2014-05-12 10:35:04

Rais Uhuru, watu nchini Kenya wanakufa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limeitaka Serikali ya Kenya kusimama kidete kulinda na kutetea maisha ya wananchi wake, kwani katika siku za hivi karibuni watu wengi wamepoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi, ajali barabarani, ujambazi na unyang'anyi, baadhi ya watu kujinyonga hadi kufa, ulevi wa kupindukia na baa la njaa kwa baadhi ya watu.

Hii inatokana na kuzagaa kwa silaha za moto kiasi cha kutishia amani na usalama kwa Nchi ya Kenya ambayo kwa miaka mingi ilikuwa ni inajivunia amani na utulivu, lakini sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa vitendo vya kigaidi na ukosefu wa: usalama, amani na utulivu.

Kamwe, Kanisa haliwezi kukubali kuona vitendo hivi vinaendelea katika Jamii, changamoto kwa kila raia wa Kenya kushirikiana kikamilifu na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuweza kutokomeza vitendo vinavyochafua hali ya ulinzi na usalama nchini humo. Ni mwaliko kwa wanasiasa na viongozi wa Serikali kuwa macho na kauli zao, ili zisiwe ni chanzo cha kuwagawa wananchi, kwani kwa sasa kipaumbele cha kwanza ni kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, ambaye pia amelaani vitendo vya rushwa na ufisadi kuanzia katika ngazi ya taifa hadi kwenye vitongoji. Maaskofu wanasema, watu wanataka kuona maendeleo, lakini wapi! Jambo la kushangaza ni viongozi Serikalini kujiongezea mishahara na marupurupu manono, wakati wananchi wa kawaida wanaendelea kuogelea katika umaskini na hali ya kukata tamaa.

Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yapewe msukumo wa pekee katika mikakati ya Serikali ya Kenya. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka wananchi wote kuungana kwa pamoja ili kupambana kufa na kupona dhidi ya rushwa na ufisadi; viongozi walioko madarakani waache mchezo mchafu wa uchu wa mali na madaraka na badala yake waanze kujielekeza katika utoaji huduma kwa wananchi wa Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.