2014-05-11 15:05:02

Je, wewe wito wako chanzo chake nini?


Mama Kanisa anapoadhimisha Siku ya 51 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa, leo Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea ushuhuda kutoka kwa Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa pamoja na Padre John Francis Mratibu wa utume na malezi, Shirika la Wamissionari wa Mtakatifu Claret, Afrika Mashariki. RealAudioMP3

Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaita watu ili kushiriki katika kazi ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa kuwajalia neema na baraka wanazohitaji katika utekelezaji wa dhamana hii. Mwenyezi Mungu anamwita kila mtu kwa namna tofauti kabisa, kwa chambo na nyenzo pengine tofauti na mwenzake. Kuna baadhi ya watu wamevutwa na mandhari ya Seminari, maisha mazuri ya Kipadre na Kitawa; Ibada na Liturujia ya Kanisa.

Askofu Mkude anasema, yeye alivutwa zaidi kwenda Seminari Ndogo ya Bagamoyo kutokana na msisitizo uliotolewa na mwalimu wake walipokuwa shule ya msingi. Aliambiwa kwamba, Bagamoyo ni mahali pa kuwafunda vijana ili kuwa Mapadre na kwamba, Seminari ni kitalu cha vijana wenye adabu na heshima, kama ilivyokuwa inajionesha kijijini kwake. Akapenda hata naye kuhesabika kuwa ni kati ya vijana waliokuwa na adabu njema, kwa vile wamesoma Seminari Ndogo ya Bagamoyo.

Askofu Mkude anakiri kwamba, mawazo ya mwanzo hayatoshi kukomaza wito na maisha ya Kipadre, kumbe, daima kuna haja ya kuwapata watu kama Mzee Eli watakaofafanua wito huu ili kupata sura na mwelekeo kamili. Hawa ni wazazi, walimu na walezi mbali mbali. Maisha na wito wa Kipadre daima una changamoto na magumu yake, lakini una raha zake pia. Mtu akipenda kuwa Padre mwema na mtakatifu anaweza kabisa!

Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda anasema, imani na hatimaye wito wa maisha yake ya Kipadre ni matunda na sadaka ya Mama yake Mzazi pamoja na Kaka yake aliyemwonesha uzuri wa kutumikia Kanisani. Akatamani, akapenda na kujitosa kwa kusoma masomo Kanisani pamoja na kutumikia Ibada ya Misa Takatifu. Huu ukawa ni mwanzo wa wito na maisha yake ya Kipadre. Akabahatika kuchaguliwa kwenda Seminari ndogo Kahengesa, kati ya vijana 10 waliotoka Parokiani kwake, wawili tu ndio waliofaulu kwa neema ya Mungu kufikia Daraja takatifu la Upadre.

Askofu Nyaisonga anasema, aliendelea na masomo ya kidato cha V na VI katika Shule ya Sekonadri ya Sangu, Jimbo Katoliki Mbeya. Mkurugenzi wa miito Jimbo Katoliki Mbeya alikuwa karibu na kijana wake katika malezi. Baada ya kidato cha VI akishawishiwa kuendelea na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria ili baadaye aendelee na Chuo Kikuu, lakini Mkurugenzi wa miito alimtaka aende Jeshini ili baadaye aendelee na masomo ya Seminari. Akamua kwenda Jeshini na hatimaye, Seminari kuu kwa masomo ya Falsafa. Huko kaendelea na majiundo ya Kipadre, leo hii ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda baada ya kuhamishiwa kutoka Jimbo katoliki Dodoma.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa anasema kwamba, Kristo ndye mchungaji mkuu, kiongozi mwaminifu na mkweli, mtiifu na mnyenyekevu; mwingi wa upendo na huruma, changamoto kubwa kwa Mapadre kujitahidi kumuiga Yesu Kristo, Mwalimu na Bwana.

Mapadre wanapaswa kujenga na kudumisha: uaminifu, unyofu, unyenyekevu, huruma na upendo. Hizi ni tunu ambazo zinaleta mvuto na mashiko kwa waamini na hivyo kumkimbilia Kristo kwa njia ya Mapadre wake, kutokana na ushuhuda amini. Mapadre wawe ni vyombo makini vya kuwawezesha watu kumkimbilia Mungu na Kristo wake. Mapadre watambue kwamba, Kristo ni mfano na kielelezo cha kuigwa, ili kuendeleza utume na huduma takatifu ulimwenguni.

Padre John Francis Mratibu wa utume na malezi, Shirika la Wamissionari wa Mtakatifu Claret anasema, Shirika lake lilianza kuingia Afrika Mashariki kunako mwaka 1993, wanashirika wakiwa wanatokea Nigeria na hivyo wakatua nanga Jimbo kuu la Mombasa, Kenya na baadaye Wamissionari wa Claret kutoka India, walifika nchini Tanzania na wengine wakaenda Uganda. Leo hii wana mapadre 11 wazalendo ambao wako tayari kutangaza Injili ya Furaha sehemu mbali mbali za dunia kadiri ya mahitaji ya Shirika.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.