Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais
wa Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na Padre Antonio Spadaro, mkurugenzi mkuu
wa Jarida la "Civiltà Cattolica" wameshiriki kujibu maswali ya waandishi wa habari
Jumamosi, 10 Mei 2014 katika Onesho la Vitabu Kimataifa mjini Torino, Kaskazini mwa
Italia.
Kimsingi wamezungumzia kuhusu mchakato wa mawasiliano unaofanywa na
Baba Mtakatifu Francisko pamoja na azma yake ya kutaka kufanya mabadiliko makubwa
katika Sekretarieti ya Vatican mintarafu ushauri uliotolewa na Makardinali wakati
wa mikutano yao elekezi.
Anasema, Jamii nyingi zinaendelea kukumbwa na saratani
ya rushwa inayopenyeza mizizi yake katika medani mbali mbali za maisha, kumbe kuna
haja kwa Jamii kuendelea kuwa macho na makini kupambana kufa na kupona na vitendo
vya rushwa vinavyodhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Mabadiliko yanayotekelezwa
na Baba Mtakatifu ni kuhakikisha kwamba, Sektretarieti ya Vatican inatekeleza dhamana
yake kadiri ya mahitaji ya Kanisa la Kiulimwengu, kwa kutambua kwamba, uongozi ni
huduma.
Licha ya watu kutumia diplomasia na mbinu mbali mbali za uongozi, lakini
Baba Mtakatifu Francisko ameamsha dhamiri za watu, anaendelea kuwajengea watu imani,
matumaini na mapendo thabiti, licha ya magumu na changamoto mbali mbali zinazoendelea
kujitokeza duniani.
Kardinali Parolin anasema, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu
Francisko nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014 ina mwelekeo wa
kiekumene, ni hija ya sala na tafakari kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Hija
hii pia inagusa masuala ya kisiasa.
Ni matumaini ya Vatican kwamba, Israeli
na Palestina wataendelea na majadiliano ya amani. Kuna haja ya kuendeleza juhudi za
kusitisha vita na kujikita katika amani na upatanisho wa kitaifa nchini Syria, ambako
kuna idadi kubwa ya watu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Vita ni chanzo kikuu
cha mateso ya watu, kumbe kuna haja ya kuanzisha mchakato mpya unaojikita katika majadiliano
ya kweli, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.
Kardinali Gianfranco Ravasi
anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anaendelea kutoa changamoto
kubwa katika masuala ya mawasiliano ya kijamii, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni
wa watu kukutana, kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama ndugu.
Padre
Antonio Spadaro anasema, katika onesho la vitabu kimataifa huko Torino, watu wengi
wameonesha kiu na hamu ya kutaka kununua na kujisomea vitabu vya maisha ya kiroho.
Huu ndio mwelekeo wa soko la vitabu vingi vinavyouzika sokoni. Kumbe, ushiriki wa
Vatican katika onesho hili ni kutaka kuzima kiu ya watu katika maisha ya kiroho kwa
kuwapatia vitabu vile ambavyo roho inapenda. Watu wanapenda kumsikiliza Papa Francisko
kwani ni kiongozi anayezungumza mambo yanayogusa undani wa mtu katika Jamii mamboleo.