2014-05-07 09:34:06

Onesheni ushirikiano wa dhati!


Kardinali Gerard Ludwig Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, hivi karibuni amekutana na kuzungumza na Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kutoka Marekani, LCWR, linalowakilisha asilimia 80% ya Watawa wa kike nchini Marekani, kuonesha ushirikiano wa karibu wakati wa kufanya tathmini ya kina kuhusu mafundisho tanzu ya Kanisa, utume unaotekelezwa kwa sasa na Askofu mkuu Peter Sartain wa Jimbo kuu la Seattle, Marekani.

Kardinali Muller anasema, Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Marekani linayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, linakuza na kudumisha imani na mafundisho tanzu ya Kanisa kama msingi wa maisha ya kitawa na kazi za kitume. Sheria za Kanisa na upembuzi wa kina ni mambo yanayokwenda bega kwa bega. Kwa sasa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linafanya tathmini kuhusu imani ya Kanisa.

Huu ni mwendelezo wa kazi iliyokuwa imeanzishwa na Kardinali Joseph Levada, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kunako mwaka 2012. Lengo ni kuimarisha umoja na mshikamano wa Kikanisa kuhusu uelewa na mafundisho ya Kanisa, ili watawa waendelee kugundua na kufurahia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili hatimaye, umoja na udugu viweze kutawala ndani ya Kanisa, Familia ya Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.