Jeshi la Polisi nchini Kenya lifanyiwe marekebisho makubwa!
Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya anasema kwamba, kuna haja ya kuharakisha mageuzi katika mfumo na utendaji
wa Jeshi la Polisi nchini Kenya, ili Jeshi la Polisi liweze kuwajibika zaidi kwa wananchi,
kwa kulinda maisha na mali zao. Ni wajibu wa raia kutambua kwamba, ulinzi na usalama
uko mikononi mwao na kwamba, wanapaswa kushirikiana kikamilifu na Jeshi la Polisi,
ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.
Askofu
mkuu Okoth anasema, wananchi wa Kenya kwa sasa wanaishi katika mazingira hatarishi
na wasi wasi mkubwa kutokana na ukosefu wa amani na utulivu, kwani kuna silaha nyingi
za moto ambazo zimezagaa mikononi mwa wananchi. Ni wajibu wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana
na wananchi kuhakikisha kwamba, silaha hizi zinadhibitiwa, ili watu waweze kuwa na
uhakika wa usalama wa maisha na mali zao.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya
linasema, kuna haja kwa Serikali kuimarisha kikosi cha intelijensia kitaifa, ili kukabiliana
na matukio ambayo yanataka kuvuruga misingi ya haki, amani na utulivu nchini Kenya.
Jeshi la Polisi linapaswa kuwa makini kutokana na madhara ya ulevi wa kupindukia ambao
umesababisha katika siku za hivi karibuni, watu wengi kupoteza maisha au kulazwa hospitalini,
huko Nairobi.