2014-05-09 15:12:32

Jengeni dhamiri nyofu, ukarimu na ujasiri ili kudumisha mshikamano, utu na heshima ya binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 9 Mei 2014 amekutana na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon aliyekuwa ameambana na viongozi wakuu wa taasisi za Umoja wa Mataifa mjini Vatican, waliokuwa wanakutanika mjini Roma kwa ajili ya kupanga mikakati ya shughuli za Umoja wa Mataifa.

Hili ni tukio ambalo linafanyika anasema Baba Mtakatifu siku chache tu baada ya Kanisa kuwatangaza Papa Yohane XXIII na Papa Yohane Paulo II kuwa ni watakatifu. Hawa ni viongozi waliojitosa kimasomaso kwa ajili ya maendeleo ya mtu mzima na maridhiano kati ya watu. Mtakatifu Yohane Paulo II alibahatika kutembelea makao makuu ya taasisi za Umoja wa Mataifa huko New York, Geneva, Vienna, Nairobi na Aia.

Baba Mtakatifu anawashukuru wakuu wa taasisi za kimataifa kwa kusimama kidete kudumisha amani, heshima na utu wa binadamu; ulinzi na utetezi wa watu, hasa maskini pamoja na kuendelea kujikita katika uwiano wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kati ya watu.

Matokeo mazuri ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa Mwaka 2015 hasa katika sekta ya elimu ni kielelezo tosha kabisa cha kazi zinazoratibiwa na Baraza la wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyoko chini ya Umoja wa Mataifa. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, watu bado wanadai na kutamani matunda bora zaidi.

Baba Mtakatifu anawahimiza kuendelea kujibidiisha katika mchakato wa kuwaletea watu maendeleo endelevu katika medani mbali mbali za maisha na kwamba, kinachokosekana kwa sasa katika mikakati ya kiuchumi na kisiasa ni binadamu kuendelea kuwekwa pembeni, kiasi cha kushindwa kufaidika zaidi na mikakati hii.

Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa siku za usoni hayana budi kupangwa kwa kuzingatia ukarimu na ujasiri, ili yaweze kusaidia kupambana na miundo inayosababisha: umaskini, njaa pamoja na kuwajengea watu uwezo wa kutunza mazingira, kupata fursa za kazi nzuri pamoja na kulinda familia, tunu msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu kiuchumi na kijamii.

Hapa lengo liwe ni kupambana kufa na kupona na uchumi unaowatenga watu, utamaduni usiojali mahangaiko ya watu pamoja na utamaduni wa kifo mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kupokelewa bila upinzani.

Baba Mtakatifu Francisko amewasimulia kisa cha Zakayo tajiri aliyekutana na uso angavu wa Yesu, akaguswa kutoka ndani mwake, akaamua kuongoka na kukumbatia haki jamii, changamoto ya kufanyiwa kazi katika utekelezaji wa mikakati ya kisiasa na kiuchumi, kwa kuwa na dhamiri nyofu inayowasaidia wanasiasa kujenga ukarimu na ujasiri wa kumwilisha moyo wa mshikamano; kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu; kwa kuenzi Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu amewakabidhi binadamu.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuibua sera na nadharia za kiuchumi na kisiasa kwa kujikita katika ukarimu na mahitaji ya binadamu kwa ajili ya kumhudumia mtu kikamilifu kama alivyofanya Zakayo alipokutana huruma ya Yesu. Baba Mtakatifu akifuata mawazo ya watangulizi wake anasema kwamba, maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanayojikita katika usawa yanaweza kupatikana ikiwa kama watu watazingatia mshikamano usiojikita katika ubinafsi katika hatua mbali mbali, kwa kusaidia kujenga na kudumisha maendeleo ya wengi, pamoja na ugavi bora zaidi wa mafao ya kiuchumi unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta umma na ile ya watu binafsi

Baba Mtakatifu anaendelea kuwatia shime viongozi wakuu wa Umoja wa Mataifa katika mkutano wao wa kuratibu shughuli za Umoja wa Mataifa kwamba, hii ni huduma kwa binadamu wote, inayohitaji maadili yanayovuka imani na maoni kwa kuzingatia mambo msingi yaani udugu na mshikamano hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Amewatakia neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili yao na familia zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.