2014-05-10 15:47:05

Mwilisheni kanuni maadili ili kuyatakatifuza malimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa Mfuko wa Centesimu Annus kwa ajili ya Papa kwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu katika kupambana na changamoto katika ulimwengu mamboleo kwa njia ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kukazia dhana ya mshikamano inayoongozwa na kanuni ya auni iliyofanyiwa kazi kwa namna ya pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II na kuboreshwa zaidi na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kichungaji, Upendo katika Ukweli!

Baba Mtakatifu anasema katika mikakati ya uchumi mamboleo, dhana ya "mshikamano" ni neno linalosababisha kichefuchefu kwa watu wengi na kusahau kwamba, mtikisiko wa uchumi kimataifa umesababishwa kwa kiasi kikubwa na kumong'onyoka kwa tunu msingi za kimaadili, kwa kutokuwa na ugavi sawa wa rasilimali na bila kutoa kipaumbele cha kwanza katika fursa za ajira. Umefika wakati kwa wachumi na watunga sera kumwilisha tunu hizi msingi katika mchakato wa: uzalishaji, kazi, biashara na masuala ya fedha!

Baba Mtakatifu anawapongeza wanachama wa Centesimus Annus kwa kuweka nadharia katika matendo mintarafu uzoefu na mang'amuzi yao. Wafanyabiashara wa Kikristo wanapaswa kuongozwa na kanuni msingi za Injili katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, mafao ya wengi, fursa za ajira na kazi nzuri; mambo yanayoweza kutekelezwa ikiwa kama kanuni msingi za maadili na utu wema zinazingatiwa na kuthaminiwa na wengi!

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kikristo, yaani Parokia, Jimbo, Chama cha Kitume ni mahali muafaka ambako mfanyabiashara, mwanasiasa, mtaalam au mwanaharakati anapaswa kuchota nguvu ya kuweza kujadiliana na jirani zake, vinginevyo, maeneo ya kazi yanakuwa ni magumu, kiasi cha kujenga uadui na hatimaye kutokuwa safi kwa ajili ya maisha ya kibinadamu.

Kwa kweli anasema Baba Mtakatifu, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinawapatia majaribu makubwa wafanyabiashara, changamoto ya kutowatelekeza wale wote wanaoteseka kutokana na athari hizi, kwa njia ya mshikamano na ushuhuda wa imani tendaji.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanawaalika waamini walei kujikita katika dhamana ya kuyatakatifuza malimwengu kwa kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Wanachama wa Centesimu Annus kwa njia ya msaada wa Mungu na Kanisa wanaweza kutolea ushuhuda kwa kumwilisha kanuni maadili katika ulimwengu wa wafanyakazi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema ushuhuda huu ni muhimu sana na anapenda kuwatia moyo ili waweze kusonga mbele katika imani, sala, ili kukabiliana na changamoto za kila siku. Anawaalika waamini walei kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia kipaji cha ushauri, ili waweze kufikiri na kutenda kwa ajili ya mafao ya wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka wanachama hawa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, Mama wa shauri jema.







All the contents on this site are copyrighted ©.