2014-05-12 11:08:11

Kweli Serikali imeshindwa kufahamu mahali walipofichwa wasichana 200?


Kardinali John Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria anaitaka Serikali kuonesha kwa vitendo juhudi za kutaka kuwaokoa wasichana zaidi ya 200 waliotekwa nyara na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram na kwamba, kitendo hiki ni fedheha kubwa kwa Serikali ya Nigeria.

Wananchi wanashindwa kuelewa kile kinachoendelea nchini Nigeria, kiasi cha kutoweza kutambua mahali walipo wasichana hawa 200?. Wananchi wa Nigeria pamoja na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kusali kwa ajili ya kuachiliwa huru kwa wasichana hawa ambao wana umri kati ya miaka 16 hadi 18.

Viongozi wa kidini nchini Nigeria wanaendelea kushirikiana kwa pamoja, ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa. Ni jukumu la Serikali ya Nigeria kupambanua mambo msingi yanayopelekea vitendo vya kigaidi na utekaji nyara kuendelea kushamiri licha ya sera na mikakati madhubuti inayoendelea kutolewa na Serikali kuu! Jambo la msingi ni kupambana na umaskini wa hali na kipato; kusimama kidete kupinga rushwa, ufisadi na utawala mbovu, ili kuwaanza mchakato wa ujenzi wa haki na amani, udugu na mshikamano.







All the contents on this site are copyrighted ©.