2014-05-08 15:12:55

Ungameni imani na kuimwilisha katika matendo pamoja na kuitolea ushuhuda angavu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi tarehe 8 Mei 2014 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu pamoja na sala kwa ajili ya kuombea huruma na amani kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, Napoli, Kusini mwa Italia.

Katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kufanya toba na wongofu wa ndani changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Petro kwa Wakristo wa kwanza, ili kuanza kufanya hija katika maisha mapya yanayojikita katika imani inayomwilishwa katika matendo, kama alivyofanya Mwenyeheri Bartolo Longo. Alisali na kutafakari kuhusu umaskini, ukosefu wa haki msingi za binadamu kwa namna ya pekee alionja na kugundua kwamba, utu na heshima ya mwanadamu vilikuwa havipewi kipaumbele cha kwanza.

Kardinali Parolin anasema, upendo unakoleza matumaini na kuanzisha mchakato wa maisha mapya, hata kama binadamu ataendelea kukabiliana na shida na mahangaiko ya ndani kama vile uvunjifu wa haki msingi za binadamu, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Waamini wanapaswa kujikita katika matumaini na utulivu wa ndani pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika matendo!

Kardinali Parolin anakazia umuhimu wa waamini kukiri imani yao na kuendelea kushikamana kama walivyokuwa Mitume na Bikira Maria, kwa ajili ya kutangaza, kujenga na kushuhudia ufalme wa Mungu pamoja na kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Injili kama alivyofanya Bikira Maria, mtumishi mnyenyekevu wa Bwana na Mama wa Imani. Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei ni kielelezo cha mahangaiko na furaha ya watu; imani na matumaini; mwaliko kwa waamini kumwangalia Kristo, ili kumtolea ushuhuda wa kweli kwa kushiriki katika utume wa Kanisa.

Kardinali Parolin anawataka waamini kuishuhudia imani yao ili iweze kuzaa matunda kama alivyofanya Mtakatifu Petro, kwani hata karne ya ishirini na moja, kuna Wakristo wanaoendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao. Ni watu wanaopaswa kuombewa ili waweze kuwa imara na kamwe wasikate tamaa, ili hatimaye, waweze kumwilisha imani yao katika utimilifu.

Kardinali Parolin anasema, imani inapaswa kumwilishwa katika matendo kwa njia ya mapendo kwa jirani, kama kielelezo makini cha utekelezaji wa amri mpya ya mapendo kwa Mungu na jirani. Mwenyeheri Bartolo Longo, mwamini mlei, alijitahidi kumwilisha imani katika matendo kwa njia ya mapendo kwa jirani zake pamoja na kujiaminisha katika huruma ya Mungu. Sala ya Rozari Takatifu yakawa ni matofali ya ujenzi wa Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, nyumba ya sala na matumaini kwa watu wapya.

Kardinali Parolin anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mwanga wa dunia kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa unaojikita katika kutangaza Injili ya Furaha na kuishuhudia kwa njia ya matendo, baada ya kukutana na Yesu Mfufuka ambaye amejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Haya ndiyo mambo msingi katika imani ya Kikristo inayoungamwa na kumwilishwa katika mapendo kwa Mungu na jirani pamoja na kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa njia ya ushuhuda angavu wa maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.