2014-05-13 15:30:05

Salam za rambi rambi kwa kifo cha Kardinali Cè!


Baba Mtakatifu ametuma salam za rambi rambi kwa Askofu mkuu Francesco Moraglia kufuatia kifo cha Kardinali Marco Cè, Patriak mstaafu wa Jimbo kuu la Venezia, Italia kilichotokea Jumatatu usiku tarehe 12 Mei 2014. Baba Mtakatifu anapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa Familia ya Mungu Jimboni Venezia na wale wote walioguswa na msiba huu.

Baba Mtakatifu anasema, Marehemu Kardinali Cè ni kiongozi aliyelihudumia Kanisa kwa furaha, kwanza kabisa Jimboni mwake Cremona alikozaliwa, Jimbo kuu la Bologna, akiwa msaidizi mkuu wa Kardinali Poma na kama kiongozi wa kiroho wa Vijana Wakatoliki Italia na baadaye kama kiongozi mwenye busara na mnyenyekevu wa Jimbo kuu la Venezia.

Baba Mtakatifu anakumbuka kwa namna ya pekee huduma za maisha ya kiroho zilizotolewa na Marehemu Kardinali Cè, katika kutangaza Neno la Mungu kwa njia ya mafungo kwa Makleri na vijana pamoja na kushiriki katika kumwilisha maadhimisho makini ya Liturujia ya Kanisa katika maisha ya waamini. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Baba Mtakatifu anapenda kuiweka roho ya Marehemu Kardinali Marco Cè huko Yerusalemu ya mbinguni. Anawapatia wote baraka zake za kitume kwa wote wanaoomboleza.

Ratiba ya mazishi ya Marehemu Kardinali Cè, inaonesha kwamba Jumatano asubuhi, waamini watafanya maandamano ili kutoa heshima zao za mwisho na mazishi yatafanyika, Jumamosi asubuhi, tarehe 17 Mei 2014 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Marko, Venezia.







All the contents on this site are copyrighted ©.