Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 51 ya Kuombea Miito Mitakatifu!
Neno la Mungu linasema kwamba, Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji,
akifundisha katika masinagogi yao, na kuhubiri Habari Njema ya Wokovu, na kuponya
magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano aliwahurumia, kwa sababu
walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Ndipo alipowaambia
wanafusi wake “mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache”.
Baba Mtakatifu
Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 51 ya Kimataifa kwa ajili ya Kuombea Miito
Mitakatifu inayoadhimishwa, tarehe 11 Mei 2014, Jumapili ya Kristo mchungaji mwema,
inayoongozwa na kauli mbiu “Miito, ushuhuda wa ukweli” anasema, sehemu hii ya Maandiko
Matakatifu inashangaza kwani kabla ya kupata mavuno mengi kuna haja kwanza kabisa
ya kutayarisha shamba, kupanda na kulitunza, lakini kazi hii kubwa ndani ya Kanisa
inafanywa na Mwenyezi Mungu na kwamba, shamba linalozungumzwa na Kristo ni mwanadamu,
yaani ni Wakristo.
Mwenyezi Mungu ndiye kiini cha mavuno mengi kutokana na
neema na umoja unaojionesha kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake. Yesu anawaalika wafuasi
wake kuomba ili watendakazi waweze kuongezeka katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hawa
ndio “washiriki wa Mungu” wanaojitosa kimasomaso kwa ajili ya Injili ya Kanisa.
Kwa
mtu aliyeguswa na neema ya Munguinayookoa kama ilivyokuwa kwa Mtume Paulo anatambua
kwamba, chemchemi ya miito yote mitakatifu ndani ya Kanisa ni neema kutoka kwa Mwenyezi
Mungu na kwamba, waamini wenyewe ndilo “shamba la Mungu”. Hii ni kazi inayoweza kufanywa
na Mwenyezi Mungu peke yake kwa kuonesha moyo wa shukrani kwa njia ya upendo na hatimaye,
kumwabudu Mungu kutokana na matendo yake makuu aliyomkirimia mwanadamu, jambo ambalo
anasema Baba Mtakatifu linahitaji uhuru wa mtu binafsi.
Waamini mara nyingi
sana wamesali na kuimba kwamba, wao ni mali ya Mungu, watu na kondoo wa malisho yake
na kwamba, Mwenyezi Mungu amemchagua Yakobo na Israeli kuwa mali yake mwenyewe. Kwa
hakika waamini ni mali yake Mungu si kwa vile anataka kuwafanya kuwa watumwa la hasha!
Lakini wanaunganishwa na Agano la milele na kwamba, upendo wake wadumu milele. Nabii
Yeremia anawakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu anachunga wito wa kila mtu ili
Neno la Mungu liweze kutimia ndani mwake kama ufito wa mlozi, kielelezo cha maisha
mapya. Kila kitu kinatoka kwa Mwenyezi Mungu ni ni zawadi ya Mungu kwa waja wake:
dunia, maisha, kifo, hali ya sasa na ile ijayo na Mtume Paulo anawakumbusha waamini
kwamba wao ni Wakristo na Kristo ni wa Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema
waamini ni mali ya Mungu kutokana na uhusiano wa pekee walionao na Kristo unaojikita
katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia kuwa na maisha mapya. Kristo anaendelea
kuwaongoza wafuasi wake, wao wanapaswa kumwamini na kumpenda kwa moyo, akili na nguvu
zote. Kila wito unamchangamotisha mwamini kufanya hija inayomwondoa kutoka katika
ubinafsi wake, ili kujishikamanisha na Yesu pamoja na Injili yake.
Waamini
wanapaswa kufikiri na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu, iwe ni katika wito wa maisha
ya ndoa na familia, maisha ya kuwekwa wakfu au wito wa kipadre. Hii ni safari inayomwezesha
mwamini kumwabudu Kristo kwa njia ya huduma makini kwa Kristo pamoja na jirani. Kumbe,
waamini wote wanaalikwa kumwabudu Kristo kutoka katika undani wa mioyo yao sanjari
na kuacha nafasi kwa neema inayofumbatwa katika Neno la Mungu, ikue na kuwaletea mabadiliko
katika huduma makini kwa jirani.
Baba Mtakatifu anasema, waamini hawana haja
ya kuwa na wasi wasi kwani Mwenyezi Mungu anafuatilia kwa ukamilifu kazi ya mikono
yake na katika kila hatua ya maisha na kamwe hawezi kuwatelekeza! Yesu moyoni mwake
anataka kutekeleza mpango alionao juu ya maisha ya kila mwamini na anataka kutekeleza
mpango huu kwa kuzingatia utashi na ushiriki wa kila mwamini.
Papa Francisko
katika ujumbe wake kwa Siku ya 51 ya Kuombea Miito Mitakatifu anaendelea kusema kwamba,
hata leo hii Kristo anaishi na kutembea katika uhalisia wa maisha ya waamini wake;
anafanya hija na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; anaponya magonjwa
na kuendelea kutembea na wagonjwa. Baba Mtakatifu anawalika waamini kusikiliza kwa
makini sauti ya Kristo ili kutambua ni wito gani ambao Mwenyezi Mungu anawataka kuuishi,
kwani maneno yake ni roho na maisha; wawe tayari kutenda kila jambo ambalo Kristo
anawaambia.
Waamini wanachangamotishwa kufanya hija ya kijumuiya, ili kupata
nguvu inayohitajika. Wito ni tunda linaokomaa katika shamba lililotayarishwa vyema
katika upendo unaomwilishwa kwenye huduma na katika uhalisia wa maisha ya Kanisa.
Hakuna wito unaozaliwa katika ubinafsi na kwa ajili ya masuala binafsi. Wito unabubujika
kutoka katika moyo wa Mwenyezi Mungu na kukua katika watu waaminifu na wanaoonja upendo
wa kidugu na kwa njia ya ushuhuda wa maisha na upendo wa kidugu, watu wengine wanaweza
kuwatambua kwamba, wao kwa hakika ni wafuasi wa Kristo.
Baba Mtakatifu anasema
kwamba, hii ni changamoto inayowataka waamini wakati mwingine kufanya maamuzi magumu
kwani wanaweza kukutana na vizingiti ndani na nje ya maisha yao, wanavyopaswa kuvishinda,
kwani wakati mwingine Neno la Mungu linaweza kupokwa na Shetani; mahangaiko ya ndani,
hali ya kukata tamaa pamoja na vishawishi vya malimwengu. Mambo haya yanaweza kuwakatisha
wengi tamaa kwa kutafuta njia ya mkato, lakini waamini wanakumbushwa kwamba, furaha
ya kweli inabubujika kutoka katika imani kwa Yesu Kristo ambaye ni mwaminifu na kwamba,
waamini wanaweza kufanya hija pamoja naye na kuwa kweli ni wafausi na mashahidi wa
upendo wa Mungu kwa kufungua mioyo kwa mambo makuu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hii
ndiyo changamoto kwa Wakristo.
Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu, Mapadre,
Watawa, Jumuiya na Familia za Kikristo kuhakikisha kwamba, wanashiriki kuelekeza miito
mitakatifu katika utakatifu wa maisha, kwa njia ya mifano bora na maisha adili yak
ila mwamini. Vyama vya Kitume na watu binafsi wajitahidi kutoa msaada wa mali na mali
kwa watu wanaojisikia kuwa na miito mitakatifu.
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha
Ujumbe wake wa Siku ya 51 ya Kimataifa ya Kuombea Miito kwa kuwataka waamini wote
kujitahidi kuwa ni udongo mzuri kwa ajili ya kusikiliza, kupokea na kulimwilisha Neno
la Mungu, ili liweze kuzaa matunda ajaa! Waendelee kujishikamanaisha na Kristo kwa
njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti nyingine
zinazoadhimishwa na Mama Kanisa, kwa njia ya mshikamano wa kidugu.
Kwa njia
hii, furaha ya kuwa ni wadau wa Mungu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita
katika huruma na ukweli; haki na amani itaongezeka maradufu. Mavuno yatakuwa mengi
kadiri ya neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa njia ya unyenyekevu, kila mwamini
ataweza kuipokea zawadi hii moyoni mwake.
Ujumbe huu umehaririwa na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.