2014-05-10 11:47:16

Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI kutangazwa Mwenyeheri tarehe 19 Oktoba 2014


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 9 Mei 2014 amekutana na kuzungumza na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa linalowatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu na kuridhia kutangazwa kwa miujiza iliyofanywa kwa maombezi ya Watumishi wa Mungu wafuatao ili waweze hatimaye kutangazwa kuwa ni Wenyeheri:

Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI, aliyezaliwa kunako tarehe 26 Septemba 1897, huko Concesio, Italia na kufariki dunia tarehe 6 Agosti 1978 kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo.

Mtumishi wa Mungu Luigi Caburlotto, Padre wa Jimbo na mwanzilishi wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Yosefu. Alizaliwa tarehe 7 Juni 1817, huko Venezia, Italia na akafariki dunia tarehe 9 Julai 1897.

Kanisa limetambua karama za kishujaa zilizooneshwa na Mtumishi wa Mungu Giacomo Abbondo, Padre wa Jimbo, aliyezaliwa tarehe 27 Agosti 1720 huko Salomino na kufariki dunia tarehe 9 Februari 1788, huko Tronzano, Italia.

Katika orodha hii kuna Mtumishi wa Mungu Giacinto Alegre Pujals, Padre wa Shirika la Wayesuit, aliyezaliwa kunako tarehe 24 Desemba 1874 huko Terrassa, Hispania na kufariki dunia tarehe 10 Desemba 1930 mjini Barcellona, Hispania.

Kanisa limetambua ushujaa wa Mtumishi wa Mungu Carla Barbara Colchen Carrè de Malberg, Mama wa familia, Mwanzilishi wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Francisko wa Sales, aliyezaliwa tarehe 8 Aprili 1829 na kufariki dunia tarehe 28 Januari 1891, huko Lorry-les-Metz, Ufaransa.

Katika mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Kardinali Angelo Amato, Papa ameridhia kwamba, Mtumishi wa Mungu Giovanni Battista Montini atangazwe kuwa Mwenyeheri tarehe 19 Oktoba 2014, katika Ibada itakayofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.