Haki, amani, mazingira na mshikamano kati ya binadamu!
Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anthony, kilichoko mjini Roma, kuanzia tarehe
29 Aprili hadi tarehe 9 Mei, 2014 kimekuwa kikiendesha kozi maalum kuhusu haki, amani
na ukamilifu wa uumbaji. Ni kozi ambayo imewashirikisha Watawa wa Shirika la Mtakatifu
Francisko wa Assisi ambao utunzaji wa mazingira ni sehemu ya karama na maisha yao
ya kiroho. Wanafunzi na wadau mbali mbali wa mazingira wamehudhuria kwa wingi.
Takwimu za
Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 232 ambao wamelazimika
kuzihama nchi zao kwa sababu mbali mbali, moja ya sababu hizi ni kutafuta ajira katika
medani za kimataifa. Kuna watu millioni 16, kati yao kuna watu wanaotafuta hifadhi
ya kisiasa; kuna watu millioni 28. 8 ambao hawana makazi maalum kutokana na vita na
kinzani za kijamii; watu millioni 15 wamejikuta wanakuwa ni wakimbizi kutokana na
madhara ya maafa asilia na wengine millioni 15 ni wale wanaojikuta wametumbukia katika
kundi la wakimbizi na wahamiaji kutoka na sakata la maendeleo ya mwanadamu!
Padre
Gabriele Bentoglio, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati
akitoa muhadhara Chuoni hapo anasema, makundi yote haya yanahitaji huduma maalum ya
kichungaji sanjari na kusimama kidete kupambana kufa na kupona na watu wanaojihusisha
na biashara haramu ya binadamu. Kanisa litaendelea kuweka mbinu mkakati wa kusaidia
kusitisha biashara hii pamoja na kuwasaidia waathirika.
Makanisa mahalia hayana
budi kuliangalia tatizo la wakimbizi na wahamiaji ili kujiwekea mikakati ya kichungaji,
kwa kukuza na kudumisha majadiliano, kwa kuonesha ushuhuda wa upendo, utu na heshima
ya binadamu; kwa kuwajengea uwezo wakimbizi na wahamiaji, ili waweze kujitegemea pamoja
na kujenga mazingira bora zaidi yanaonesha ukarimu, mshikamano na umoja wa kidugu;
mambo ambayo yanapaswa kuendelezwa na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema.
Mama
Kanisa hana budi kujielekeza zaidi katika majadiliano na wadau mbali mbali ili kupata
suluhu ya kinzani za kijamii, kisiasa na kikabila ambazo zimepelekea mauaji ya kimbari
pamoja na kuibua makundi makubwa ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum.
Uhuru wa kidini ni jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa, kwani migogoro
na kinzani za kidini zimekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Watu
wengi kwa sasa wanahofu na wala hawana uhakika wa usalama wa maisha yao kutokana na
fujo pamoja na vurugu za kidini sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa bado linahamasishwa
kujielekeza zaidi katika utamadunisho, ili kweli Injili ya Kristo iweze kupewa msukumo
wa pekee katika maisha na vipaumbele vya waamini.
Ikumbukwe kwamba, imani
ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, hata waamini wanahamasishwa kuwashirikisha
wengine zawadi hii, kama ilivyo hata kwa wahamiaji na wakimbizi, ambao wamesaidia
kuleta ari na mwamko wa maisha ya kiroho katika nchi zile ambazo wamepokelewa kwa
heshima na taadhima.
Padre Bentoglio anasema, Kanisa haliangalii makundi makubwa
ya wahamiaji na wakimbizi wala idadi yao, katika masuala kama haya, Kanisa linaona
kwa kila mkimbizi na mhamiaji ile sura na mfano wa Mungu, changamoto na mwaliko wa
kuwaheshimu na kuwathamini wakimbizi na wahamiaji kama binadamu, wanaopaswa kuheshimiwa
na kupewa haki zao msingi. Kila mtu anawajibika kutekeleza wajibu wake katika kudhibiti,
kulinda na kuwatetea wakimbizi na wahamiaji.
Padre Gabriele Bentoglio amewapongeza
waamini walei wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji
wanaotafuta nafuu ya maisha ugenini. Hili ni kundi ambalo linapaswa kusaidiwa kukuza
ukarimu huu kwa njia ya majiundo makini na endelevu. Kanisa liangalie uwezekano wa
kuwaandaa wachungaji watakaojikita katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, kwa
kuwapatia elimu na majiundo kamili.