia ya sala!







All the contents on this site are copyrighted ©.