Vatican yalaani utekaji nyara unaofanywa na Boko Haram nchini Nigeria
Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, vitendo vya Kikundi
cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria kuendelea kuwateka wasichana ni uvunjifu
mkubwa wa haki msingi za binadamu, ambao umekuwa ukifanywa na Kikundi hiki nchini
Nigeria.
Udhalilishaji na udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu na mbaya
zaidi kati ya watu wasiokuwa na hatia ni jambo ambalo linapaswa kushutumiwa sana na
watu wote wenye mapenzi mema. Wasichana hawa wanadhalilishwa kimwili na kiroho, vitendo
ambavyo kamwe haviwezi kuvumiliwa.
Padre Lombardi anasema, Vatican inaungana
na watu wote wenye mapenzi mema kuomba kuachiliwa mara moja kwa wasichana wa shule
waliotekwa nchini Nigeria, ili waweze kuendelea na maisha yao ya kawaida. Vatican
inaendelea kusali na kutumainia kwamba, mchango wa watu wenye nia njema utaweza kusaidia
kumaliza kabisa vitendo vya kigaidi ambavyo vimeendelea kuwa ni chanzo kikuu cha maafa
makubwa kwa watu na mali zao!