Kanisa ni Jumuiya ya watu wanaoishi Heri za Mlimani, nyumba ya maskini na wote wanaodhulumiwa!
Waraka wa Injili ya Furaha "Evangelii Gaudii" ni mwaliko kwa waamini kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa Uinjilishaji ambao ni msingi wa maisha na utume wa Kanisa. Bado
kuna haja ya kwenda nje ya mipaka iliyotolewa ushuhuda wa pekee na Wamissionari watakatifu
na wakarimu ili kushiriki katika kuimarisha miundo mbinu ya Uinjilishaji ili kuendeleza
dhamana ya Umissionari ndani ya Kanisa.
Uinjilishaji katika ulimwengu wa utandawazi
unaojikita katika mabadiliko makubwa ya kijamii, unalitaka Kanisa kuwa ni la Kimissionari
linalotoka nje ili kuinjilisha, kwa kufanya mang'amuzi ya kina kuhusu tamaduni na
mwono wa mwanadamu. Kanisa halina budi kubadilika na kujikita zaidi na zaidi kwa Kristo,
ili kutafakari pamoja na kuungana na Kristo pamoja na Roho Mtakatifu, kwa kutambua
kwamba, Roho Mtakatifu analiwezesha Kanisa kuona njia, mbinu na mifumo mipya ya Uinjilishaji.
Roho
Mtakatifu analijalia Kanisa nguvu ya kujikita katika hija ya kimissionari ili kutangaza
Injili ya Furaha, ili watu wengi zaidi waweze kuangaziwa na mwanga wa Kristo, kwa
wale waliosikia Habari Njema na wale ambao wamekataa kumkubali Yesu. Ndiyo maana Mama
Kanisa anawahamasisha waamini kutoka kifua mbele ili kuwatangazia wote Habari Njema
ya Wokovu, kwani watu wana kiu ya kusikia Injili ya Kristo! Watu wasifungwe na udhaifu
na dhambi binafsi mambo yanayoweza kukwamisha ushuhhuda na utangazaji wa Injili. Mchakato
wa kukutana na Yesu unawajalia waamini furaha ya kumtangaza Yesu kwa kila kiumbe!
Hii
ni hotuba ya iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 9 Mei 2014, kwa
Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa waliokuwa wanafanya mkutano wao
wa mwaka mjini Roma. Baba Mtakatifu anasema kwamba, Kanisa kwa asili ni la kimissionari
na linawajibika kutekeleza huduma ya upendo kwa wote na kwamba, mshikamano na udugu
ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake duniani na kwa ajili ya dunia.
Uinjilishaji
unawalenga wote, lakini kwanza kabisa hauna budi kuwafikia maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, watu wanaelemewa na mzigo wa maisha, ili kuendeleza utume wa
Yesu aliyeyamimina maisha yake, ili watu waweze kupata utimilifu wa maisha. Kanisa
ni Jumuiya ya watu wanaoishi Heri za Mlimani, nyumba ya maskini na wote wanatengwa
na kudhulumiwa; ni kwa ajili ya watu wenye njaa na kiu ya haki.
Ni jukumu
la wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kuhakikisha kwamba, Jumuiya
za Waamini zinapokea na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini pamoja na kuacha milango
yake wazi kwa wale wanataka kupata hifadhi! Mashirika haya ni nyenzo muhimu sana katika
utekelezaji wa ukarimu katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu, changamoto na mwaliko
wa kutekeleza dhamana hii kwa uvumilivu na uwajibikaji wa kimissionari. Kuna kundi
kubwa la Familia ya Mungu linalohitaji kuonja upendo wa Kristo ili kukuza ari na mwamko
wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya Uinjilishaji.
Baba Mtakatifu Francisko,
mwishoni, anawashukuru wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kwa majitoleo
yao katika huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaopania kuwaonjesha watu wote upendo
na mwanga wa Kristo. Bikira Maria awasindikize na kuwasaidia katika dhamana ya Uinjilishaji.