Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 11 Mei 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kutoa Daraja Takatifu la Upadre
kwa Mashemasi kumi na watatu kutoka Jimbo kuu la Roma. Mapadre hawa wanaitwa kushiriki
Ukuhani wa Kristo aliouanzisha kwa njia ya Agano Jipya. Akaamua kati ya wafuasi wake,
kuchagua baadhi kuwa ni Mitume, ili waendeleze utume wake binafsi kama Mwalimu, Kuhani
na Mchungaji.
Mashemasi hawa wamefikia uamuzi uliofanywa katika ukomavu, ili
kujitoa kwa ajili ya huduma kwa Kristo: Mwalimu, Kuhani na Mchungaji kwa kushirikiana
kwa dhati katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa miongoni mwa Familia
ya Mungu, Hekalu la Roho Mtakatifu. Mashemasi hawa wamewekwa wakfu ili wafanane na
Makuhani wa Agano Jipya kwa kuungana na Maaskofu wao mahalia, ili kutangaza Injili
na kuwachunga Watu wa Mungu pamoja na kushiriki katika maadhimisho ya Liturujia ya
Kanisa na hasa zaidi katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Baba
Mtakatifu amewakumbusha Mapadre wateule kwamba, wanashiriki utume wa Kristo, Bwana
na Mwalimu kwa kufundisha Neno la Mungu ambalo wao wenyewe wamelipokea kwa furaha
kutoka kwa walezi wao. Huu ni mwaliko wa kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha katika
imani tendaji: Wanapaswa kuwa waaminifu kwa Mafundisho ya Kristo ili kuwamegea Watu
wa Mungu ile furaha na ushuhuda wa maisha yanayolijenga Kanisa la Mungu.
Kama
Mapadre wataendeleza kazi ya kuwatakatifuza Watu wa Mungu na kutolea Sadaka takatifu
ya Fumbo la Pasaka linaloadhimishwa kila siku Altareni. Kwa njia ya Sakramenti ya
Ubatizo, watalijalia Kanisa watoto wapya, kwa Sakramenti ya Upatanisho, watawaondolea
waamini dhambi zao kwa kuwaonjesha huruma na upendo wa Kristo, jambo ambalo wanapaswa
kulipatia kipaumbele cha kwanza. Wawajengee watu ari na moyo wa kukimbilia kwenye
kiti cha huruma kwa ajili ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Ni wajibu
wao kuhakikisha kwamba, watu wanaingia kwa Kristo ambaye ni mlango wa huruma.
Kwa
njia ya Mpako wa wagonjwa, watawasaidia na kuwaombea wamini wagonjwa katika shida
na mahangaiko yao kwa njia ya Sala ya Kanisa, watakuwa ni sauti ya Watu wa Mungu na
kwa ajili ya ulimwengu mzima. Mapadre watambue kwamba, wameteuliwa kati ya watu kwa
ajili ya mambo ya Mungu, mwaliko wa kutekeleza utume huu kwa furaha na upendo kadiri
ya mapenzi ya Mungu na wala si kwa ajili ya kuridhisha matakwa yao! Mapadre wajitahidi
kuwa kweli ni wachungaji wema.
Mwishoni, Baba Mtakatifu anawakumbusha Mapadre
wapya kwamba, kwa kushiriki utume wa Kristo wakiwa wameungana na Askofu wao mahalia,
wajitaabishe kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo, ili waweze kuwapeleka
wote kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu. Daima mbele yao wawe na sura ya Kristo Mchungaji
mwema aliyekuja si kwa ajili ya kuhudumiwa bali kuhudumia na kutoa maisha yake ili
kuokoa wale waliokuwa wamepotea!