Majadiliano ya kiekumene yajikite katika mahangaiko ya Wakristo!
Patriaki mkuu Karekin wa Pili, Mkuu wa waamini Wakatoliki wa Armenia pamoja na ujumbe
wake, Alhamisi tarehe 8 Mei 2014 wamekutana, wakasali na kuzungumza na Baba Mtakatifu
Francisko mjini Vatican, ili kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo,
ambaye amependa Makanisa haya mawili kuendelea kushikamana, katika upendo na udugu,
kwa kushirikiana ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza
duniani.
Patriaki mkuu Karekii wa Pili amemwambia Baba Mtakatifu Francisko
kwamba, bado anaendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala.
Amemshukuru kwa ushupavu na majitoleo yake ya kichungaji, kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Kanisa Katoliki sanjari na kuendelea kuimarisha imani na tunu msingi za maisha
ya Kikristo sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi kwa kusimama kidete kulinda
na kutetea: utu na heshima ya binadamu, amani na utulivu kati ya watu.
Patriaki
mkuu Karekin wa Pili amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya utume miongoni mwa vijana, lakini zaidi kwa kuwa ni sauti ya maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni wa Jamii, mambo ambayo yanaendelea kuwahamasisha
watu kulipenda Kanisa la Kristo. Anasema, kwa upande wake, Kanisa nchini Armenia linajielekeza
zaidi katika kukuza na kudumisha uhuru, haki na amani.
Kanisa linaendelea
kuwekeza katika majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuhimiza ushirikiano
kati ya Makanisa, ili kwa pamoja kuweza kujifunga kibwebwe kukabiliana na changamoto
mbali mbali zinazojitokeza duniani.
Wakati huu nchi mbali mbali zinapofanya
kumbu kumbu ya Vita kuu vya Dunia ambavyo vimepelekea maafa makubwa kwa watu, katika
Karne ya ishirini, anasema, kuna haja ya kulaani vita inayoendelea sehemu mbali mbali
za dunia kwani ni chanzo kikuu cha umaskini na mateso na mahangaiko ya watu wanaolazimika
kuyakimbia makazi yao ili kuokoa maisha yao. Historia inaonesha kwamba, hata leo hii
bado kuna mauaji ya kimbari yanaendelea duniani.
Patriaki Mkuu Karekin wa
Pili ametumia fursa hii kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Armenia kunako
Mwaka 2015 katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja ya "dhambi kubwa" ili kusali
kwa ajili ya kuwaombea mashahidi hawa wa imani na amani na kwamba, wanatarajiwa kutangazwa
kuwa watakatifu na Kanisa la Armenia. Amemwomba Mwenyezi Mungu awaongoze katika njia
ya haki na amani, ili waendelee kutekeleza mapenzi yake, kwa sasa na kwa siku zote,
amina!