2014-05-08 15:10:12

Damu ya mashahidi imekuwa ni chemchemi ya umoja wa Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 8 Mei 2014 amekutana, akazungumza na kusali pamoja na Patriaki mkuu Karekini wa Pili, mkuu wa waamini Wakatoliki wa Armenia, aliyechaguliwa kunako mwaka 1999. Ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Kitume la Warmenia wapatao millioni sita walioenea sehemu mbali mbali duniani, ili kujenga na kudumisha udugu.

Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na ushirikiano na umoja kati ya Makanisa haya mawili, mambo ambayo yameendelea kuimarishwa katika miaka ya hivi karibuni kwa hija ya kichungaji iliyofanywa na Papa Yohane Paulo II, kunako mwaka 2001 pamoja na Patriaki mkuu Karekin wa Pili alipomtembelea Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2008 na Papa Francisko alipoanza kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, mwaka 2013.

Papa Francisko amekumbushia matukio makuu ya kiimani yaliyomshirikisha Patriaki mkuu Karekin II, kama vile: ushuhuda wa imani katika karne ya ishirini, tukio ambalo lilikwenda sanjari na maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, wafuasi wa Kristo sehemu mbali mbali za dunia wameendelea kumwaga damu, pengine kuliko hata ilivyokuwa kwenye Karne za mwanzo mwanzo wa Kanisa na kwamba, katika matukio kama haya, Warmenia wanayo nafasi ya heshima.

Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Patriaki mkuu Karekin II kwa kukumbatia Fumbo la Msalaba katika maisha na utume wake, hali inayoonesha jinsi ambavyo waamini wa Armenia walivyoyamimina maisha yao kwa kushiriki katika mateso ya Kristo. Ushuhuda huu wa imani thabiti kamwe haupaswi kusahaulika.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mateso na madhulumu ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia yamesaidia mchakato wa umoja miongoni mwa wafuasi wa Kristo, kiasi kwamba, damu ya mashahidi hawa imekuwa ni chemchemi ya umoja wa Kanisa. Haya ni majadiliano ya kiekumene katika mateso na ushuhuda, changamoto kwa Wakristo kujikita katika hija ya upatanisho kati ya Makanisa kwa kujiachilia chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu.

Hii ni dhamana wanayopaswa kuitekeleza kama shukrani za dhati kwa Wakristo walioteseka, kiasi kwamba, mateso yao yamekuwa ni kielelezo cha wokovu kwani wameshiriki pia mateso ya Kristo. Papa Francisko anampongeza Patriaki mkuu Karekin II kwa jitihada zake za kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na matunda ya kazi hii yanajionesha kwa namna ya pekee, kwa kazi iliyofanywa na Tume shirikishi ya Kitaalimungu ya Majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox kutoka Mashariki. Itakumbukwa kwamba, Armenia ndiyo makao makuu ya Tume hii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote awafarijiye katika dhiki zao zote ili nao waweze kuwafariji walioko katika dhidi za namna zote kwa faraja hizi walizofarijiwa na Mungu. Wakristo hawana budi kumkimbilia Mwenyezi Mungu kwa imani na matumaini kwa kutambua kwamba, kuna kundi kubwa la mashahidi linalowaunga mkono; waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu ili awakirimie umoja kama vile Kristo mwenyewe alivyoomba katika Sala yake ya kikuhani wakati wa Karamu ya Mwisho.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa kuombea umoja miongoni mwa Wakristo, ili siku moja, wote kwa pamoja waweze kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwamba, sala yao ya shukrani iwawezeshe kustahili kushiriki katika wokovu.







All the contents on this site are copyrighted ©.