2014-05-06 08:28:22

Wajengeeni wananchi wa Burundi mazingira ya amani, ushirikiano na upatanisho!


Baada ya mateso na mahangaiko ya wananchi wa Burundi yaliyotokana na mauaji ya kimbari, umefika wakati kwa Burundi kuwapatia wananchi wake mazingira bora ya utapatanisho wa kitaifa na ushirikiano mwema kati ya watu. Ni changamoto na mwaliko kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi kujikita katika ujenzi wa amani, ushirikiano na matumaini nchini Burundi, kwa kusimama kidete kupinga utengano na kuendelea kusaidia familia na vijana kutekeleza nyajibu zao.

Maaskofu wanapaswa kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kama alivyojisadaka Askofu mkuu Michael A. Courtney, Balozi wa Vatican aliyeuwawa kikatili nchini Burundi wakati akitekeleza utume wake. Umoja na mshikamano, imani, udugu na ushirikiano kati ya Maaskofu wa Makanisa mahalia na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kikolezo kikuu katika mchakato wa kutangaza Injili ya Kristo pamoja na kutekeleza mkataba wa makubaliano kati ya Serikali ya Burundi na Vatican uliotiwa sahihi kunako mwaka 2012 na kuridhiwa na pande hizi mbili mwezi Februari 2014.

Hii ni sehemu ya hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyowakabidhi Maaskofu Katoliki Burundi waliokuwa wanafanya hija ya kitume mjini Vatican, Jumatatu tarehe 5 Mei 2014. Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza Maaskofu Katoliki Burundi kujikita katika mchakato wa majadiliano na watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha, sanjari na kutolea ushuhuda na ujasiri wa imani pamoja na kweli za kiinjili zinazofafanuliwa barabara kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, wananchi wa Burundi bado wamegawanyika na madonda ya kinzani na mauaji ya kimbari bado hayajapona sawasawa, changamoto ya kutubu na kuongoka kwa kujikita katika upendo wa kidugu na msamaha wa kweli, kwa kukazia haki, amani, utu na heshima ya wote pamoja na upatanisho wa dhati, kilele cha uinjilishaji kioneshe ushuhuda wa waamini wakiokita maisha yao kwa Kristo, kama kielelezo cha imani tendaji.

Baba Mtakatifu anasema, Mapadre ni kundi la kwanza linalopaswa kuonesha wongofu wa ndani, kwa kujitosa kimaso maso kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Ni mwaliko kwa Maaskofu kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya Majandokasisi, hali inayoonesha kwamba, kuna ongezeko kubwa la miito ya kipadre na kitawa nchini Burundi.

Hawa ni watu wanaohitaji majiundo makini: kiroho, kimwili, kiutu na kichungaji. Hapa kuna haja ya kuweka uwiano mzuri katika ya shughuli za uongozi, kichungaji na maisha ya Kisakramenti, kwani haya ni mambo makuu matatu yanayotegemeana na kukamilishana anasema Baba Mtakatifu. Waseminari wajenge na kudumisha utamaduni wa majadiliano binafsi na Yesu kwa njia ya Sala, tayari kujikita katika dhamana ya kimissionari ili kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu anasema, miito ya kipadre inakabiliwa na hali tete, kumbe vijana wanapaswa kusindikizwa kwa busara katika safari ya majiundo yao ya maisha na wito wa Kipadre. Wasaidiwe na walezi ambao kweli ni mfano bora wa kuigwa, watu wanaoonesha furaha na utimilifu wa maisha ya kipadre, hali inayoweza kuwasaidia vijana kuwa na maamuzi bora badala ya kujuta baadaye.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza watawa wanaomwilisha imani yao katika matendo, hasa katika sekta ya elimu, afya na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ambao bado ni wengi nchini Burundi. Hawa ni watu wanaonesha ukarimu na mapendo ya kidugu. Maisha ya kitawa katika majimbo mbali mbali, hayana budi kupewa uangalizi maalum, ili watawa waweze kupata majiundo makini na thabiti, tayari kukubaliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi, ili waweze kuwa imara kwa ajili ya mafao ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anawapongeza waamini walei, vyama na mashirika ya waamini yanayojitosa kimasomaso kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa mahalia nchini Burundi na kwamba, kuna umuhimu wa pekee kushirikiana na kushikamana ili kweli waamini waweze kuwa ni wamissionari nchini Burundi.

Baba Mtakatifu anasema, vijana wanahitaji kupatiwa majiundo makini na endelevu kuhusu jamii na familia pamoja na kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, kwa kuzingatia ubora na umuhimu wa elimu kwa vijana wa kizazi kipya. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuwaandaa walimu bora, wachamungu wanaokita maisha yao katika Injili. Kuna haja pia ya kutoa elimu ya dini shuleni, kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kwa kufundisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, ili jamii iweze kujengeka katika msingi wa kiutu na ukweli.

Burundi ni nchi ambayo imekumbwa na vita, kinzani na kwamba, umaskini bado upo na kwamba, licha ya juhudi kubwa za uinjilishaji wa kina zilizofanywa na Kanisa, kuna haja ya kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kukazia ari, mwamko na matumaini ya kimissionari, ili kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.