2014-05-07 07:48:15

Jifungeni kibwebwe kuinjilisha!


Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni kielelezo msingi cha umoja na mshikamano wa Kanisa la kiulimwengu katika huduma kwa Familia ya Mungu katika nchi za kimissionari. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kwa Kanisa anaendeelea kuhimiza ari na mwamko mpya katika shughuli za kimissionari, ili watu wengi zaidi waweze kutangaziwa Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kuna mabadiliko makubwa katika ulimwengu, hali ambayo inalitaka Kanisa kubadilika kwa kusoma alama za nyakati, kwa kutambua kwamba, kazi za kimissionari ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa.

Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni wadau wakuu katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu kwenye Makanisa mahalia, changamoto kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, mashirika haya yanayasaidia Makanisa mahalia kukua na kukomaa ili yaweze kuwajibika katika maisha na utume wake kwa kuwajibika kikamilifu katika mikakati ya Uinjilishaji. Kanisa la Kiulimwengu litaendelea kushirikiana na Makanisa mahalia katika shughuli na mikakati ya Uinjilishaji, lakini Makanisa mahalia kwa sasa hayana budi kuanza kujipanga vyema zaidi.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumatatu tarehe 5 Mei 2014, wakati wa kufungua mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa unaoendelea mjini Roma, kwa kuwashirikisha wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Anasema, Mashirika haya ni muhimu sana katika huduma ya Uinjilishaji wa watu na kwamba, kuna haja kwa Makanisa mahalia pia kushirikiana kwa dhati katika imani na mapendo.

Kardinali Filoni anakiri kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zimelitikisa hata Kanisa, kwani misaada iliyokuwa inatolewa kwa Makanisa mahali Afrika, Asia na Amerika ya Kusini, kwa sasa imepungua kwa kiasi kikubwa, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kushikamana katika kuchangia ustawi na maendeleo ya Makanisa mahalia kwa njia ya kujitegemea.

Waamini waendelee kuhamasishwa kushiriki katika huduma za kimissionari kwa hali na mali; kwa kushirikishana imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu. Waamini wajitose wenyewe na kwa njia ya sala katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu!

Naye Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa amewashukuru wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa katika utekelezaji wa utume wao kwenye Makanisa mahalia kwa kutambua kwamba, Mashirika haya ni nyenzo muhimu sana katika kupanga vipaumbele na utekelezaji wake katika mchakato wa Uinjilishaji.

Anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kutoka kifua mbele kuwatangazia watu Injili ya Furaha kwa kukazia ari na mwamko mpya wa kimissionari ndani ya Kanisa, ili kuwafikia wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: kijiografia, kiuchumi na kiutu! Wainjilishaji wanapaswa kuwa kweli ni watu wanaosheheni furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao! Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa hayana budi kuendeleza ushirikiano na mshikamano wa shughuli za kimissionari kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima!

Askofu mkuu Rugambwa anasema, kuna mabadiliko makubwa ndani ya Jamii na Kanisa katika ujumla wake, kiasi kwamba, nyakati hizi pengine ni vigumu sana kufanya kazi na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na sababu mbali mbali kwa mafano: nyanyaso za kijinsia, kashfa, mabadiliko ya sheria katika nchi mbali mbali pamoja na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Mambo yote haya yanahitaji kuwa na mabadiliko na mikakati madhubuti!

Askofu mkuu Rugambwa anasema kuna haja ya kuimarisha mawasiliano kati ya Wakurugenzi wa kitaifa na Sekretarieti ya Kimataifa; kuendeleza majadiliano katika ukweli, kusaidiana, kuheshimiana na kuthaminiana kwa kutambua kwamba, wote ni wadau katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, wanahamaishwa kufanya mageuzi makubwa, ili Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa yaweze kuwa kweli ni Familia ya Mungu inayowajibika. Amekazia pia kuhusu masuala ya ukweli na uwazi, uwajibikaji na weledi katika masuala ya fedha za Kanisa.

Mwishoni, Askofu mkuu Rugambwa amewataka Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kuwa kweli ni madaraja na viungo kati ya Makanisa Mahalia, Mabaraza ya Maaskofu, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Sekretarieti ya Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa. Makanisa mahalia kwa sasa hayana budi kujifunga kibwebwe kutekeleza wajibu wake wa Uinjilishaji na kwamba, Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima!







All the contents on this site are copyrighted ©.