Kila mwaka, Dominika ya nne ya Pasaka, inaitwa dominika ya Mchungaji Mwema, tungeweza
pia kuiita dominika ya “Mchungaji mzuri” kwa sababu kuna pia wachungaji wabaya wanaoweza
kuwafanya kuwa wabaya wale wanaowaongoza. Yesu ni mchungaji mzuri na wale wanaomfuata
wanaweza kuwa wazuri na wakupendeza. Kwa wakristu wa zamani hata wa siku hizi Mfano
wa Mchungaji Mwema ni mzuri sana kwa watu wote wa zamani bila kujali itikadi zao kadhali
ni mfano mzuri kwa viongozi wa dini na serikali wa leo.
Katika Biblia, Mungu
anafananishwa na mambo mengi sana, kama vile Mzabibu, Mkulima, Mfalme lakini hasa
picha hii ya Mchungaji kwa sababu imechukuliwa kutokana na mazingira ya hali halisi
ya wafugaji.
Farao mfalme wa Wamisri naye alikuwa anaitwa pia Mchungaji na
watu wake, wakati wafalme wa Israeli hawakuwa wanaitwa hivyo. Kwa sababu yawezekana
wafalme hawa hawakujionesha kuwa wachungaji wa watu wao, na badala ya kuliunganisha
taifa la Mungu wao walilitawanya, na hivi Mungu anaahidi kumtuma mchungaji mwingine,
au Yeye mwenyewe atakuja kuwa mchungaji wao.
Kama tusomavyo katika Zaburi
na katika Kitabu cha Nabii isaya: “Bwana aliwaongoza watu wake kama kondoo, akawachunga
kama kundi jangwani.” (Zab. 78:52); “Wewe uchungaye Israeli, usikie, wewe umwongozaye
Yusufu kama kundi.” (Zab. 80:1); “Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu.”
(Zab. 23:1); “Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi
mwake; na kuwachukua kifuani mwake, nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.” (Isaya
40:11).
Picha ya mchungaji inaeleweka vizuri kabisa kwa mwafrika, kwa sababu
tunayo makabila ya wafugaji, aidha kuna karibu kila familia hasa kijijini ina mfugo
fulani (lakini siyo mfugo wa wanyama wadogo wadogo kama vile chawa, kunguni na panya
wa nyumbani) bali mifugo kama mbuzi, kondoo na ng’ombe. Picha ya kibiblia ya mchungaji
ina maana ya kulisha chakula, yaani kuangalia na kutunza. Mchungaji anatakiwa awalishe
kondoo wake wote bila ubaguzi.
Mchungaji anategemewa pia kufahamu wapi kuna
malisho mazuri na kuna maji ya kunywa. Mchungaji mzuri anaweza kuitambua tabia ya
kila kondoo na kujua kondoo wanaoumwa, wanaochechemea, wadhaifu, wakorofi, wenye mbio
na walio goigoi nk. Mchungaji anategemewa pia kuelewa ishara za hatari, au za mnyama
mkali anayeweza kutokea na awe tayari kupambana na adui ili kuwatetea kondoo wake
usiku na mchana.
Katika Injili ya leo, Yesu anatumia lugha ya mafumbo iliyojaa
dharau na kwa bahati nzuri anaowafumbia lugha hiyo wanamshtukia na hivi kusababisha
mtafaruku mkubwa hadi wanafikia hatua ya kumwambia kuwa ana mapepo na mwenda wazimu,
na baadaye wanataka hata kumkamata ili kumtia ndani au labda kumrushia mawe. Hapo
yaonekana dhahiri kwamba Yesu aliwapa vidonge vikali vilivyowafanya watafakari na
wakakugundua mara moja “Fumbo mfumbie mjinga”. Hebu tuangalie Yesu aliongea nini hadi
kuwachokoza: “Amin, amin, nawaambieni, yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo…
huyo ni mwivi naye ni m nyang’anyi”. Kwa nini maneno hayo yalete uchokozi?
Ili tuweze kuelewana maana ya fasuli hii vizuri budi kwanza tulione neno hili la kiswahili
“zizi” ambalo tafsiri yake hapa imepotoshwa. Yaonekana neno hilo limefasiriwa moja
kwa moja kutoka lugha ya kiingereza “Sheephold” au kwa kilatini “ovile” yenye kumaanisha
kizizi. Kumbe, neno lililotumika katika lugha asilia ya kigiriki ni “aulen” neno
ambalo katika Biblia lingetakiwa litafsiriwe “court” na kwa kiswahili ni ukumbi, ikimaanisha
hasa ukumbi ule wa Hekalu la Yerusalemu uliokuwa umezungukwa na ukuta. Ukumbi huo
walikuwa wanaingia waamini wa kawaida ili kusali na kutoa sadaka zao. Wahusika waliokuwa
wanaianglia na kuitunza sehemu hiyo, walikuwa ni Wakuu wa kiyahudi waliohusika na
mambo matakatifu. Ikumbukwe pia kwamba, tuko Yerusalemu, ambako kabla Yesu aliwafukuza
wafanyabiashara kutoka humo hekaluni (Yoh 2:14-16).
Yesu anaposema wale wasiongia
hapo ukumbini kwa kupitia mlangoni, hao ndiyo wevi na wanyang’anyi alitaka kusema
kwamba katika ukumbi huo walikuwa waumini kama kondoo walaojisetiri au kutunzwa, nao
wanajisikia kuwa katika mazingira matakatifu, matulivu, ya amani na ya kuwasiliana
na Mungu. Hiyo ndiyo maana ya mfugo. Waumini hao wanategemea kulindwa, kutunzwa, kuangaliwa,
kutetewa na kulishwa kiroho. Kulishwa kwa maneno mazuri, mifano mizuri. Lakini hatuna
budi kuangalia pia hatari inayoweza kuupata mfugo uliofungiwa ndani bila kutolewa
nje, mfugo huo unakosa uhuru. Kumbe, yabidi kondoo watoke nje ya kizizi ili wajisikie
huru na waende malishoni wasijekufa njaa. Kondoo hao watatoka nje kwa kupitia mlangoni.
Ndiyo sasa inaingia picha ya wevi.
Hao si wengine bali hao wahusika wakuu
wa pahala hapo patakatifu (wakuu wa hekalu) waliowafungia waumini ndani ya ukumbi
wa hekalu. Humo wanawapandikiza watu mafundisho yao. Wanawaeleza juu ya mungu ambaye
anaweza kurubuniwa na sadaka zao, na majitoleo yao, na liturjia yao, na wanadaiwa
kulipa mapesa kama vile ingekuwa kumnunua Mungu, au kutungiwa sala refu wanazobidi
kuzisali la sivyo Mungu huyo atakasirika na kuwaadhibu. Kadhalika yabidi waumini kujitakasa
makosa na kujitawadha ili kuogopa adhabu ya Mungu.
Hii ndiyo dini inayoingiza
woga kwa watu. Huyo siyo Mungu kwani hakuna furaha katika kumfuata. Aina hii ya kuwaongoza
watu Yesu anaiita “Wizi mtupu!” Wevi wa aina hiyo wanaweza kuwa viongozi wa dini,
viongozi wa siasa hasahasa wa chama tawala cha wakati wa Yesu, ndiyo waliowanyonya
watu, waliowakandamiza na kuwasababishia watu mateso ya kila aina. Aina nyingine ya
viongozi wanaitwa wanyang’anyi.
Hawa ndiyo wanamapinduzi, au wakereketwa wa
dini au kwa upande wa siasa wangeitwa viongozi wa vyama vya upinzani, au wenye siasa
kali, wenye nia njema ya kutaka kuirekebisha jamii ili iwe huru na ya haki zaidi.
Viongozi hao walikuwa na itikadi mpya na nzuri, na walifanikiwa kuwarubuni watu. Lakini
kasoro yao ni kwamba walitumia mbinu potovu katika kuingiza sera zao. Yaani, walitengeneza
chuki, uhasama, walihubiri kulipiza kisasi, walipendekeza hata matumizi ya silaha.
Kuteka watu kwa mtindo huo Yesu anauita “Unyang’anyi mtupu!”
Wevi na wanyang’anyi
hao wanashikilia ukuu, uongozi, utawala na kupigiwa magoti, lakini wanawadanganya
watu. Hawa hawapiti mlangoni. Viongozi hao wanamwiba Mungu watu wake. Wanaiba furaha
zao, wanaiba hali ya kujisikia watoto wa Mungu, na hali ya kupendwa na Mungu. Wevi
ni wale wanaokufanya uwe mtumwa na usiwe huru, na hii ni picha mbaya ya Mungu. Kondoo
wanashindwa kutoka nje kwa sababu wamefungiwa ndani, ni vipofu. Wanamhitaji mchungaji
awaangaze, awafungue macho. Kutokana na sauti yake anayowaita wanafunguka masikio,
wanamtambua anawaita na kuwaongoza nje. Yesu anataka kuwafungua watu watoke nje ya
wigo huo.
Mlango ni ufahamu wetu, ni uelewa wetu. Hiyo ni nguvu aliyotupatia
Mungu ya kupambanua mambo, au ya kutambua neno la kweli, Neno la Mungu au sauti ya
adui anayetupeleka kwenye kifo. Uwezo aliotupatia Mungu wa kupambanua kati ya mwanga
na giza, kati ya kifo na uzima huo ndiyo mlango. Uwezo ule uliokuwa umedumazwa sasa
unaweza kusikia sauti ya Kristu anayefungua macho na kukufanya uutambue mlango upo
wapi ili uweze kutoka nje.
Mfungua mlango huo si mwingine bali ni dhamiri
ya mtu, anayeweza kuelewa sauti ya Mchungaji na kufungua moyo, kwa sababu anatambua
anakupeleka kwenye uhuru, kwenye maisha. Kila mmoja wetu anayo dhamiri ambayo ningeweza
kusema ni roho mtakatifu anayeweza kukuangaza uweze kupambanua sauti nyingi zinazoahidi
mambo mazuri lakini ya uwongo kabisa.
Injili inarudia sana neno hili kusikiliza
sauti. Watu wanasikiliza neno la Kristu. Anawaita kondoo wake kwa jina. Mchungaji
anamfahamu kila mmoja wetu kwa jina, hatuelewi kama kikundi cha watu. Anawaongoza
nje. Anawafungua kondoo wote na kuwaweka huru. Anawatoa watu wake kama vile alivyowatoa
toka utumwani Misri. Mambo ya ulimwengu yanatufungia kwenye wigo, tunafungwa.
Lakini
Yesu anatufungua. Kama hutoki toka ukumbi huo huwezi kuwa huru wala kuwa na furaha.
Maisha yakufungwa kwenye wigo yanakuwa ya woga, yanakuwa ya mtumwa. Wengine wanajaribu
wanajaribu kuutoroka ukumbi huo vibaya na wanajikuta wameingia kwenye ukumbi ulio
mbaya zaidi. Mmoja unaweza ukajikuta umeingia kwenye ukumbi wa mali, wa maraharaha,
wa kazi, wa uongozi, au ukumbi wa vyama vya kisiasa.
Kadhalika unaweza ukatumbukia
kwenye wimbi la mambo ya kisasa ambako watu wameridhika na kusema: “wote wanafanya
hivi”. Aidha unaweza kuingia kwenye ukumbi wa tabia yako mbovu au vionjo vyako. Hatimaye
ukajikuta bila kujitambua kwamba wewe ndiye mwizi na mnyang’anyi mkuu wa wewe mwenyewe.
Yesu
anasema: “Mimi ni mlango wa kondoo” maana yake siyo wa ukumbi mpya, bali mlango wa
kondoo ambao kondoo wanaweza kupita. Ni mlango wanapoweza kutoka, na ambapo mchungaji
mzuri wanaweza kupita vizuri katika mlango ambao ni Kristu. Anayeingia kwa njia ya
Yesu ataokoka kutoka utumwani. Yesu Mchungaji mwema anatualika kusikiliza sauti yake.
Sauti inayoweza kutusaidia kupambunua sauti mbalimbali hasa ile sauti ya wevi na wanyang’anyi.
“Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuelekeze kwenye furaha za mbinguni, kusudi sisi kondoo
wako wanyonge tufike huko alikotoka mchungaji wetu shujaa. Tunaomba hayo kwa njia
ya Kristo Bwana wetu. Amina”