2014-05-09 07:04:32

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili IV ya Kipindi cha Pasaka


Mpendwa msikilizaji wa kipindi tafakari masomo Dominika, tunaendelea na kipindi kama kawaida tukiwa tayari Dominika IV ya Pasaka. Katika Dominika hii tunaongozwa na sura ya 10 ya Injili ya Yohane ituambiayo juu ya MCHUNGAJI MWEMA. Bwana ndiye mchungaji mwema na anatualika nasi kuwa wachungaji wema wa taifa la Mungu.Hii ni jumapili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa. RealAudioMP3

Katika Somo la kwanza toka kitabu cha Matendo ya Mitume tunakutana na mahubiri ya Mt Petro kwa Wayahudi akiwaeleza maisha ya Yesu Kristu aliyeishi katikati yao, akifanya kazi njema na kuishi vema na kila mtu. Kisha maelezo hayo anawalaumu kwa kumsulubisha na kumweka msalabani pasipo hatia. Hata hivyo anawaambia kuwa huyu mliyemsulubisha kuwa Bwana na Kristo, ndiyo kusema amepokea taji ya utukufu toka kwa Mungu.

Mpendwa msikilizaji mahubiri haya yalikuwa makali na yalibubujika toka hekima na kisima cha Roho Mtakatifu na hivi yaliwachoma Wayahudi moyo. Wakiguswa na hilo wanamwuliza Mt Petro, tufanye nini sasa? Mt Petro anawajibu: TUBUNI MKABATIZWE kwa jina la Kristu, ili mkapate ondoleo la dhambi na mkapokee kipawa cha Roho Mtakatifu. Aidha anawaambia ahadi hii ni kwa vizazi vyote. Basi waliobatizwa kadiri ya somo hili ni watu 3000 ikimaanisha kukua kwa Kanisa la Mungu.

Mpendwa msikilizaji inawezekana ukaona kwamba pengine jambo hili liko mbali nawe kwa maana umebatizwa tayari, lakini nakuhakikishia liko karibu nawe. Daima Mama Kanisa anaweka mbele yetu Neno la Mungu ambalo daima ulisikiapo lazima likuchome moyo na likugeuze ili uishi ubatizo wako katika upya wake. Mizizi na vinyemelezi vya dhambi daima viko karibu nasi na kwa njia hiyo tunamsulubisha Bwana. Ndiyo kusema kila baada ya adhimisho la Ekaristi au Neno la Mungu yafaa kuuliza tufanye nini, Bwana anakujibu Tubuni na kuiamini Injili na hapo ndipo utakuwa mchungaji mwema (Mk. 1:15).

Katika Somo II (1 Pet. 2:20-25) Mt Petro awaalika watu, kustahimili katika maisha hata kama kuna mateso. Petro anakuja na mahubiri haya akitazama jamii yake inayomzunguka; anaona wale waliobatizwa hivi karibuni wanaweza kukata tamaa kwa maana wengine bado wako chini ya wakoloni. Aidha hakuona hatari ya kukata tamaa tu bali hata kutafsri ukristu kama mapinduzi ya kivita!

Ndiyo kusema anawaalika kujibu mateso kwa njia ya upole na uvumilivu kama Bwana alivyofanya mbele ya watesi wake. Anakazia hilo akisema “Kwa maana Kristu naye aliteswa kwa ajili yenu, hivi ni kielelezo cha uhakika, mkialikwa kufuata nyayo zake. Anaendelea kusema Bwana hakutenda dhambi na wala alipotukanwa hakurudisha matukano bali daima alijikabidhi kwa Baba yake. Aidha kwa kifo chake msalabani, alizichukua dhambi zetu, ili tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki. Kwa njia ya Kristu sisi si wa kupotea bali wa kuokoka tukimfuata Mchungaji mwema.

Mpendwa mambo haya yanatugusa moja kwa moja hivi leo, yaani tazama madhulumu yanayofanywa na viongozi wasio waaminifu katika vipindi vyao, jinsi ambavyo wanaleta hatari kwa taifa. Je tupambane nao kwa njia ya vita? Hapana; yatupasa kujadiliana nao daima tukitafuta njia ya upole na upendo. Mkristu anaalikwa daima kuingiza mbegu ya mapendo katika mazingira ya watu katika nyanja zote yaani iwe siasa au uchumi au maisha ya kawaida na toka hili watu watasema hawa hakika ni wanafunzi wa Bwana.

Mpendwa mwana wa Kanisa katika somo la III (Yn 10:1-10) tunakutana na Neno la Bwana likitualika daima kuwa wanyoofu na wakweli badala ya kufuata maisha yasiyo na utaratibu! Ndiyo kusema kuwa wachungaji wema. Katika mantiki hiyo, Mama Kanisa akiongozwa na hekima ya Mungu anachagua Dominika IV ya kipindi cha Pasaka kuwa Dominika ya Mchungaji mwema.

Tunatafakari sehemu ya kwanza ya sura hiyo ambayo inamwonesha Mchungaji mwema kwa picha ya matumizi ya mlango badala ya sehemu nyingine za zizi. Mwinjili Yohane anaendelea mbele akinukuu maneno ya Bwana kutaja sifa nyingine ya Mchungaji mwema, akisema; mchungaji lazima ajue sauti ya kondoo na kondoo wajue sauti yake.

Aidha mchungaji mwema huwatangulia kondoo wake na humfuata na kama ni mgeni hawatamfuata! Bwana akisha kuwaeleza hayo, na kwa kuwa hawakuwa wameelewa vema, alitangaza kuwa sasa yeye NDIYE MLANGO WA KONDOO na mtu akiingia kwa mimi ataokoka, ataingia na kutoka na atapata malisho ya majani mabishi yaani uhuru kamili. Mwivi huja kuchinja na kuangamiza lakini mimi nalikuja kwa ajili ya kondoo wawe na uzima tele.

Mpendwa msikilizaji yafaa kujiuliza na kufanya utafiti wa kiroho na kihistoria, hivi kwa nini Bwana anachagua picha ya mchungaji? Wakati wa enzi za Bwana wachungaji walikuwa ni watu wasioheshimika kabisa. Aidha walidharauliwa kwa sababu ya kuishi milimani na makondeni. Wachungaji hawa hawakuwa waaminifu na wema na hata mahakama hazikuamini ushahidi uliotolewa nao.

Pamoja na haya yote tunaona Bwana anawachagua wao washuhudie kuzaliwa kwake pale Betlehemu; wanakuwa ni marafiki zake wa kwanza kabisa hapa duniani! Jambo jingine muhimu, katika Palestina wachungaji walikuwa na mazoea ya kukusanya kondoo wao na kuwaweka katika zizi moja wakati wa usiku na hivi walilindwa na mchungaji mmoja wakati wengine wakilala usiku. Kila asubuhi, kila mwenye kondoo alienda pale mlangoni mwa zizi na kuanza kuzungumza na mlinzi wa usiku na kwa mazungumzo haya kondoo wake walitambua sauti yake na kujikusanya wakimzunguka. Kwa kupiga mruzi waliweza kumfuata na ilikuwa hivi kwa siku nzima. Kondoo walikuwa na uhakika na usalama bila mashaka.

Bwana ni Mchungaji mwema kwa maana analilinda taifa lake na kwa njia yake aliye mlango wote tumepata kuwa wana wa Mungu. Kwa kumwaga Damu yake tumepata kuondolewa dhambi zetu. Ndiyo kusema hakupata kutokea mwingine kabla na baada yake kwa ajili ya kazi hiyo, kumbe yeye ni pekee mlango halali wa kumwona Mungu. Huyu Kristu mchungaji mwema anajua kila sauti ya kila mmoja wa kondoo, hachukui sauti ya kundi bali sauti ya kila mmoja katika uzito wake.

Kumbe, hakuna aliye mkuu kuliko mwingine mbele ya mchungaji mwema bali sote tuna thamani ileile kadiri ya kila kipaji cha mmoja wetu. Mpendwa pamoja na kwamba kuna mchungaji mwema bado kuna mwivi ambaye huingia zizini kwa njia ya kificho! Wakati wa Bwana hawa wevi walikuwa viongozi wa kisiasa waliokuwa wakidai kujihusisha na ustawi wa watu, kumbe kinyume chake njia ya unyonyaji na dhuluma kwa watu.

Katika zama zetu hivi leo wapo watu wa namna hii, ambao daima majukwaani wanayo maneno mazuri ya kimaendeleo katika nyanja zote lakini kinachotendeka ni ufisadi na unyonyaji pindukia kiasi cha kudidimiza mataifa yao. Hawa si wachungaji wema bali ni watu wa mshahara na wanyang’anyi wanaoangamiza maisha ya wananchi.

Mpendwa msikilizaji pamoja na kwamba Bwana aijua kila sauti ya kila mmoja wetu, haiondoi uhuru wetu na wajibu wa kujitahidi kujua sauti yake. Sauti yake tunaijua kwa njia ya Neno lake, kwa njia ya Kanisa lake, kwa njia ya viongozi halali aliowaweka yeye mwenyewe na si wale wanaojiweka kwa njia ya rushwa na kampeini chafu na chafuzi dhidi ya watu halali!

Ndiyo kusema, basi kama mmoja hatahangaika ili kuitambua sauti yake itakuwa hata ngumu kuitambua siku ya mwisho wakati atakapotoa mruzi akiita waliowake kwa ajili ya kuondoka! Aidha katika maisha ya kila siku itakuwa ngumu kutofautisha sauti yake toka sauti nyingine za wahuni katika ulimwengu huu!

Mpendwa mwana wa Mungu, Kristu ndiye geiti la kuingilia, yuko pale kuweza kuruhusu nani aingie na nani asiingie zizini kwa ajili ya kuwaona kondoo. Aidha ataka kusema yeye ndiye mlango pekee wa kuingia mbinguni. Anasema wengine walionitangulia ni majizi na majangiri.

Katika hili hamaanishi manabii bali alenga kuwakemea viongozi wa siasa waliokuwa wakiwanyonya watu kabla yake na wakati wake. Ndiyo kusema wajibu wako katika maisha yako hivi leo ni kuchagua kunyonywa au kuwa huru. Kama wataka kuwa huru basi mwendee Bwana aliye mchungaji mwema, ikiwezekana kwa kuimba “Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu” Kisha kibwagizo hicho malizieni ukisema “niache niende nikamtafute daima Bwana na hivi kuachana na mizani ya kidunia!

Nikimalizia tafakari hii nataka niseme kuwa kila mmoja wetu anaalikwa kuwa mtakatifu kama Baba yetu wa mbinguni, na ili kufikia hilo lazima kuwa msamaria mwema, maskini wa roho, mwenye kufanya toba daima na kisha kuweni MCHUNGAJI MWEMA KATIKA JUMUIYA YAKO NA FAMILIA YAKO.

Nakutakieni furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe, nawe ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya kama jumuiya ya kwanza ya Waamini. Tukutane tena kipindi kijacho. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.