2014-05-11 15:30:14

Chanjo imeokoa maisha ya watu wengi Barani Afrika


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa kuwekeza katika chanjo ni moja ya uwekezaji wa maana zaidi na wa akili zaidi ambao mataifa yanaweza kufanya katika kuboresha afya ya raia wake na hali ya baadaye ya mataifa duniani.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa afya bora ni msingi mkuu wa ujenzi wa jamii zenye chumi bora na kuwa afya ni maendeleo. Rais Kikwete ameyasema hayo Alhamisi, Mei 8, 2014 wakati aliposhiriki katika Uzinduzi wa Azimio la Viongozi wa Afrika wa Mpango wa Chanjo za Watoto wa Afrika hadi Mwaka 2020 Unaosimamiwa na Mpango wa Pamoja wa Dunia wa Chanjo (GAVI - Alliance) kwenye Hoteli ya Transcorp Hilton mjini Abuja, Nigeria.

Azimio hilo la Mpango huo wa Immunise Africa 2020 limezinduliwa katika mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mheshimiwa Donald Kaberuka. Chini ya Mpango huo, nchi za Afrika zinapanga kutumia kiasi cha dola za Marekani milioni 700 kati ya mwaka 2016 na 2020 kwa ajili ya kugharimia chanjo zitakazonunuliwa na GAVI. Hii ni mbali na mabilioni ya fedha ambayo nchi za Afrika zitatumia kwenye maeneo mengine ya afya.

Kwenye tukio hilo, Mheshimiwa Kaberuka ameungwa mkono na Rais Kikwete, Rais Macky Sall wa Senegal na Rais John Mahama wa Ghana ambaye amewakilishwa na waziri wake wa afya. Rais Kikwete amesema kwenye tukio hilo: “Azimio tunalolitoa leo ni kauli ya kuonyesha misimamo thabiti ya viongozi wa Afrika kuwekeza zaidi katika shughuli hii takatifu. Tunafanya hivyo kwa sababu tunatambua kuwa faida za chanjo ni kubwa zaidi kuliko kuwa faida za kiafya.”

Ameongeza Rais Kikwete: “ Jamii zenye afya bora zinazaa chumi zenye afya bora. Afya ni maendeleo. Chanjo ni moja ya uwekezaji maana zaidi na wa akili zaidi ambayo mataifa yanaweza kufanya kwa kuboresha afya ya raia wake na hali ya baadaye ya mataifa yetu duniani.”

Dkt. Kaberuka akizungumza kwenye tukio hilo amesema: “Nchi zinazowekeza katika upatikanaji wa chanjo leo, watavuna matunda makubwa ya uwekezaji huo katika muda mfupi na wa kati ujao.”

GAVI Alliance ambayo ilianzishwa mwaka 2000 na ambayo Mwenyekiti wake wa kwanza wa Bodi ya Wakurugenzi alikuwa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela imesaidia kuwawezesha watoto milioni 440 kupata chanjo na kuokolewa katika hatari ya vifo.

Faida za GAVI Alliance zimekuwa wazi kabisa kwa Tanzania kiasi cha kwamba Septemba mwaka jana, 2013, Taasisi ya Bill na Melinda, moja ya taasisi zinachangia fedha nyingi katika kudumisha Mpango huo wa GAVI ilitangaza kuwa Tanzania ilikuwa imefikia lengo la Millenia kuhusu watoto na chanjo la kupunguza vifo vya watoto kwa theluthi mbili.

Mpaka sasa Tanzania imefanikiwa kuchanja asilimia 93 ya watoto wake wote na miaka miwili iliyopita, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa GAVI ambako chanjo mbili mpya zilianza kutumika nchini ikiwa nchi ya kwanza duniani kutumia chanjo hizo. Chanjo hizo ni ile ya homa ya mapafu na ugonjwa wa kuharisha.

Baadhi ya nchi duniani zinazochangia katika kugharimia GAVI Alliance ni pamoja na Australia, Canada, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, India, Ireland, Italia, Japan, Luxembourg, Uholanzi, Norway, Russia, Jamhuri ya Korea, Afrika Kusini, Hispania, Sweden, Uingereza na Marekani.

Taasisi nyingine zinazogharimia GAVI Alliance ni Umoja wa Ulaya, Mfuko wa OPEC, Bill and Melinda Gates Foundation, Lion Club International Foundation, Vodafone, Comic Relief, Anglo American, JP Morgan na taasisi nyingine nyingi. Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Algeria, Mheshimiwa Mohamed Larbi Ould Khelifa, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Mheshimiwa Michael Froman na Mwakilishi wa Kampuni ya Marekani ya General Electric katika Afrika Bwana John Rice.








All the contents on this site are copyrighted ©.