2014-05-13 08:26:33

Maisha ya Jumuiya si lelemama yataka moyo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu mchana, tarehe12 Mei 2014 amekutana na kuzungumza na Majaalimu, Walezi, Makleri na Waseminari wanaoishi na kusoma kwenye vyuo mbali mbali vya Kipapa mjini Roma. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee anasema anawakumbuka na kuwaombea wananchi wa Ukraine ambao kwa sasa wanakabiliana na hali ngumu katika maisha yao kutokana na machafuko ya kisiasa na kinzani za kijamii zinazoendelea nchini humo.

Baba Mtakatifu anasema, yuko karibu nao kwa njia ya sala na sadaka yake! Baba Mtakatifu anasema, hata Wakristo sehemu mbali mbali za dunia bado wanaendelea kudhulumiwa na kuteswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu katika mazungumzo na Jumuiya ya wasomi wa Kanisa mjini Roma, alitumia mtindo wa maswali na majibu kama njia ya kuzungumza nao ili kushirikishana mawazo, uzoefu na mang'amuzi katika maisha na utume wa Kanisa. Jambo la msingi amekazia umuhimu wa majiundo makini kwa Makleri na kuwa tayari kurudi kuyahudumia majimbo na mashirika yao kwa ari na moyo mkuu. Katika malezi, mambo makuu manne hayana budi kuzingatiwa anasema Baba Mtakatifu.

Mambo haya ni: majiundo ya maisha ya kiroho na kiakili; majiundo ya maisha ya kijumuiya na hatimaye, majiundo ya shughuli za kichungaji, mambo ambayo yanategemeana na kukamilishana. Baba Mtakatifu anasema, haya ni maisha yanayojikita katika Ibada ya Misa Takatifu, Sala na tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kumwilishwa katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji, kwa kutambua kwamba, wao wameitwa kwanza kabisa kuwa ni Mapadre.

Baba Mtakatifu anasema, inasikitisha kumwona Padre ambaye amezama kwenye vitabu na kusahau mambo mengine muhimu katika maisha na wito wa kipadre. Hii ni hatari kubwa. Makleri wajitahidi kulifahamu Kanisa kwa njia ya majiundo yao darasani, katika sala na tafakari ya Neno la Mungu, kwani uelewa makini wa Kanisa unatolewa na Mama Kanisa mwenyewe na wala si vinginevyo! Kutolifahamu Kanisa barabara kutawafanya watu waishi kwenye ombwe!

Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa Seminari kama kitalu cha majiundo ya maisha na wito wa Kipadre ndani ya Kanisa. Anatambua fika matatizo, changamoto na fursa zilizoko Seminarini, kwani hii ni Jumuiya makini ya majiundo ya Kipadre. Ni Jumuiya inayotembea na kuimarishana katika fadhila za Kikristo. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, maisha ya Jumuiya si lele mama yataka kweli moyo! Maisha haya ni sawa na "Jehanamu" kama ambavyo aliwahi kusema Mtakatifu mmoja na wala si Paradiso mahali pa "kula kuku kwa mrija"! Kwani hapa ni mahali pa toba na ukuaji na wongofu wa ndani. Ni mahali pa kuheshimiana na kusaidiana katika imani, mapendo na matumaini, kwa kuishi kidugu.

Baba Mtakatifu anasema "majungu si mtaji" katika maisha ya Kijumuiya, vinginevyo wangetajirika wengi. Makleri wajenge ujasiri wa kuambiana ukweli, kwani majungu ni sumu ya maisha ya Kijumuiya. Makleri wawe na ujasiri wa kujenga hoja na kusimamia ukweli hata kama una uma kiasi gani; wajenge utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na upendo, daima wakitafuta kujenga na kuimarisha ukweli na umoja wa Jumuiya. Kamwe wasijenge ngome za kutaka kulipizana kisasi, bali wajielekeze zaidi katika sala ili kujenga mchakato wa kusamehe, kwani kukosa na kukosehana ni sehemu ya ubinadamu, lakini kusamehe ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Makleri kukesha na kuendelea kupapalia maisha na wito wao wa Kipadre, kwani mahali ambapo kuna hazina yao, hapo kwa hakika utakuwepo moyo wao. Katika mashaka na wasi wasi, wamkimbilie Bikira Maria, Mama wa shauri jema, ili aweze kuwafunika kwa mbawa zake za Kimama. Makleri wajenge utamaduni wa kuchunguza dhamiri zao kila siku kama sehemu ya mchakato wa kupima maisha na wito wao wa Kipadre.

Pale inapobidi, wasisite kupata ushauri kutoka kwa wataalam. Sala ni jambo muhimu kwa ajili ya kuhitimisha siku katika maisha na wito wa kipadre, lakini uzoefu anasema Baba Mtakatifu Francisko unaonesha kwamba, wengi wanahitimisha siku yao kwa kuangalia Luninga!

Tukutane tena katika sehemu ya pili ya mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Wasomi kutoka vyuo vikuu vya kipapa mjini Roma.
Mazungumzo haya yamehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.