2014-05-10 08:34:52

Wajengeni watu katika umoja, utakatifu na mapendo!


Hija ya kitume inayofanywa na Maaskofu mahalia mjini Vatican inalenga pamoja na mambo mengine kuimarisha umoja, upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni nafasi ya kusali na kutafakari, ili kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Yesu Kristo, kwa ajili ya huduma ya Injili.

Ni wakati muafaka wa kufanya tathmini ya kina kuhusu maisha na utume wa Kanisa nchini Eritrea na Ethiopia, kwa kujadili furaha na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa. Hata katika utofauti wa nchi kama unavyojionesha kwa Eritrea na Ethiopia, lakini kwa pamoja wanabeba ndani mwao utajiri na huduma kwa Kanisa moja la Kristo!

Maaskofu wanahamasishwa kutangaza Injili ya Kristo, kwa kuwajenga na kuwaimarisha waamini katika utakatifu, umoja na mapendo. Ni mwaliko wa kushirikiana kwa dhati kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu inayowaka mapendo ya Kristo, jambo la kufurahisha na kujivunia kwa Kanisa nchini Eritrea na Ethiopia.

Imani inayoendelea kustawi na kushamiri katika nchi hizi ni matunda ya kazi za kimissionari, watu waliothubutu kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu, changamoto na mwaliko wa kuwa na ari pamoja na mwamko mpya wa shughuli za kimissionari, ili kuwawezesha watu kuishi na kuadhimisha vyema imani yao!

Hii ni hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Maaskofu kutoka Eritrea na Ethiopia, Ijumaa tarehe 9 Mei 2014 baada ya kuhitimisha hija yao ya kitume inayofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Anasema, dhamana ya Uinjilishaji waliyokabidhiwa na Mama Kanisa wanaitekeleza kwa kushirikiana na Mapadre wao ambao ni wasaidizi wao wa karibu, Kanisa linawashukuru Mapadre na Wamissionari, kwa kazi kubwa ya kuhubiri, kuadhimisha Sakramenti za Kanisa pamoja na utekelezaji wa matendo ya huruma, kama kielelezo cha uwepo wa Kristo kati ya watu wake.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza Maaskofu kujitaabisha katika malezi ya Majandokasisi wao, ili waweze kuwa kweli ni watakatifu na watangazaji mahiri wa Neno la Mungu, hawana budi kuendelea kuinjilishwa, kwa kukazia majiundo makini Seminarini; majiundo yanayomgusa mtu mzima, kiroho, kiakili na kichungaji; ili Mapadre wawe ni watu wa sala, wanaojisomea pamoja na kujisadaka pamoja na Maaskofu kuwaonesha kwamba, wanawajali na kuwathamini, kwa kuwa wakarimu katika kuwatekelezea mahitaji yao msingi: kiroho, kimwili na majiundo endelevu; wao wenyewe wasaidiane na kutaabikiana, ili kujenga na kuimarisha udugu, ili kutolea ushuhuda wa ufuasi wa Kikristo!

Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa Katoliki Eritrea na Ethiopia ambalo ni matunda ya ushirikiano wa watu mbali mbali, waliojisadaka hata kujenga na kuimarisha Jumuiya za Kanisa mahalia. Hawa ni wamissionari waliojitosa katika huduma kwenye sekta ya elimu, afya na huduma za kichungaji, ili kuwaonesha sura ya Kristo kwa kuishi Injili. Baba Mtakatifu anawashukuru wote hawa akiungana na Maaskofu wao pamoja na kuwahimiza Maaskofu kuendelea kuwahudumia katika mahitaji ya kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anasema, dhamana ya Uinjilishaji ni kwa Wakristo wote, changamoto kwa Kanisa kuendelea kutoa majiundo makini kwa Makatekista, Waamini walei, Vijana, ili waweze kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Kristo hasa pale wanapokabiliana na changamoto za maisha. Baba Mtakatifu anawataka waamini walei kuwasaidia vijana kufanya maamuzi makini kuhusu maisha yao hasa kutokana na ukweli kwamba, fursa za ajira ni adimu kwa wengi. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana na viongozi walei ili waweze kutekeleza wajibu wao barabara.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu pamoja na waamini walei kumtolea Kristo ushuhuda makini, kwa kusaidia kupambana na umaskini ambao kwa kiasi kikubwa ni matunda ya vita ya muda mrefu katika nchi hizi. Ushirikiano na wadau mbali mbali unaweza kuleta nafuu kwa wananchi wengi, kwa watoto wanaokabiliana na utapiamlo wa kutisha pamoja na watoto yatima.

Baba Mtakatifu anawakumbuka vijana wanaohatarisha maisha yao kwa kufunga safari za hatari ili kutafuta maisha bora zaidi, lakini wawakumbuke wazee wanaobaki nyumbani wakiteseka bila msaada. Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wao.








All the contents on this site are copyrighted ©.