Mawasiliano kwa ajili ya huduma ya utamaduni wa kweli wa kukutana ndiyo kauli mbiu
itakayoongoza semina ya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM, kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Mei 2014.
Askofu mkuu
Cladio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii katika ujumbe
wake kwa njia ya video anasema, bila shaka mwelekeo wa semina hii hautajikita katika
suala la teknolojia peke yake, lakini kama sehemu ya tafakari ya kina inayofanywa
na Mama Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika maboresho ya matumizi ya njia
za mawasiliano ya jamii.
Maaskofu wanapaswa kutambua kwamba, wanadhamana na
wajibu nyeti katika matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya Jamii. Baba Mtakatifu
Francisko anaendelea kuwachangamotisha viongozi wa Kanisa kuwa mstari wa mbele katika
matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya Jamii, ili kuhakikisha kwamba, Injili
ya Furaha inatangazwa hadi pembezoni mwa maisha ya watu ndani ya Jamii husika.
Mawasiliano
yanapaswa kuwa ni huduma inayowawezesha watu kukutana na kushirikishana mang’amuzi
na vipaumbele vya maisha. Semina hii itawashirikisha Maaskofu mabingwa katika masuala
ya njia za mawasiliano ya kijamii kutoka Hispania na Amerika ya Kusini.
Askofu
mkuu Claudio Maria Celli anawatakia kheri na baraka tele Maaskofu Katoliki Amerika
ya Kusini, katika mchakato wa kuendeleza utajiri mkubwa ambao maendeleo ya sayansi
na teknolojia unatoa kwa Mama Kanisa katika jitihada zake za kichungaji za kutangaza
Ufalme wa Mungu na Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.