Vatican na Uturuki kuendeleza majadiliano ya kidini
Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, Alhamisi tarehe 8 Mei 2014 limefanya mkutano
na ujumbe wa Rais kutoka Uturuki unaoshughulikia masuala ya kidini (Dyanet), ili kuangalia
uwezekano wa pande hizi mbili kushirikiana kwa karibu zaidi, kama ilivyokuwa imependekezwa
kunako mwaka 2002.
Mwezi Septemba, 2012, viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa
la majadiliano ya kidini walikutana na ujumbe kutoka Uturuki, ili kuangalia na kuweka
mikakati ya utekelezaji wa maazimio yaliyokuwa yamefikiwa katika hatua za awali. Mwezi
Mei, 2013, ujumbe kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, ulitembelea Uturuki
ili kufafanua mambo msingi ambayo pande hizi mbili zingependa kushirikiana. Mkutano
uliofanyika mjini Vatican, imekuwa ni fursa ya kutathmini uhusiano wa pande hizi mbili
katika mchakato wa majadiliano ya kidini.