Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, TUMSIFU YESU KRISTO.
Tukiwa bado
shangweni mwa Paska, tunaendelea kumwomba Kristo Masiha, atujalie amani siku zote,
atuimarishie utashi wetu ili tudumu katika heri ya Upasaka. Katika mafundisho yake
ya Juma, Baba Mtakatifu Fransisko alitufundisha akituhimiza tusitafute uzima katika
mambo mafu; kwa mwangwi wa neno lile ‘kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu’.
Mpendwa
Msikilizaji, kipindi chote cha kwaresma, tulikuwa tunajibidisha kurekebisha mwenendo
wetu na kukuza zaidi maisha ya fadhila. Ikumbukwe kwamba ‘hatukuwa likizo ya dhambi’
na sasa ndiyo tunafungulia, hapana. Tulikuwa tunajijenga ili tupande kiwango katika
maisha yetu ya imani na maadili na katika juhudi yetu ya kumwendea Mungu.
Katika
kipindi hiki, tuendelee kuhimizana juu ya kuongeza bidii ya kubaki katika wema wa
Pasaka. Mara nyingi huwa tunaitafuta amani kwa juhudi sana, ila kwa bahati mbaya yetu,
huwa tunasahau kuitunza. Vipindi vilivyopita tulitafakari kuwa maisha ya dhambi ndiyo
kaburi letu. Kwa neema ya Mungu na kwa nguvu ya Yesu Mfufuka anayetushirikisha uzima
wake, sisi nasi tumetoka katika kaburi hilo la dhambi na mauti. Sasa tunaalikwa kuongeza
jitihada za kubaki katika uzima huu mpya, uzima wa kimungu tunaoupata katika Kristo.
Hutokea
mara nyingi sana, wengi wetu tunafanya jitihada za makusudi za kurudi makaburini.
Ni kama tulikuwa likizo ya dhambi, sasa likizo imekwisha tunarudi tena madhambini
kwetu. Katika kipindi kile tulichambua makaburi yetu kama vile, uzembe katika imani,
uvivu, magomvi na mafarakano, nk. Tukasema tumefufuka pamoja na Kristo, hatupo huko
tena. Sisi tu hai, hatupatikani tena kati ya wafu. Tuna uzima wa kimunngu, tuna imani
na amani katika Yesu, tuna matumaini tele na tumejawa upendo kwa Mungu na jirani.
Hayo yote ndiyo hali ya neema.
Huwa inakuwaje basi katika maisha yetu, tukatafuta
amani, tunakuwa nayo wiki mmoja au muda mfupi, baadaye fujo zinarudi kwa kasi mpya
kana kwamba zilikuwa likizo vile. Hata katika familia zetu, tutatafuta maelewano mema,
tutaombana misamaha na kusameheana na hali njema inaonekana kwa muda fulani tu, baadaye
tunarudi katika ubaya uleule. Katika juhudi za kujirekebisha, tunatafuta kuwa watu
wema, kisha tunakuwa wema kwa muda mfupi halafu baadaye tunarudia ukorofi kwa spidi
kali, na kuwa wakorofi zaidi kuliko pale mwanzoni. Kufanya hivyo ndiyo kujirudisha
makaburini. Je, inawezekana kujijenga katika wema na kuendelea kuwa mwema zaidi? Hali
yoyote njema, hujengwa, hutunzwa na huendelezwa.
Mpendwa msikilizaji, ikumbukwe
kwamba, daima tunapigana na nguvu ya uovu iliyomo ndani mwetu. Tunataka tushinde kabisa
hila za mwovu ambaye daima anatusukumia makaburini na anapenda kutuvutia makaburini
daima. Tukiwa katika hali njema, tukiwa jirani na Mungu, mwovu hapendi. Tufanyeje
basi?
Kwanza kabisa tutambue kuwa, zoezi la kiroho la Kwaresma, ni wajibu wa
nyakati zote. Tujibidishe daima katika matendo ya upendo, sadaka na majitoleo mbalimbali.
Daima tujibidishe kuwa watu wa sala, watu wa kufunga na kutoa sadaka kuwapa maskini.
Masikini hawapo kipindi cha Kwaresma tu. Wapo nyakati zote. Baba Mtakatifu katika
mafundisho yake, daima ametualika kufumbua maacho kumtazama jirani mhitaji.
Daima
tunapiga mbio bila kuchoka, kujitahidi kuvitawala vilema vyetu vya roho na mwili.
Vilema vyetu visipotawaliwa, vitatutesa na kutuweka katika hali ya u-kaburi-kaburi
daima. Katika moja ya tafakari tulisema, kila mmoja anajua kaburi lake ni nini na
liko wapi. Tupo ambao kaburi letu ni kilema cha wivu. Tuna wivu uliopitiliza. Tupo
ambapo kaburi letu kubwa ni uwongo, umbea, uzushi na majungu. Haipiti siku bila kusema
uwongo. Tupo ambao kaburi letu ni wizi, udokozi na dhuluma. Tupo ambao kaburi letu
ni ukorofi, daima tunakuwa wakorofi wa kuzua fujo kati ya watu, kila ulipo lazima
watu wakose raha. Tupo ambao kaburi letu ni uvivu, madeni na njaa. Tupo ambao kaburi
letu ni kukosa imani kwa Mungu, nk.
Baada ya zoezi lote la Kwaresma, sasa
‘tumefufuka pamoja na Kristo, na tutafute yaliyo juu Kristo aliko...(Kol. 3:1-17).
Tupende kujiweka karibu na Mungu kwa njia ya sala, kusoma, kuyajifunza na kuongozwa
na maandiko matakatifu. Tujijenge katika dhamiri yenye hofu ya Mungu daima, ili tusitumikishwe
na kongwa la yule mwovu. Ni kwa njia hiyo tu, tunaweza kubaki katika furaha na mng’ao
wa kipasaka. Na mng’ao wa utukufu wa kipasaka, unatujaza tumaini jema, furaha, amani
na baraka tele.
Ni kwa utukufu huo sote tunaomsadiki Kristo tunatumwa sasa
kutangaza habari njema ya ufufuko. Na popote tulipo tuwe ishara ya furaha, amani na
tumaini jema. Ni kwa utukufu huo sisi nasi tunafanywa kuwa baraka kwa watu wengine,
kwani tumefanywa kuwa uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu na watu wa milki
ya Mungu, tuliyoitwa ili tupate kuzitangaza fadhili za Bwana, aliyetutoa gizani (Rej.
1Pet. 2:9). Kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.