2014-05-11 09:10:45

Waamini walei waliojiweka wakfu kwa Kristo na Kanisa lake ni wana mapinduzi!


Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza na kuwashukuru waamini walei wanaojisadaka kwa kujiweka wakfu mbele ya Kristo na Kanisa lake na kwa njia hii wanakuwa ni wana mapinduzi wa kweli kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayomwilisha upendo wa Mungu kati ya watu.

Baba Mtakatifu ameyasema hayo, Jumamosi tarehe 10 Mei 2014 alipokutana na kuzungumza na Baraza la Waamini Walei waliojiweka wakfu nchini Italia. Baba Mtakatifu amesema, ilikuwa ni tarehe 2 Februari 1947 wakati Papa Pio XII alipoandika Waraka wa kichungaji ujulikanao kama "Provida Mater Ecclesia" ulioliwezesha Kanisa kuanzisha miundo mbinu ya kitaasisi kwa ajili ya Mashirika ya Waamini walei waliokuwa wanajiweka wakfu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hili lilikuwa ni tukio la kishupavu lililofanywa na Papa Pio XII kwa wakati ule.

Tangu wakati huo, Waamini walei waliojiweka wakfu kwa Kristo na Kanisa lake wamekuwa ni msaada mkubwa kwa Kanisa, kwani wametumia muda wao binafsi kwa ajili ya kutafakari, kusali pamoja na kushiriki katika utume na maisha ya Kanisa wakiendelea kuwa uraiani bila kufungwa na maisha ya kijumuiya au utume maalum kama ilivyo kwa watawa!

Kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao anasema Baba Mtakatifu, wanaendelea kushiriki katika mambo ya kisiasa, kiuchumi, elimu na maisha ya kifamilia na kwa njia hii wanashiriki kikamilifu katika wito wa kuyatakatifuza malimwengu kwa kuendelea kuwa ni chachu ya imani, matumaini na mapendo kati ya watu.

Katika kiini cha maisha ya mwanadamu: changamoto za jamii mchanganyiko, ndiyo kauli iliyokuwa inaongoza mkutano mkuu wa Baraza la Waamini Walei waliojiweka wakfu nchini Italia. Huu ndio utume wa kinabii unaotekelezwa na waamini hawa, kwa kuwaonjesha watu upendo wa Mungu anayeokoa; anayetibu na kuganga majeraha ya maisha ya mwanadamu kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, mwaliko wa kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani pamoja na kuishi na watu wengine.

Baba Mtakatifu katika hotuba aliyowakabidhi wanachama hawa anawakumbusha kwamba, Italia ni nchi ambayo ina idadi kubwa ya Mashirika ya Waamini walei waliojiweka wakfu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, chachu ya imani, matumaini na mapendo kwa wale waliokata tamaa. Maisha yao ni ushuhuda wa kinabii kati ya watu, unaopaswa kujikita katika ari na mwamko mpya wa Kimissionari unaowasukuma kuwaonjesha wengine imani na furaha ya kukutana na Yesu, bila kuelemewa na ubinafsi.

Baba Mtakatifu anawahimiza waamini hawa kufanya tathmini ya kina kuhusu utambulisho wao kama Jumuiya inayowawezesha kukutana na Mwenyezi Mungu, kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu na uvumilivu, ili kushuhudia maisha yao kati ya watu wanaoishi nao, jambo ambalo linaweza kuwa kweli ni zawadi kubwa kwa nchi husika na Kanisa katika ujumla wake.

Watambue kwamba, wao ni matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa, mwaliko wa kuwaendea watu wengi zaidi, kwa kuwa alama ya maskini kwa ajili ya maskini, lakini wakiwa na moyo unaowaka mapendo, waendelee kufanya hija ya ushuhuda wa maisha na tunu msingi za Kikristo unaojikita katika furaha.







All the contents on this site are copyrighted ©.