Katika dini nyingi iko desturi nzuri ya kiroho ya kufanya hija pahala patakatifu au
sehemu za kihistoria za dini hiyo. Hija hiyo mara nyingi hufanyika kama moja ya kuadhimisha
tukio fulani muhimu linalomhusu mtu binafsi ili kujichumia neema anayohitaji mhiji
au alhaji.
Papa pia
hufanya hija sehemu mbalimbali kama vile Lourdes, Fatima, Loreto, Namugongo, Nchi
Takatifu, nakadhalika. Hija ya Papa haiwi kwa ajili yake binafsi tu, bali hasa ni
kuchuma neema kwa ajili ya kanisa zima, pia inakuwa kwa ajili ya kuimarisha mahusiano
ya kuletesha haki, amani na upendo kati ya nchi na nchi.
Mwaka huu kuna jubilei
za dhahabu kadhaa za kikanisa zitokanazo na Mtaguso wa pili wa Vatican. Zaidi pia
ni mwaka wa 50 tangu Papa Paulo VI alipohiji nchi ya ahadi na kuzungumza na Patriaki
Anathagora wa Yerusalemu. Papa Fransis atahiji nchi ya ahadi ikiwa ni kuadhimisha
jubilei ya dhahabu ya hija hiyo ya Papa Paulo VI. Katika hija hiyo, Papa atakutana
na viongozi muhimu wa serikali na dini, atakutana pia na waumini wenzetu walioko huko.
Papa atazuru sehemu chache muhimu. Mosi, ataenda Bethlehemu kuzuru na kusali
pahala alipozaliwa Yesu. Ataenda kuzuru na kusali kando ya mto Yordani alikobatizwa
Yesu. Mwisho ataenda kuangalia chumba ambacho Yesu alikula Karamu ya Mwisho na mitume
wake. Chumba hicho ni mandhali ya mwisho aliyokuwa Yesu kabla ya kuteswa na kufa kwake.
Kwa
hiyo, Wakristu wote na watu wote wenye mapenzi mema tunaalikwa mosi, kuiombea hija
hii ya Papa, kusudi asafiri salama, aende akatuombee na kufanikisha makusudio aliyojipangia
kwa faida yake, na kwa manufaa ya kanisa zima na ulimwengu kijumla, na hatimaye arudi
salama, kusudi Mungu atukuzwe katika yote.
Pili tunaalikwa sisi sote kutanguzana
na Papa kwenda katika hija hiyo, usikose kuwepo katika msafara huo wa Baba Mtakatifu.
Kutokana na msongamano wa watu na hasa kupanda gharama ya maisha, siyo wote watafanikiwa
kwenda hiyo hija. Tunaalikwa kukata tiketi ya kiroho ambayo gharama yake ni bure sanasana
inategemea uhuru wako mwenyewe, na mkatishaji tiketi ni Roho Mtakatifu mwenyewe ambaye
hata Yeye mwenyewe ataenda kwenye hija hiyo ya awali tangu atoke huko alipokufa Yesu
Msalabani. “Akainama kichwa akaitoa Roho yake”.
Kwa watakaoenda huko kwa tiketi
ya Roho Mtakatifu, mnaalikwa kusoma ramani hii au mwongozo ufuatao, utakaowasaidia
kujua sehemu mbalimbali mtakazotembelea na kuzihiji pindi mnaongozana na Papa. Hizo
ni sehemu muhimu ambazo kulifanyika mambo makuu na mazito yahusuyo ukombozi wetu.
Katika mwongozo huu tutajaribu kuzieleza kwa kifupi sana sehemu hizo kijiografia na
kiteolojia. Tutaona pia matukio yaliyotokea sehemu hizo, yahusuhuyo Yesu au mitume
wake na sisi tunaweza kupata fundisho gani toka sehemu hiyo.
Hebu twendeni
kwanza Betlehemu alikozaliwa Yesu tuhimizane kwenda huko kwa maneno ya Wachungaji
waliokuwa wanahimizana kwenda huko baada ya kupata taarifa toka kwa malaika: “Twendeni
mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.” (Lk 2:15).