2014-05-08 12:23:08

Uinjilishaji unajikita katika unyenyekevu, majadiliano na imani kwa neema ya Mungu!


Wahudumu wa Sakramenti za Kanisa wanapaswa kutoa nafasi ya neema ya Mungu kutenda kazi kati ya watu na wala wasiwe ni kikwazo kwa kuweka urasimu usiokuwa na mashiko. Ikumbukwe kwamba, kazi ya Uinjilishaji inatekelezwa na Mwenyezi Mungu.

Kumbe, waamini hawana budi kupewa nafasi ya kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti pamoja na kuendelea kujikita katika unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, kwa kukuza na kudumisha majadiliano pamoja na kuwa na imani thabiti katika neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao!

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 8 Mei 2014, kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Anasema, Neno la Mungu linamwonesha Filipo alivyokuwa msikivu kwa Roho Mtakatifu, kiasi cha kuacha yote na kwenda kuinjilisha kwa njia ya majadiliano ya kina kati yake na Malkia wa Kushi kama inavyosimuliwa katika Kitabu cha Matendo ya Mitume, kiasi kwamba, Malkia akaweza kufahamu Maandiko Matakatifu na hatimaye, akabatizwa.

Baba Mtakatifu anasema, Uinjilishaji unajikita katika majadiliano na watu wanaopaswa kuinjilishwa na wala si kupoteza muda kama wengi wanavyodhani. Watu wafundishwe kweli za Kiinjili, ili waweze kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mungu aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo.

Neno la Mungu, liliweza kumkirimia neema na wongofu wa ndani, kiasi hata cha Malkia wa Kushi kutamani kubatizwa, hii ikawa ni chemchemi ya imani inayowakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye mhusika mkuu katika azma ya Uinjilishaji, wengine ni vyombo anavyotumia kutekeleza dhamana hii.

Mambo makuu yanayohitajika katika mchakato wa Uinjilishaji anasema Baba Mtakatifu kwanza kabisa ni: unyenyekevu, majadiliano pamoja na kutumainia neema ya Mungu inayofanya kazi katika maisha ya watu. Inasikitisha kuona kwamba, hata ndani ya Kanisa kuna baadhi ya watu wanaweka vikwazo vinavyowazuia waamini kuchota neema na baraka kutoka katika Sakramenti za Kanisa!







All the contents on this site are copyrighted ©.