2014-05-09 07:02:46

Ushuhuda wa umoja miongoni mwa Wakristo ni hitaji muhimu!


Umefika wakati kwa Wakristo kuonesha kwa matendo matunda ya majadiliano ya kiekumene yaliyokwishafikiwa baina ya Makanisa katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, kama kielelezo cha mwanzo mpya wa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Ni wakati muafaka wa kujikita zaidi na zaidi katika hija na mshikamano miongoni mwa Makanisa. RealAudioMP3

Ni maneno ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza wakati alipokuwa anahojiwa na Gazeti la Croix linalochapishwa nchini Ufaransa wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Ufaransa, mintarafu mkutano wake na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija ya Papa kwenye Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014 kama kumbukumbu ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipotembelea na hatimaye kukutana na Patriaki Anathegoras mjini Yerusalemu.

Viongozi wa Makanisa wanataka kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja kamili miongoni mwa Wakristo, kwa kuvunjilia mbali kuta za chuki na uhasama ziliojengwa katika historia ya Kanisa ili kujenga umoja thabiti wa Kanisa kwa kujikita katika majadiliano. Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki kwa sasa yamekwishafikia ukomavu mkubwa katika mahusiano yao, kiasi cha kuweza kukutana na kujadiliana katika misingi ya ukweli na uwazi; haya ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Miaka 50 imeyawezesha Makanisa kufanya hija ya majadiliano ya Kiekumene, sasa yanachangamotishwa kutafuta maneno yatakaoyawezesha kuandika historia ya Kanisa katika umoja na utofauti wake; kwa kutambua imani moja katika Kristo na Kanisa lake, ili siku moja, Makanisa haya yaweze kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa pamoja kama kielelezo cha umoja na utume wa Kanisa. Hakuna haja kwa wakristo kuendelea kugawanyika, kiasi cha kudhani kwamba, Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa Wakristo wote ni jambo lisilowezekana kutokana na muda wa majadiliano kuwa mrefu. Umefika wakati wa kujipatanisha kwa kuwa na msimamo wa pamoja katika masuala ya kitaalimungu.

Ili kutekeleza azma ya umoja wa Kanisa, Patriaki Bartolomeo wa kwanza hapo tarehe 9 Machi 2014 ameitisha mkutano wa Viongozi wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox kukutana pamoja ili kujadili kuhusu umoja wa Kanisa unaopaswa kurutubishwa kwa njia ya Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kama kielelezo halisi cha umoja miongoni mwa Wakristo.

Utunzaji bora wa mazingira, ekolojia, mshikamano na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ni kati ya mambo msingi yanayoweza kuwashikamanisha Wakristo katika mikakati ya Uinjilishaji Mpya sanjari na ushuhuda wa Kiinjili, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano.

Mazingira ni kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu kuitunza na kuiendeleza kwa ajili ya mafao ya wengi, sanjari na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Lengo ni kusaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani kwa walimwengu, ushuhuda wa umoja miongoni mwa Wakristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.